
Mshambuliaji huyo anayejiongezea alama za ubora kila siku (Samatta), alifunga kwa tuta katika dakika ya 75 kabla ya mtokea benchi Roger Assale kutupia la pili akimalizia pasi ya Mtanzania huyo na kuifanya Mazembe kukamilisha ushindi wa jumla ya 4-1 na kutwaa taji la tani la michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Goli hilo lilimfanya Samatta afikishe mabao nane, hivyo kuibuka Mfungaji Bora wa Afrika na kumwongezea alama katika kinyng’anyiro cha kusaka Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba, anakuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kutwaa tuzo hiyo.
Matajiri hao wa Afrika waliwahi pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo miaka ya 1967, 1968, 2009 na 2010 wakijinyakulia dola za Marekani milioni 1.5 kwa kila taji na sasa wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya FIFA ya Klabu Bingwa duniani itakayofanyika Japan Desemba 10-20, mwaka huu.
Klabu ya USM Alger kutoka Algeria ilizawadiwa dola milioni moja kwa kufika hatua ya fainali licha ya kushindwa kufikia ndoto za kuwarithi mahasimu wao wa ligi moja, ES Setif, ambao mwaka jana waliifunga AS Vita ya DR Congo na kushinda taji la michuano hiyo mikubwa barani.
Ushindi wa 2-1 ugenini mjini Algiers katika mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita, uliipa Mazembe kujiamini zaidi katika mechi ya jana, lakini ilibidi isubiri hadi robo saa ya mwisho ya mechi ya jana kuibamiza USMA, ambayo iliwashika wenyeji katika kila idara.
Kocha wa USMA, Miloud Hamdi aliwashtua wengi baada ya kumwanzisha kipa chaguo la pili Ismail Mansouri badala ya Mohamed Zemmamouche, ambaye amecheza kwa dakika zaidi ya 1000.
Baada ya kuona mechi imekuwa sawa kwa pande zote, kocha wa Mazembe, Patrice Carteron alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili kwa mpigo, akiwaingiza Daniel Nii Adjei na Assale kuchukua nafasi za Nathan Sinkala na Solomon Asante kipindi cha pili.
CHANZO: NIPASHE
Hongereni sana samata na Uli kwa mafanikio mnayoyapata katika klabu yenu. Tunaimani mchango wenu unatokana na nidhamu na uwajibijaji wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yenu kikamilifu kwa hivyo shikeni njia hiyo hiyo mafanikio zaidi yanakuja. Mungu awabariki sana. Amin.
ReplyDelete