ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 6, 2010

Karume akamilisha maghorofa


Image
Baadhi ya Wananchi wa wakiwa katika sherehe za uzinduzi wa Nyumba mpya ya Michenzani Block No 10 pamoja na kukabidhiwa funguo watu waliovunyjiwa nyumba zao. (Picha na Ramadhan Othman).

WAKATI Watanzania wakikumbuka mauaji ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume leo, mwanawe Rais Amani Abeid Karume jana alishuhudia kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa maghorofa ulioanza mwaka 1970 visiwani hapa.

“Nimekuwa kila siku nikikerwa sana kuona majengo haya yaliyoanza kujengwa na marehemu Karume hayajakamilika. Hili lilikuwa deni kubwa, na sasa nafurahi kuona limelipwa," alisema Rais Karume alipokuwa akikabidhi fungo tano kwa watu watano miongoni mwa 92 ambao walikabidhiwa maghorofa hayo kama fidia ya nyumba zao zilizobomolewa kupisha ujenzi huo.

Alisema takriban Sh bilioni 2.1 zilitumika kukamilisha ujenzi wa majengo mawili yenye vyumba 182 na kwamba wote ambao nyumba zao zilivunjwa walipewa kipaumbele kabla maghorofa yaliyosalia kupangishwa kwa baadhi ya watumishi wa vikosi vya usalama ambao walishiriki ujenzi huo.

Rais alisema maghorofa hayo yanaonesha juhudi zilizofanywa na marehemu Karume na chama cha Afro Shiraz (ASP) katika kubadilisha makazi ya watu masikini wa Zanzibar na kusisitiza kuwa juhudi hizo hazina budi kudumishwa.

Alisema Zanzibar imekuwa ikisonga mbele vizuri na Serikali ikileta mabadiliko kwa watu wake kutokana na amani na utulivu uliopo "bila amani, utulivu na mshikamano, hatuwezi kufikia malengo yetu," alisema Karume.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa maghorofa hayo yaliyoko Michenzani, ilihudhuriwa pia na mke wa Rais Mama Shadya, Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu wake, Ali Juma Shamuhuna na viongozi wengine.

Waziri wa Ujenzi, Mansour Yussuf Himid, aliuambia umati uliohudhuria hafla hiyo, kwamba kukamilika kwa majengo hayo kumetokana na juhudi za Rais Karume alizozianza mara tu alipoingia madarakani mwaka 2000.

Alisema uchaguzi wa watu waliokuwa wakistahili fidia ya nyumba zao ulikuwa mgumu, lakini walipata majina 92 halali. Baadaye Karume alijenga majengo kama hayo kisiwani Pemba na Unguja kwa lengo la kuboresha makazi

No comments: