ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 16, 2010

Maiti ya dereva yakutwa na tundu

NDUGU SASA WAAMINI ALITESWA, TAARIFA YA DAKTARI KUTOLEWA LEO

UTATA umezidi kuzingira kifo cha dereva teksi anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa na polisi wa kituo cha Chang'ombe jijini Dar es Salaam, baada ya familia kudai kuwa maiti ya kijana wao imekutwa ikiwa na tundu na uvimbe kichwani.

Familia hiyo pia imesema maiti ya kijana wao, Mussa Juma, 27, pia imekutwa ikiwa imebabuka sehemu za siri, jambo ambalo linawatia mashaka ndugu.

Familia ilitoa madai hayo mara baada ya kuuchukua mwili wa dereva huyo kutokana na madaktari kumaliza uchunguzi wao wa kutaka kubaini sababu ya kifo cha kijana huyo ambaye polisi imedai kuwa alifariki wakati akipelekwa Hospitali ya Temeke baada ya kulalamika hajisikii vizuri wakati akihojiwa.

Akizungumza na gazeti hili jana Mwijuma Mzee, ambaye pia ni mjomba wake marehemu Mussa, alisema:

“Mimi kama mwanafamilia ninachoweza kukueleza ni kwamba mwili huo umekutwa na tundu sehemu ya mguu wa kushoto... sielewi limetokana na nini; uvimbe kichwani na amebabuka sehemu za siri. Hiki ndicho nilichoshuhudia na ninachoweza kukueleza."

Mzee alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo familia hiyo ina hofu kuwa ndugu yao aliteswa kabla ya kufikwa na mauti, lakini akasisitiza kuwa majibu ya awali yatakayotolewa na daktari aliyefanyia uchunguzi maiti hiyo, yatasaidia kupata ukweli wa tukio hilo.

Alisema wanatarajia kupata majibu hayo ya daktari leo na kwamba vipimo zaidi vimepelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya utambuzi zaidi.
Alisema sababu za kitaalamu za kupeleka vipimo hivyo kwa mkemia mkuu ni baada ya mwili huo kukutwa umejaa hewa na uvimbe, jambo alilosema linasababisha utata katika kupata ukweli halisi wa kifo chake

No comments: