Sunday, August 29, 2010

Makamba ajivua lawama sakata la uraia wa Bashe


                                                    Hussein Bashe
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuf Makamba, amesema kama aliyeenguliwa kugombea ubunge Jimbo la Igunga na chama hicho, Hussein Bashe, ni raia halali wa Tanzania basi anayestahili kubebeshwa lawama ni Wizara ya Mambo ya Ndani na si chama hicho.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Makamba alisema chama chake kilipata vielelezo kwamba Bashe si raia kutoka wizara hiyo hivyo CCM haistahili lawama.
“Wizara ndiyo ilituambia sisi kuwa Bashe si raia sasa kama wizara hiyo hiyo inasema ni raia basi ituambie kuwa taarifa ilizotupa hazikuwa sahihi, lakini hadi leo tunaendelea kuamini tulichoambiwa na wizara,” alisema Makamba.
Alisema CCM haijapata maelezo yoyote kutoka wizara hiyo kuhusu maelezo tofauti na yale waliyonayo kuhusu uraia wa Bashe.
Alisema hata Bashe kama ana vielelezo vya kuthibitisha uraia wake anapaswa kuviwasilisha CCM na kuulizia kuhusu hatma yake.
Alisema Bashe hajawasilisha vielelezo vya kuthibitisha uraia wake CCM ingawa anapaswa kufanya hivyo.
“Sisi tulimwengua kwa kigezo kwamba si raia wa Tanzania na serikali ndiyo ilitupa hizo taarifa sasa kama waliotupa sisi taarifa wametoa maelezo mengine Bashe aje atuthibitishie uraia wake na ikithibitika ni raia halali basi wizara ndiyo itakuwa imemuonea na si chama,” alisema Makamba.
Alisema hata ikithibitika kuwa uraia wa Bashe ni halali maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya kumwengua kuwania ubunge Nzega hauwezi kubatilishwa kwa kuwa mgombea tayari ameshapatikana.
Mgombea wa sasa wa jimbo la Nzega kupitia CCM ni Dk. Hamis Kigwangalah..

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake