Friday, August 20, 2010

Wateja walazimishwa kuvua viatu K'koo!

Mara nyingi tumezoea kuona waumini wa kiislamu wakiingia msikitini bila viatu, ikiwa ni njia ya kuhifadhi udhu lakini kuchelea kuchafua sehemu hiyo ya ibada.

Pia katika baadhi ya nyumba, upo utaratibu wa watu kuvua viatu kabla ya kuingia ndani, kwa maana hiyo hiyo ya kuchelea kuchafua.

Utamaduni huo sasa umeingia hata katika baadhi ya maduka jijini Dar es Salaam, ambapo sasa wateja wanalazimishwa kuvua viatu kabla ya kuingia kwenye maduka.

Hali hiyo hakika sio ngeni hata kidogo hata miongoni mwenu wasomaji.....ambapo baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka yanayouza nguo za kike hususani mitandio, vikoi na magauni maarufu kwa jina la dira wanawalazimisha wateja kuvua viatu kabla ya kuingia ndani ya maduka.

Katika sakafu na mazulia ya baadhi ya maduka hasa yaliyopo mtaa wa Narung’ombe karibu na lango la kuingia Soko Kuu la Kariakoo, eneo la shimoni yaliandikwa kwa wino mwekundu ‘Vua viatu’.

Ikiwa mteja hakuona tangazo hilo na kuingia dukani akiwa amevaa viatu hutakiwa kutoka nje na kuvua viatu, kisha kuviacha mlangoni ama kuvibeba ndipo atapewa ruhusa ya kuingia kwenye maduka hayo kwa lengo la kuangalia au kununua bidhaa mbalimbali.

Wateja wanaokataa kuvua viatu hupewa sehemu ya kukaa na kutakiwa kuelezea wanachotaka ambapo wafanyakazi wa duka watamhudumia kadri atakavyo.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake