ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 28, 2010

Mtoto wa kike unataka kulinda hadhi yako? Soma hapa!

Ni raha mustarehe tunakutana tena. Ramadhani inakwenda, hivyo ni vema kumuomba Mungu atuvushe kwenye ibada hii salama. 

Leo nimechagua nikusomeshe kwa mada hii! Jamani uswahilini kwetu kuna mambo, watu wanasema Ilala ni zaidi, wengine wanadai Temeke ni kiboko, wapo wanaoamini kuwa Mwananyamala ni ‘usipime’, ila uzoefu unaonesha kwamba tatizo ni kubwa na lipo kila mahali.

Masikini ya Mungu, hawajui kama tabia zao zinawafanya wapoteze mvuto wao. Je, mpaka sasa hujajua nazungumzia nini? Kuna wanawake wana mchezo mbaya, hawavutii hata kidogo. Mwanaume akithubutu kutoa ‘ofa’, kaumia. Atakusanya mashoga zake wote.

Mfuko wa mwanaume mmoja kwenda kuupiga ‘mtungo’ wanawake 20! Maskini ya Mungu wengi siku hizi hawana aibu? Aliyekwambia uende na mtu ni nani? Pengine alijipiga piga kwa ajili ya wawili, sasa mmekwenda 10. Ni aibu!

Zipo athari nyingi ambazo unaweza kukutana nazo kama hutoamua kubadilika. Wanasema mwanamke hulka! Kuna watu walikimbiwa baa, kaitwa yeye, akakosa ustaarabu na kuongozana na wenzake. Jamaa akabwaga manyanga chini, akakimbia! 

IKIWA ALIDHANI WEWE NI A, ATAKUONA F!
Inawezekana mwenyewe alidhani kapata mwanamke bomba, lakini wewe ukakosa ustaarabu! Kosa moja, litamfanya ajute kukufahamu. Awali, alidhani wewe hadhi yako ni alama A, ila baada ya kituko cha kuongozana na mashoga zako kuushambulia mfuko wake, atakugeuza kuwa F.

Acha mchezo huo ili ulinde heshima yako. Ifikirie aibu itakayokupata baada ya huyo jamaa kukushusha thamani. Kama ‘kampani’ yako ipo hivyo, chonde chonde jitahidi kuepukana nayo.

HUYU ANANIPENDA KWA SABABU YA MFUKO WANGU! ATAWAZA!
Mwanamke makini huwa imara sana katika matumizi ya ‘mista’ wake. Sasa wewe vipi huogopi pesa za mwanaume? Swali ambalo atajiuliza kwa haraka ni hili; Thamani yake kwako ni mfuko wake? Kama sivyo mbona humhurumii?

IKIWA ALIFIKIRIA KUKUBEBA JUMLA, BASI IMEKULA KWAKO!
Ndoa ni mipango. Ukiitwa, itika peke yako ili muende sawa, siyo unalazimisha kuitika na wenzako. Inawezekana penzi ndiyo kwanza jipya, kwahiyo linatakiwa kurutubishwa, wewe unaharibu kwa kuonesha ‘upaka mapepe’ mapema.

ANGALIA ALIVYOJIANDAA, SIYO KUKURUPUKA!
Watu wabadilike, tabia ya namna hii haifai. Mwanamke asiye na huruma hana sifa ya kuitwa mke. Angetaka uongozane na wenzako angekwambia, pengine yeye amekadiria wawili tu, yaani wewe na yeye. Ila kwa sababu huna utu, ukaamua kumkomoa kwa kumjazia mashoga zako.

Kukupenda isiwe tabu! Umtie umaskini kwa sababu eti anataka kukufurahisha. Unaongozana na mashoga zako wakati unafahamu hao ni mashangingi, bila ‘kreti’ kila mmoja hawajalewa. 
Mpo 10, kila mmoja anaagiza kuku wake mzima na chips. Huyo shosti wako macho makubwa, amemaliza paja la mbuzi hajashiba, kapiga jicho meza jirani kaona mchemsho wa ng’ombe anataka. Bili inakuja shilingi 100,000. Hatari sana!

KUNA MWENZAKO ALIVULIWA NGUO, AKAACHA SIMU!
Kuna watoto wa mjini na wanawake wengi wameumbuka walipokutana nao. Anawaruhusu muagize mnavyotaka. Huyu kaagiza mchemsho wa kuku na ile pombe ya kitajiri, bei yake mlima, yule naye kaamua ‘kujikoki’ kwa mishkaki 20. Nafasi ya kula wanayo!

Swahiba kaona mambo yamemzidia, kaamua kujitoa. Kapita mlango wa nyuma katoweka. Inakuja bili ya shilingi 200,000, huna kitu. Utaacha simu na kuvuliwa nguo ili zibaki kama dhamana. 

Kama hujui, kuna waliojikuta wakitoa penzi bila kupenda. Bili imekuja, jamaa aliyeongozana naye katoweka, akabaki kutoa macho! Mkware mmoja hivi akaamua kujitolea kumlipia. Baa ina gesti, kwahiyo kabla ya kutoa pesa ikabidi waingie chumbani.

Ni elimu kwako, kwa maana wapo waliojikuta ‘wakilumagiwa’ bila hata kinga. Inauma kwa sababu mwisho wa siku unakuja kugundua kwamba ilikuwa rahisi kukwepa mtego. 

Hujui mwanaume gani anakuja kwako kwa lengo la kukubeba jumla au anayepita tu. Ishi kwa mahesabu, kwa maana utakapoona miaka inakatika, ndiyo utaanza kujutia muda uliopoteza. Jiheshimu uheshimiwe. Achana na hulka za kuambatana kundi unapokwenda kwenye miadi.

No comments: