ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 3, 2010

Yanga yazima ngebe za JKT Ruvu, Simba yatiwa gavana Kagera


YANGA imezidi kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wake msimu huu kwa kuilaza JKT Ruvu bao 1-0 huku Kagera Sugar ikimaliza ubabe wa Simba wa kutopoteza pointi msimu huu katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.


Bao la dakika la kwanza la Mrisho Ngassa lilitosha kuipa timu yake pointi tatu muhimu zilizoifikisha kwenye pointi 33, zikiwa 10 pungufu ya vinara Simba.


Wekundu wa Msimbazi ambao waliwasili mjini Bukoba wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya Toto ya Mwanza, Jumapili walitangulia kupata bao kupitia kwa Emmanuel Okwi kipindi cha pili kabla ya Temi Felix kumtungua Juma Kaseja kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na Juma Jabu kuunawa mpira.


Mchezo huo mkali ulifanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.


Kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, dalili za Yanga kupata ushindi zilianza kuonekana mapema baada ya Ngassa kuiandikia timu yake bao mwanzoni kabisa mwa mchezo baada ya filimbi ya kwanza.


Ngassa ambaye anachuana na Mussa Hassan Mgosi wa Simba na John Boko wa Azam kuwania tuzo ya mfungaji bora msimu huu aliungaisha wavuni kona ya Nurdin Bakari na bao hilo kudumu hadi mwisho.


Kipindi cha pili, Yanga ilianza kwa nguvu na dakika ya 49, Jerry Tegete alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuicheza krosi ya Shadrack Nsajigwa.


Vijana hao wa Kostadin Papic walifanya mashambulizi ya hapa na pale katika kipindi cha pili, lakini washambuliaji wao, Ngassa, Tegete, Kigi Makassi na Geoffrey Bonny walikuwa wakipandisha mipira bila mafanikio.


Katika dakika ya 75, beki Amir Maftah alionyeshwa kadi nyekundi na mwamuzi baada ya kumpiga kiwiko Kessy Mapande wa JKT Ruvu.


Baada ya mchezo huo, Papic aliwapongeza wachezaji wake, lakini akasema Maftah alistahili adhabu ya kadi nyekundu.


Kivutio kikubwa kilikuwa mjini Bukoba ambako Simba walioingia uwanjani dakika tatu baada ya kuingia wenyeji wao, Kagera Sugar saa 9:12, walikuwa wa kwanza kuliandama lango la wapinzani wao, lakini Okwi, Jabir Aziz na Mohamed Kijuso hawakuwa makini kila walipofika langoni tangu dakika ya kwanza.


Katika dakika ya 15, Simba walipoteza nafasi safi baada ya Mgosi kubabaika akiwa na kipa Amani Simba. Hata hivyo, Mgosi alikimbia langoni mwa Kagera na kuondoa glovu za kipa huyo na kuonyeshwa kadi ya njano.


Mashabiki wa Kagera ambao waliujaza Uwanja wa Kaitaba wakiwemo wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Kagera, wamiliki wa timu hiyo hawakuisadia timu yao kushinda zaidi ya kuishuhudia ikipoteza nafasi nyingi.


Mwamuzi wa mchezo huo, Idd Mbwana wa Shinyanga ilimbidi kutoa mfululizo kadi za njano ili kupunguza munkari wa wachezaji.


Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuelekeza mashambulizi langoni mwa wapinzani wao na katika dakika ya 46 Jerry Santo alifumua shuti kali lililotoka nje.


Dakika 10 baadaye, Okwi aliwainua mashabiki wa Simba kwa kuandika bao safi kwa kichwa, mpira uliotokana na faulo iliyopigwa na Ramadhani Chombo 'Redondo'.


Katika dakika ya 71, Felix aliisawazishia Kagera bao baada ya Jabu kuunawa mpira akiwa ndani ya 18.


Kagera ilipata pigo katika dakika ya 80 baada ya kipa wake, Amani Simba kuumia baada ya kugongana na Mgosi na nafasi yake kujazwa na Aswile Asukile.


Naye George Mketo wa Kagera Sugar itabidi ajilaumu baada ya kukosa bao la wazi katika dakika ya 85 wakati kipa Juma Kaseja akiwa ametoka golini.


Simba iliwakilishwa na: Kaseja, Jabu, Kanon, Yondani, Owino, Santo, Chombo, Jabir, Mgosi, Okwi na Kijuso/Naftal.


Kagera: Amani Simba/Asukile, Martin Ruharara, David Charles, Said Mourad, Shaaban Ibrahim, George Kavilla, George Mketo, Haruna Athuman, Temi Felix, Shija Mkina na Paul Ngwai.

No comments: