Bongo Flava ni muziki wa kisasa ambao umedumu kwa miaka mingi na utaendelea kudumu zaidi na zaidi na hiyo yote ni kutokana na kuongezeka kwa mashabiki ambao idadi yao inazidi kuwa kubwa ukilinganisha na hapo awali kipindi muziki huu unaanza.
Kutokana na waendeshaji wa muziki huu, hapa namaanisha wasanii ambao wengi wao ni vijana, nawafananisha na mtoto ambaye analelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama peke yake licha ya kuwa kuna baba ambaye pengine tu hayupo tayari kumsaidia huyu mama ili mtoto apate malezi yaliyo bora yanayoweza kumfanikishia ndoto zake.
Ninapo sema wazazi wa Bongo Flava hapa nazungumzia vyombo vya habari’ ambaye ni mama wa Bongo Flava na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ambaye ni baba wa Bongo Flava.
Najua utajiuliza kwanini BASATA awe baba na vyombo vya habari viwe mama. Basata ndio wasimamizi wa sanaa nchini na ndio wenye mamlaka ya kutoa zuio la kazi yoyote ya msanii isichezwe katika media endapo hawataridhika na maudhui au maadili ya kazi hiyo na vyombo vya habari ndio wanaosupport kazi za sanaa kwa kuzifikisha kwa hadhira/jamii. Nadhani hapo unaweza kupata picha nini namaanisha katika makala hii.
Tukija kuwaangalia hawa wazazi wawili wa Bongo Flava mlezi mmoja ambaye ni ‘media house’ ndio anaonekana kuwa ana kiu ya kuona mwanaye anafika mbali japo wigo wake ni mdogo tofauti na baba ambaye ni Basata.
Vyombo vya habari nchini ndio vinawapa tumaini kubwa sana wasanii wa hapa nyumbani kwani chochote kinachotokea kwa msanii hasa katika suala zima la maendeleo/matatizo vyombo vya habari huwa vinakuwa na kipaumbele.
Mfano kwa wasanii wetu wanapokuwa katika vinyang’anyilo vya tunzo haijalishi iwe ndani ama nje vyombo vya habari lazima vitatoa support yake kwa hali na mali na tulitazamie katika upande wa pili wa matatizo. Tumeona makubwa mengi sana yakifanywa na vyombo vya habari mfano katika msiba wa Albert Mangwea,Mez B,Geez Mabovu na wengine wengi vyombo vya habari vilionesha jitihada zao na kufikia hatua hata msanii anapofungiwa kazi yake na Basata huwa vyombo vya habari vinajitahidi kutafuta suluhisho kwa kuchukua mawazo pande zote mbili ili kuleta maelewano kati ya BASATA na msanii(baba na mtoto).
Vyombo vya habari huwa haviyafanyi hayo tu kwani imefikia hatua ya kuandaa show mbalimbali na matamasha ambayo yamekuwa msaada mkubwa kwa wasanii wa Bongo Flava kujipatia kipato lakini cha kushangaza Basata(baba) huwa hawajitokezi hata kudhamini hizo show na matamasha yanayokuWa yameandaliwa na media(mama).
Basata(baba) wanaendelea kubaki nyuma hata katika kuibua vipaji vipya vya wasanii wetu ambavyo huwa vimejificha huko mitaani lakini vyombo vya habari huwa vinatumia vipindi na matamasha mfano Hawavumi ila wamo(ITV) Club Raha Leo Show (TBC1) na Fiesta (CLOUDS FM) kwa kuthamini kazi za wasanii media zimekwisha kubali mpango wa serikali kuanza kuwalipa wasanii kwa kucheza kazi zao.
Kwa upande wa Basata(baba) ambao ndio waangalizi wakuu wa sanaa nchini wamekuwa ni watu wa kutoa pongezi tu kwa vijana wetu wanaofanya vizuri na kusikika zaidi kuzungumza makosa ya kazi za wasanii. Wana umuhimu mkubwa sana lakini hawapo karibu na wasanii kama inavyotakaiwa na kwa sababu hiyo inapelekea kuwepo na uhasama wa chini kwa chini ambao ni vigumu kuja kujionesha katika jamii.
Ni ukweli usiopingika kuwa Basata(baba) wangekuwa wana uhusiano mzuri na wasanii hasa katika kuzisimamia kazi zao,kusimamia mikataba yao kama ya matangazo nakadhalika,kuzipitia kazi zao kabla hazijatoka ili migogoro ya kufungia kazi zibaki kuwa stori katika sanaa yetu na pia kuwa kipaumbele hasa kwa wasanii wanaoipeperusha bendera yetu nje ya nchi kwa kuwapa hata medani za dhahabu zitakazowapa motivation/motisha ya kujituma zaidi na kufika mbali kutokana na msaada unaotoka kwa Basata.
Niwape pongezi sana media na wasanii wote ambao wanaendelea kufanya vizuri kila mmoja kwa nafasi yake japo kuwa wote wanahitaji kutegemeana ili kuweza kuisukuma sanaa yetu kimataifa zaidi pia hata Basata(baba) nao wanahitaji pongezi pia na kwani mchango wao upo japo hawauoneshi kwa kiwango kinachostahiri.
Credit: Bossngassa.com
1 comment:
Mwandishi hana uelewa sahihi wa majukumu ya BASATA! BASATA ni regulator wa Sanaa. Sio sahihi kuifananisha BASATA na baba wa (au chombo cha kukuza) Sanaa. Sana sana majukumu ya BASATA yanaweza kufananishwa na majukumu ya referee, ambayo ni kuhakikisha kwamba kanuni za mchezo zinafuatwa; sio kutoa malezi kwa wanamichezo!
Post a Comment