
Nawashukuru wote tuliokuwa tunawasiliana kwa njia ya simu, sms, waraka pepe na hata wale niliokutana nao kwenye chati ndani ya mtandao wa facebook.
Hiyo inatosha kabisa kunifanya niamini kuwa kazi zangu zinasomwa na kukubalika kwa wasomaji wangu. Bila kupoteza wakati, sasa tunarudi kwenye mada yetu ya msingi.
Tunaangalia namna na matatizo ya kukata kiu ya mwenzi wako mnapokuwa faragha.
Tayari nilishaeleza mambo kadha wa kadha katika ufunguzi wa mada hii wiki iliyopita, sina shaka kuna mambo ambayo tayari yameshakukaa kichwani mwako. Leo niliahidi kuanza kuelezea nama ya kukabiliana na tatizo hili.
Hakuna ubishi kwamba, kutomridhisha mwezi wako ni fedheha sana, hakuna anayependa hilo litokee katika maisha yake ya ndoa, hivyo ni vema kujadili suala hili kwa undani. Sasa hebu twende kwenye vipengele vilivyosalia....
Unadhani unapatia?
Tatizo lingine ambalo limo ndani ya mada ninayoichambua hapa ni wewe mwenyewe kwanza kujihoji kama ni kweli kwamba unapatia?
Ni kweli mwenzi wako anaridhika? Unaweza kukaa na mwanandoa mwenzako kwa miaka mingi, kumbe hajawahi kufurahia faragha tangu mmekutana kwa mara ya kwanza na siku zote amekuwa akikuvumilia akiamini kwamba utabadilika lakini wapi!
Hilo ni jambo ambalo unatakiwa kuliweka kichwani mwako, ulitafakari kabla ya kurukia katika kipengele kinachofuata hapa chini.
Mchunguze sasa...
Yawezekana kabisa ukawa na mwenzi wako lakini asiwe anafurahi na asikuambie! Je, ni sahihi kukaa kimya bila kujua kama unachokifanya kinakubalika? Ni uzembe kufikiri unamfurahisha mpenzi wako kumbe siyo!
Msikie Julius wa Magomeni, Dar es Salaam, anavyoelezea: “Nimejaliwa mke mzuri sana, kweli mke wangu anavutia na siku zote nilikuwa nawaza namna ya kumfanya asinisaliti. Niliamini nikiwa mkali kwenye mambo yetu, basi nitamfanya asifikirie kabisa kunisaliti.
“Kwahiyo nikiwa maeneo hayo nakuwa mtundu sana, lakini hata siku moja sikuwahi kumuuliza mke wangu kama anafurahia, lakini siku moja, baada ya kumwona ananionesha ushirikiano zaidi, nikaamini mke wangu atakuwa amefurahia sana mapenzi.
“Basi nikamuuliza, vipi mwenzangu tunakwenda sawa? Jibu alilonipa lilinihuzunisha sana. Alinijibu kwamba, afadhali nimemuuliza mwenyewe, lakini ukweli ni kwamba tangu nimekutana naye hajawahi kumaliza safari yake, hasa siku hiyo! Nilitamani kuzimia, lakini nashukuru kwamba, kuanzia hapo nilijifunza kitu, kumbe nilikuwa si lolote.
Basi, nikachukua hatua. Asikwambie mtu, Rose sasa hivi anafurahia sana kuwa na mimi.”
Huo ni mfano wa wazi ambao sina haja ya kuongezea kitu kingine chochote mbele ya nukuu ya msomaji wangu Julius. Hebu sasa tuone kipengele kinachofuata.
Jadilianeni pamoja!
Kuambiwa huwezi kazi, kusikufanye uchukie au ukate tamaa, unatakiwa kukaa chini na mwenzako na kuzungumza naye. Ni mambo madogo tu jamani, inawezekana kuna eneo dogo sana unalokosea, ambalo ukikaa sawa, basi utakuwa unamfurahisha mpenzi wako.
Hakuna njia nzuri na bora kama ya kujadiliana; msikilize, anapenda kufanyiwa nini, wapi unakosea na wapi unatakiwa kudili napo zaidi? Mambo haya mkijadiliana kwa pamoja ndipo mtakapoweza kufikia kwenye mwisho mzuri ambao bila shaka si utamfurahisha tu yeye, bali amani katika ndoa yenu itatawala na hofu ya kusalitiwa itatoweka.
JE, WEWE UPO KWENYE TATIZO HILI?
Kama wewe unayesoma makala haya sasa hivi, upo kwenye tatizo hili, usiwe na wasiwasi. Kila kitu kinawezekana rafiki zangu. Hakuna mtu aliyeumbwa kwa kasoro au kuwa na kasoro fulani! Wote wapo sawa, ila baadhi ya mambo tunaharibu wenyewe! Ona mwenyewe hapo chini.
Zungumza kwa ishara
Usiende haraka, achana na lugha chafu. Kauli kama: “Sijui wewe ni mwanaume gani, yaani hujui kitu kabisa, tangu nimekuwa na wewe sijawahi ‘ku-enjoy love’ kabisa,” na “Ukweli ni kwamba huwezi kunikata kiu yangu kabisa, hivi we’ mwanaume ukizidiwa kete na wanaume wenzako utamlaumu nani?” Kauli hizi hazifai kabisa katika kumwelekeza mpenzi wako.
Anza kwa ishara kwanza, unaweza ukaacha kutoa ushirikiano wa kutosha, akikuuliza, ndiyo umweleze sababu lakini kwa taratibu na sauti iliyojaa unyenyekevu, si ukali wala kuropoka. Lakini pia unaweza kumpelekea magazeti, majarida au vitabu ambavyo vinaelezea namna ya kumridhisha mwenzi wako. Pia unaweza kutumia hata mikanda ya kikubwa kwa ajili ya kumuamsha usingizini.
Ni imani yangu kwamba, mada imeeleweka vizuri sana. Ukiwa na maoni au maswali zaidi, tafadhali usisite kuwasiliana nami. Ahsanteni sana kwa kunisoma.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;www.shaluwanew.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment