
Yes, tunaongea kuhusu mapenzi. Leo nataka kutoa dawa muhimu sana kwa dada zangu. Unajua kama upo kwenye uhusiano ni vyema pia uwaze juu ya mustakabali wa uhusiano huo.
Hakuna kitu muhimu katika mapenzi kama kufanya yale ambayo mpenzi wako atakuwa anapenda. Sasa hapa nimekuandalia mambo ya msingi zaidi kumi ambayo mpenzi wako anayahitaji zaidi kutoka kwako.
Kwa maneno mengine, kama utaweza kuyatimiza, basi utakuwa umempa msukumo wa yeye kufikiria kukuoa. Hebu jiulize; unadhani mwanaume anahitaji nini zaidi kutoka mwanamke? Ni uzuri, mvuto na ngono?
Sababu nilizotaja hapo si muhimu sana, zinaweza kuwepo, lakini zikawa za mwisho kabisa, ila zipo zile muhimu zaidi. Mpo rafiki zangu?
Kama wewe ni mwanamke ambaye tayari upo katika umri wa kuolewa na bado hujaolewa, mada hii ni muhimu sana kwako. Pia, kama wewe ni msichana ambaye upo katika umri wa kuwa na mchumba mwenye nia ya kufunga ndoa, hili ni darasa tosha kwako!
Rafiki zangu, katika Mila na Tamaduni za Kiafrika, suala la ndoa ni heshima, zamani ilikuwa wazee ndiyo wanaowatafutia vijana wao ndoa, umri ukifika, hata kama ulikuwa hujui au hujawa tayari kufanya hivyo, unaletewa mke/mume!
Siku hizi hali ni tofauti, muda ukifika mwenyewe unatakiwa kujua na kuchukua hatua za kuwa na mwenzi sahihi ambaye atatimiza ndoto zako. Hakuna mtu ambaye yupo tayari kuwa katika uhusiano wa bahati mbaya. Uhusiano ambao mwisho wake haujulikani. Hakuna.
Pamoja na ukweli, wapo baadhi ya watu ambao anakuwa katika uhusiano na mwenzi wake lakini kichwani akiwa hana ndoto zozote, achilia mbali ndoa, yaani hawazi chochote zaidi ya kujistarehesha mwili tu. Nataka hapa uchukue pointi moja muhimu sana; nazungumza na wale wenye nia ya kutaka kuingia kwenye ndoa pekee.
Katika mada hii, nazungumza zaidi na dada zangu, wapo ambao wamekuwa na wanaume wengi katika mapenzi, lakini siku chache baada ya kuanzisha uhusiano huo, wanaume hao wanawakimbia. Mwingine anaweza kuwa kashatembea na wanaume lukuki, lakini wote wanamwacha.
Zipo fikra mbaya kwa baadhi ya dada zangu, utamsikia mwingine akisema; “Lazima nimelogwa, hii mikosi haiwezi kuniandama mimi peke yangu, kwani mimi nina nini? Mbona wenzangu wanaolewa nabaki mimi nahangaika?”
Unaweza kuwa na maswali mengi sana kichwani mwako, ukilaumu na kulalamika kwamba umelogwa, kumbe hakuna kitu cha aina hiyo. Dada yangu, linapokuja suala la maisha yako ya baadaye, suala la ndoa, achana na fikra za kulogwa, tuliza akili kisha tafuta sababu za wewe kubaki ukihangaikia ndoa kwa miaka mingi bila mafanikio.
Najua upo wewe mwanamke mwenye zaidi ya miaka 30 ambaye una kila kitu isipokuwa mume! Nakuona unavyoteseka, nakuona jinsi unavyotumia fedha zako nyingi kulazimisha mapenzi wa wanaume ili uolewe, lakini imeshindikana. Tulia, mada hii itakufumbua!
Rafiki zangu, yapo mambo ambayo kama usipoyaruhusu kichwani mwako na kuyafanyia kazi, huwezi kutoka katika utumwa ambao unao. Utaendelea kuamini kwamba eti huna ngekewa ya kuolewa, kumbe tatizo ni dogo tu. Wapo baadhi ya wanawake ambao wameshakubali hali zao, kwamba wao siyo wa kuolewa, kisa eti tayari wana miaka 40 na bado hajaolewa na hajatokea mtu wa kumwambia kuwa anatamani kufunga naye ndoa! Unawaza tofauti sana dada yangu.
Tatizo kubwa linalilosababisha usiolewe ni kukosa VIGEZO muhimu vya kuwa mke. Inawezekana una sifa za kuwa mwanamke lakini umekosa sifa za kuwa mke. Inawezekana kabisa.
Wanaume nao huwa na sifa muhimu ambazo wanahitaji kutoka kwa mwanawake ambazo angalau anaweza kuanza kuwaza kuoa, akiwa nazo. Zipo sifa nyingi sana, lakini hapa nitakuchambulia zile muhimu zaidi kumi. Hii ni mada ndefu kidogo msomaji wangu, ambayo inaweza kuchukua majuma matatu hadi manne, lakini itakuacha na funzo la kutosha.
Sasa angalia sifa ambazo wanaume wengi wanahitaji wanawake ambao wanatarajia kuwaoa wawe nazo.
KWANZA: Umpende kwa dhati. Hii ni sifa ya kwanza na muhimu sana katika mapenzi hasa yanayoelekea kwenye ndoa. Inawezekana ukaona ni sifa ya kawaida, ambayo pengine kabla hata ya kuiandika, ulishakutana na mtu akakueleza au wewe mwenyewe unafahamu juu ya jambo hili.
Hapa nazungumzia zaidi ya unavyofahamu, nikisema penzi la dhati namaanisha penzi la moyoni. Moyo wako uwe na penzi lisilo na doa, kama moyoni utakuwa unampenda sana mpenzi wako, bila shaka utaonesha kwa vitendo.
Penzi la dhati, kusaidiana, kushauriana, kushirikiana kwenye furaha na matatizo, dhiki na faraja. Ni rahisi sana mpenzi wako kujua kama ni kweli una mapenzi ya dhati au unaigiza. Atagundua tena kwa muda mfupi sana.
Atakuchunguza akizungumzia kuhusu ndugu zake, unavyochukulia, atakuangalia anapokuwa katika msongo wa mawazo kama unamsaidia. Ataangalia mambo mengi sana na mwisho atagundua kama penzi lako ni la dhati au ni kiinimacho.
Onesha mapenzi yako yote ili uwe na sifa hii, acha roho mbaya, kuwa mpole, mkarimu na mwenye kuchukulia matatizo ya mwenzako kama yako! Hapa hapana ugumu sana, kama kweli moyoni mwako kutakuwa na mapenzi ya dhati. Kukishakuwa na mapenzi ya kweli, basi sifa hii ni muhimu na tayari utakuwa umeshakuwa na moja ya sifa 10 muhimu zitakazokuwezesha uwe na tiketi ya kuelekea kwenye ndoa.
Nafasi yangu ni finyu, nivumilieni hadi wiki ijayo tena katika mwendelezo wa mada hii.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wakewww.shaluwanew.blogspot.com
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake