
Kila Jumatano kama leo, huwa nimejaa tele hapa kwenye hii safu, nikitoa dawa kwa ajili ya matatizo mbalimbali ya kimapenzi katika uhusiano. Leo, nimeona nifafanue hili, maana wengi wamekuwa wakiuliza, nimeona si vibaya kuwasaidia wengi kwa wakati mmoja.
Kiukweli ni mada ya ndani sana, lakini nitatumia zaidi tafsida kufikisha ujumbe kwa walengwa pekee. Yes...kuna hiki kilio cha kutofurahishana kimahaba kati ya wapenzi wanapokuwa faragha.
Sioni haya kusema kwamba, wengi wanaokabiliana na tatizo hili ni wanawake! Yaani hawa wapo wengi sana ambao hata ile raha ya mapenzi yenyewe hawaijui! Wanabaki kusikia kwa mashoga zao tu, wanapokwenda salon.
Hakuna shaka kwamba, msingi mkuu wa ndoa, baada ya upendo ni tendo lenyewe la ndoa. Hiki ndicho hasa kinachowaunganisha, maana hata hao watoto wanapatikana kwa njia hii.
“Nina miaka saba ya ndoa, tunao watoto wawili na mume wangu, lakini kiukweli kabisa, sijawahi kufurahia mapenzi hata siku moja, nafikia mahali nawaza kutafuta mwanaume mwingine nje,” anasema mama Helena, mkazi wa Soweto, Mbeya kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno.
Mama Shamanona wa Dodoma anasema: “Mr. akija anakuwa na miharaka yake, tunakutana harakaharaka, akimaliza haja zake anakoroma, ananiacha nateseka, nimeshavumilia nimechoka, nimeona ni bora nitoe dukuduku langu kwako mshauri unaweza kuwa na mawazo ya kunisadia.”
Wapo wengi, lakini hao ni baadhi yao tu. Je, unadhani ni sahihi wanawake hao watafute wanaume wengine nje ya ndoa zao kwa ajili ya kusaka penzi bora? Penzi bora ni lipi hasa? Ni usaliti? Majibu ya maswali yote hayo hapo ni kwamba si sahihi!
Moto hauzimwi kwa moto, bali maji. Tatizo huwa halikimbiwi wala kuhairishwa, isipokuwa hutafutiwa njia za utatuzi. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na tatizo. Hebu kwanza tuone maana ya kuridhishana, halafu tuendelee na vipengele vingine.
DHANA YA KURIDHISHANA!
Katika mapenzi ni vizuri wote mkatoka mkiwa mmekata kiu zenu ipasavyo. Hakuna mapenzi ya upande mmoja! Si kweli kwamba wanaume pekee ndiyo wanaotakiwa kumaliza haja zao na kuwaacha wanawake wakiwa bado wanawahitaji!
Baadhi ya mila za makabila fulani, huzingatia hili, kwamba mwanamke hana uwezo wa kumwambia mumewe; “Sijaridhika.”
Akifanya hivyo, anaweza kupigwa lakini pia ataonekana kama mwanamke asiye na staha. Hiyo si sahihi, kama ilikuwa zamani, katika kizazi kipya haitakiwi kupewa nafasi kabisa.
TATIZO LIPO WAPI HASA?
Vipo vitu vingi sana vinavyochangia tatizo la kutoridhishana faragha. Hapa nitachambua machache, ambayo angalau yatakupa mwanga na kukufanya ujue upo kwenye kundi gani, halafu baada ya hapo, nitakupa dawa ya moja kwa moja ya tatizo hili.
(i) Utayari kisaikolojia
Pamoja na mambo yanayoweza kusababisha kushindwa kuridhika faragha, utayari kwa kisaikolojia unatajwa kushika nafasi ya juu zaidi.
Yapo matatizo mengi, lakini kutolewa usichana kwa njia ya ubakaji ni kati ya sababu hizo. Mwanamke anapobakwa huwa haridhiki na kinachotokea pale ni maumivu, hivyo kuanza kuchukia kabisa tendo hilo.
Kama mwanamke huyo hatapata ushauri mzuri wa wataalamu mapema, anaweza kupatwa na tatizo hili.
(ii) Mawazo
Kushinda kutwa nzima mara nyingi kwa mtindo wa kujiinamia, kunatajwa pia kama sababu ya kutofurahia mapenzi na si kufurahia tu bali hata kuondoa kabisa hamu ya tendo hilo.
Inashauriwa, kujitahidi kadri ya uwezo wako wa mwisho kuhakikisha tabasamu linakuwa sehemu ya maisha yako. Kuwa na furaha ni jambo jema, kwani zaidi ya kuchangamsha ubongo, mwili unakuwa katika msisimko wa kufurahia mapenzi.
(iii) Ukali
Kama upo kwenye uhusiano na mwenzi ambaye muda wote anakuwa mkali, hilo ni tatizo lingine litakaloweza kukupunguzia ari ya kufanya na kufurahia tendo la ndoa.
Mwanaume ambaye muda wote ni mkali, mgomvi, mwenye masimango, anachangia kwa kiasi kikubwa mwanamke kumuogopa na kukosa utayari wa tendo lenyewe, mwisho anakuwa haridhiki na tendo lenyewe.
(iv) Mazingira
Ndiyo...mazingira yanaweza kabisa kusababisha mwanamke asifurahie mapenzi. Mathalani anaishi ukweni, ndugu zake au kwenye nyumba ndogo ambayo inaweza kuruhusu watu wa chumba kinachofuata kusikia kila kitu katika chumba chao.
Kikubwa hapa ni woga au aibu, kwani huwaza zaidi jinsi atakavyofedheheka atakapokutana na watu hao mitaani. Hili linatosha kabisa kupoteza hamu ya tendo au kutoridhika akiwa na mwezi wake faragha.
(v) Maandalizi
Huwezi kumla kuku akiwa mzima, lazima achinjwe, atayarishwe na kubandikwa jikoni, huo ndiyo utaratibu uliopo hata kwenye suala la mapenzi. Wanaokurupuka ndiyo husababisha wenzi wao kutofurahia mapenzi.
Sina shaka umepata kitu kipya kichwani mwako. Umegundua upo katika kundi gani, hapo sasa ni hatua nzuri zaidi ya kuelekea kwenye kujua namna ya kufanya ili kukabiliana na tatizo hili. Natamani sana kuwapa dawa hiyo leo, lakini kutokana na nafasi yangu finyu, nalazimika kuishia hapa, lakini TIBA KAMILI ni wiki ijayo, usikose tafadhali.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Mtembelee kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake