Wednesday, August 4, 2010

Ili penzi lako linoge, epuka makosa haya!

Sina shaka rafiki zangu mtakuwa wazima wa afya njema na mchakato wa kutafuta maisha bora zaidi unaendelea. Nawashukuru wote ambao mmekuwa mkinitumia ujumbe mfupi wa maneno, waraka pepe na kunipigia simu mkinipongeza kwa kazi hii. Nasema ahsateni sana.

Hakuna shaka kwamba kila aliye kwenye uhusiano ana ndoto zake; Wapo ambao wapo kwa ajili ya kupoteza muda, wengine wakiwa na nia ya kudumu na wenzi wao wakitegemea siku moja kufunga ndoa. Hawa ndiyo ninaozungumza nao leo.

Kama ni kweli upo katika uhusiano na unapenda kuishi na mpenzi wako siku za baadaye, lazima uwe makini katika kila unalolifanya, lengo likiwa ni kukuongezea pointi za kumfanya huyo akupendaye awaze zaidi juu ya kufunga ndoa na wewe.

Hapa nazungumza na wanawake, wapo ambao wanafanya makosa tena makubwa, lakini hawajui kama wanakosea, jambo ambalo ni hatari sana. Katika mada hii, nitakuonesha makosa makubwa ambayo wanawake wengi wamekuwa wakiyafanya bila kujua kuwa wanakosea…

KUMUONESHA MPENZI WAKO HANA UJANJA!
Wanaume wanapenda kupendwa kwa dhati, kama wakiwa wamependa kweli, nao huwa na msimamo sana. Lakini hakuna kosa kubwa ambalo mwanamke anaweza kulifanya kwa mwanamke kama kumuonesha kwamba yeye hana ujanja kwako!

Amefika na hafurukuti kwa lolote. Fanya manjonjo yote lakini usijisahau. Kupendwa ni kawaida katika maisha, lakini kupendwa kwa mapenzi ya dhati ni bahati! Usicheze na bahati hiyo, kuwa makini na uoneshe mapenzi yako ya kweli, lakini siyo kumtishia au kufanya vituko vitakavyomfanya aone kabisa kwamba umemuoana ‘wa kuja’ katika mapenzi. Umenisoma rafiki?

KUMUONGELEA MWENZI ALIYEPITA
Mwanaume anapokuwa na wewe, hakuna ubishi kwamba anatambua huko nyuma ulikuwa na uhusiano na wanaume wengine, vinginevyo awe ‘amekufungua kwenye makaratasi’ mwenyewe!

Lakini hii si tiketi ya wewe kuzungumza juu ya wanaume wako waliopita. Hakuna mwanaume anayependa kusikia habari za mpenzi wako wa nyuma, kwanza, anaumia. Ila kubwa zaidi anaanza kukufikia kwamba wewe si mwanamke thabiti, kwani una msululu wa wanaume nay eye yupo kwenye historia ya cheni ndefu ya wanaume wake.

Kubwa zaidi, mwanaume anaamini kwamba, kutokana na kuzungumza kwako kuhusu wanaume waliopita (hasa kwa mbaya), siku akiachana na wewe atarajie kusemwa kwa mwenzi wako mpya, jambo ambalo hatapenda kuliruhusu litokee.

Unadhani atafanya nini ili aepukane na tatizo hilo? Unafikiri kuna njia nyingine kweli zaidi ya kuachana na wewe? Eti rafiki zangu, ipo kweli?...utaachwa!

KUWAZUNGUMZIA VIBAYA WENZAKO 
Mwanaume anapenda kuwa na mwanamke makini, anayejua thamani ya uanamke wake na thamani ya mwanaume pia. Mwanamke mwenye hekima ni yule anayechagua pia maneno ya kutoa mbele ya mpenzi wake. Kubwa zaidi katika hili, ni ile hali ya kuzungumza sana kuhusu mabaya ya wanawake wenzako.

Mathalani, kuwapa wanawake wenzako majina mabaya kama changu, Malaya, dadapoa, mhuni, mlupo na mengine yanayofanana na hayo. Mwanaume wako hatatamani kusikia kauli kama hizo, kuzungumzia kwako mara nyingi habari au tabia mbaya kuhusu wanawake wenzako, kutamfanya aanze kufikiria kuwa unapenda kuwa kama wao!

Kama sivyo, ni vyema kuchagua mambo ya kuzungumzia juu ya wanawake wenzako. Ingekuwa bora zaidi, kama ungesifia wanawake wanaovaa vizuri, wanaoheshimu waume zao, wenye tabia njema, wanaosifika mbele ya jamii n.k, kufanya kwako hivyo, kutamfanya mwenzi wako aone kuwa unatamani kuwa kama wao.

KUTOKUWA NA STAHA
Kupenda kumshika kimahaba, kumkumbatia au kuwa naye kimapenzi zaidi mbele za watu, kunamfanya mwenzi wako aone kama umepungukiwa tabia njema. Kwa tafsiri ya haraka, ataona kuwa hujiheshimu.

Kawaida (hasa kwa mila za Afrika), mambo ya mapenzi huwa ya faragha zaidi. Kujionesha mbele za watu mkifanya mambo yanayoashiria mapenzi, kunawapunguzia heshima na pengine mtaonekana kama wahuni tu, na siyo wenzi wenye mnaotumia akili wenye ndoto njema za baadaye. 
Nafasi yangu ni ndogo, kwa leo nasihia hapa, wiki ijayo tutaendelea. Ahsanteni sana kwa kunisoma. 

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake