ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 17, 2014

Serikali,Chadema sasa jino kwa jino

  Kisa maandamano, migomo ya kupinga Bunge la Katiba
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeingia kwenye mgogoro na Serikali, baada ya kusisitiza kuwa ‘inyeshe mvua au isinyeshe’ kitafanya maandamano kama ilivyotangazwa.

Msimamo huo unaonekana kama mgogoro baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kuzuia maandamano hayo huku Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, akisema serikali kupitia vyombo vya usalama itahakikisha inasimamia amani na utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, alisema kazi iliyobakia ni kutekeleza azimio la Mkutano Mkuu wa chama hicho na kwamba jambo hilo halina mjadala.

“Kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama, siyo tamko la Mbowe (Freeman), ni tamko la mkutano mkuu wa chama chombo ambacho kimaamuzi ndicho chombo kikuu kuliko vikao vyote vya chama...sisi kama watendaji tunapaswa kusimamia utekelezaji,” alisema.

Alisema kauli ya Jeshi la Polisi ni ya kawaida kwa kuwa mara kadhaa limekuwa likizuia vyama vya upinzani kuendesha siasa jambo ambalo hawatalikubali.

“Kauli ile ya polisi ni kukurupuka baada ya kuwasikia wabunge wa CCM wakizungumza bungeni. Kwa bahati nzuri sisi Chadema hatukurupuki, tutafuata kanuni, sheria na taratibu za nchi kufanya maandamano.”

“Maandamano yatafanyika, inyeshe isinyeshe, kuche kusiche, kwa kufuata taratibu za nchi zinazoruhusu maandamano. Tamko la Mkutano Mkuu litatekelezwa na kila mwana-Chadema. Tutafanya maandamano ya amani yasiyokuwa na fujo, polisi ndio huwa wanakuja kufanya fujo kwa kuleta mabomu kwa wananchi wasio na silaha.”

Lwakatare alisema kamwe polisi haiwezi kukipangia chama hicho namna ya kufanya siasa na badala yake jeshi hilo linapaswa kusimamia ulinzi wa raia na mali zake na kazi ya siasa iviachie vyama vya siasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi, alisisitiza kuwa maandamano hayo yatafanyika na tayari ameitisha kikao cha kamati tendaji kupanga ni lini na wapi yaanzie.

“Sisi tuko imara, hatutishiki na hatutanii katika hili, vijana tuko tayari na vijana wako tayari nchi nzima na ninavyozungumza sasa hivi wajiandae kwa mapambano haya. Niwaambie tu polisi wasikubali kutumika kwa maslahi ya kisiasa,” alisema.

“Vijana tuko tayari na tutaandamana kwa sababu ni haki yetu ya kisheria, wao ndio watakaovuruga amani watakapoleta mabomu na risasi.”
Alisema wanaoleta fujo nchini ni wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliopo bungeni hivi sasa wakijadili Katiba ambayo haitaleta manufaa yoyote kwa taifa na badala yake wanapoteza fedha za umma.

Katambi alisema kisheria kama akidi isipotimia, Bunge Maalum la Katiba linakosa uhalali, hivyo kinachofanyika bungeni ni ufujaji wa fedha za umma.

MSIMAMO WA SERIKALI
Wakati Chadema ikitangaza msimamo huo, Serikali imetoa onyo kali na kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi au kuruhusu kujazwa hofu, ikisema kuwa ipo macho na kupitia vyombo vya usalama, itahakikisha inasimamia amani na utulivu.

Akitoa kauli ya serikali bungeni juzi usiku, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema hakuna mgogoro wa kisiasa nchini, lakini alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitahakikisha vinasimamia amani na utulivu.

Kauli hiyo imetolewa siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, kutangaza maandamano na migomo isiyoisha kushinikiza kuvunjwa kwa Bunge Maalum la Katiba kwa madai kwamba limekuwa likitafuna fedha za umma huku wakijua katiba haiwezi kupatikana.
“Hakuna sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi wala kuruhusu kujazwa hofu, serikali ipo macho na kupitia vyombo vya usalama, serikali itasimamia sheria na taratibu zilizowekwa.”

“Ili kuhakikisha taifa linakuwa na utulivu, kuhakikisha wananchi kwa ujumla wanakuwa na utulivu wa kufanya shughuli zao za kujipatia riziki, shughuli zao za kuchangia maendeleo ya taifa, serikali itasimamia yale ambayo tunayafanya hapa kwa kutumia katiba, sheria na kanuni. Tutahakikisha taifa hili linaendelea kuwa na utangamano,” alisema.

Alisema mchakato huo wa Katiba mpya waliutaka wenyewe na kuuridhia na pia wajumbe hao wanayo fursa ya kuwawakilisha Watanzania kufanya kazi ya kutengeneza Katiba itakayopendekezwa kwa amani na utulivu ili wananchi waipigie kura.

Alisema shughuli zinazoendelea za Bunge hilo ni halali kisiasa na kisheria na kwamba mjadala wa kutaka shughuli hizo zisitishwe zimehitimishwa rasmi na Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoketi chini ya majaji watatu katika kesi iliyofunguliwa na Saed Kubenea, kwa hati ya dharura, akipinga pamoja na mambo mengine kuendelea kwa shughuli hizo za bunge.

“Mahakama Kuu ya Tanzania leo (juzi) imesema bunge hili linaweza kuendelea na shughuli zake, kwa maana hiyo mjadala huo umefungwa rasmi hivi leo,” alisema.

Akifafanua kuhusu uhalali wa bunge hilo alisema: “Kwa ajili ya kuondoa shaka yoyote kwa wajumbe wa bunge hili na kwa wananchi wanaotutazama na kutusikiliza, napenda kuwamegeeni, takwimu tulizonazo hivi sasa.”

Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha kulikuwa na wajumbe 630 na kwamba kati ya hao waliotoka nje ya bunge hilo kwa maana ya kususia ni 130 ambao ni sawa na asilimia 21 tu ya wajumbe wote.

Alisema wajumbe waliobaki ni 500 hii ikiwa ni sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote.“Natambua wingi wa kundi la wajumbe 201, imejitokeza dhana kwamba wajumbe waliobaki humu ndani ni wa aina moja, hiyo siyo kweli.

“Kati ya wajumbe 500 walioko hapa, wajumbe wa kundi la 201 wapo 189.“Tukienda ndani zaidi kwenye takwimu wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati ya hao 125 ni toka kundi la 201,” alisema.

Alisema kwa kuangalia takwimu hizo kwa jicho lolote lile, yaani kwa jicho la wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wajumbe wa kundi la 201 ni kundi kubwa na sehemu muhimu ya wajumbe waliobaki.

Kwa upande wa Zanzibar, alisema wapo wajumbe 152 ambao kati yao 64 wanatoka kundi la 201.“Sasa kwa nini tunapenda kusisitiza takwimu hizi kwa kundi hili la 201…ni kwa sababu ya wingi wao kitakwimu, lakini pia kwa wingi huo wanawakilisha makundi yote ya taifa letu,” alisema na kuongeza: “Kwa hiyo ni dhahiri kwa namna yoyote ile waliobaki humu ndani ni wengi kwa idadi kubwa na ya uwakilishi.”

Alisema wajumbe walioamua kususia bunge hilo hawafikii hata theluthi moja ya wajumbe wote.“Hii ina maana kwamba kwa kuzingatia matakwa ya kisheria uamuzi upatikane, ufikiwe kwa maridhiano, mashauriano, kwa kushawishiana kwa hoja…wajumbe waliobaki na walio wengi wanaweza kutumia wingi wao, lakini pia wanao uhalali wa kisiasa na kisheria,” alisema.

Alisema pamoja na uhalali wa kisiasa na kisheria bado ndani ya bunge hilo kuna utaratibu wa kufikia muafaka kwa maridhiano lakini kwa upande wa wajumbe waliotoka hawakuona au kutaka kukubali utaratibu huo.

Bunge Maalum la Katiba liliitishwa na Rais Jakaya Kikwete, Februari 18, mwaka huu, na liliendelea hadi Aprili 25, kabla ya kupisha Bunge la Bajeti.

Dk. Migiro alisema kabla ya kuahirishwa kwa bunge hilo, baadhi ya wajumbe wa vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi walijitoa bungeni Aprili 16. (Vyama vingine vilivyojitoa katika mchakato huo ni DP na NLD.)

Alisema wakisusia bunge hilo walidai lilikuwa na kauli za matusi na dharau dhidi yao lakini wakafanya hivyo kwa kuwaita waliobaki kuwa ni Intarahamwe, jina ambalo alidai ni dharau kubwa kweli kweli.

TANZANIA KWANZA WATOA TAMKO
Mwenyekiti wa Tanzania Kwanza, Said Nkumba, amesema waliobaki kwenye mchakato huo wamekusudia kuwapatia Watanzania Katiba bora kwa mstakabali wa taifa.

“Tuna amini kwamba Watanzania hawatakubali kuona mchakato huu ukikwamishwa na kikundi cha watu wachache kisicho na nia njema, kinachoendelea kupandikiza mbegu za chuki na uhasama ndani ya taifa letu, tunaomba wananchi wadumishe amani katika kipindi hiki muhimu kwa maslahi ya taifa zima,” alieleza Nkumba.

Nkumba ambaye katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma jana aliambatana na Fahmi Dovutwa-Mwenyekiti wa UPDP, Augustino Mrema-Mwenyekiti wa TLP na Juma Ally Khatib-Mwenyekiti wa Tadea, alisema hawategemei Mtanzania mwenye fikra pevu, kuacha shughuli zake na kuungana na Ukawa kuandamana na kufanya migomo isiyo na tija.

Alisema Ukawa walitakiwa kuweka maslahi yao binafsi na ya vyama vyao pembeni na kutekeleza majukumu waliyoagizwa na wananchi waliowapa nyadhifa walizonazo na kwamba, waliobaki bungeni siyo wana-CCM pekee bali kuna mchanganyiko wa makundi unaoleta uwakilishi kwa jamii nzima ya Watanzania.

Imeandikwa na Restuta James; Dar, John Ngunge, Jacquelina Massano, Emmanuel Lengwa na Editha Majura, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

KANYAGA TWENDE MPAKA KIELEWEKE