ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 9, 2010

Al Shabab yaipiga marufuku BBC Somalia

al-Shabab
Wapiganaji wa al-Shabab wamefunga vituo vyote vya redio vinavyopeperusha matangazo ya BBC kwa njia ya FM katika miji mitano ya Somalia ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Mogadishu.
Kundi hilo pia limeamuru redio washirika HornAfrik, kusimamisha matangazo yote ya BBC.
Al Shabab inaishutumu BBC kwa kueneza kile inachodai ni hoja za wakoloni wa Kikristo dhidi ya Waislamu.
Masikitiko makubwa
Mkuu wa kitengo cha BBC kinachosimamia bara Afrika na maswala ya kimataifa, Jerry Timmins ameelezea masikitiko makubwa kuhusu hatua hiyo akisema itawaathiri zaidi watu wa Somalia.
Alisema hakukuwa na onyo lolote kutoka kwa al-Shabab kufunga vituo vya FM vinavyopeperusha matangazo ya BBC katika lugha za Kisomali, Kiarabu na Kiingereza.
Bwana Timmins amesema shirika la BBC limekuwa likitangaza kwa Kisomali kwa zaidi ya miaka 50 na kama ilivyo desturi, BBC hutoa ripoti kuhusu pande zote husika nchini Somalia ikiwa ni pamoja na al-Shabab.
BBC inawashauri wasikilizaji kufuatilia matangazo yake kwa lugha ya Kisomali kupitia kupitia tovuti ya bbcsomali.com, kwenye masafa mafupi na pia simu ya mkononi.
 

No comments: