Tuesday, September 21, 2010

INASIKITISHA!!!!

Na Richard Bukos
Inasikitisha, walimu wawili wa kiume wa Shule za Msingi Kijitonyama na Good Shefa zote za jijini Dar es Salaam wanaodaiwa kuwabaka wanafunzi wao, mwishoni mwa wiki iliyopita walisababisha watu waliofurika mahakamani kuangua vilio baada ya kuwaona wakati wakipandishwa kizimbani kusomewa mashitaka yao.

Mwalimu, Ezekiel Mchome anayedaiwa kubaka akiwa chini ya ulinzi.
Katika sakata hilo, Jumatano iliyopita Mwalimu, Ezekiel Mchome (50), anayefundisha Shule ya Msingi Good Shefa, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Temeke mbele ya Hakimu, Mbona Masabo na kusomewa shitaka la kumuingilia kimwili Mwanafunzi wa Darasa la Tatu mwenye umri wa miaka minane (jina linahifadhiwa) anayesoma Shule ya Msingi Chamazi. 

Akimsomea shitaka hilo, Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Pamphil Mlowola alimwambia mshitakiwa, anadaiwa kumuingilia kimwili mwanafunzi huyo kwa nyakati tofauti jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Mwalimu Ally Mgaza naye akiwa chini ya ulinzi kwa madai ya kubaka.
Mwalimu huyo aliyeingizwa kizimbani hapo huku akirushwa ‘kichurachura’ na afande aliyemchomoa mahabusu alikana kutenda kosa na kutakiwa kuwekewa dhamana ya shilingi 500,000 au kwenda mahabusu. Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Oktoba 13, mwaka huu.

Mpaka mwanahabari wetu anaondoka eneo la tukio, mwalimu huyo alikuwa akichungulia kwenye nondo za mahabusu ya mahakama ambapo ndugu yake mmoja alionekana akihangaika kumdhamini. 

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Makumbusho, Ally Mgaza naye siku iliyofuata alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Wilaya ya Kinondoni, Mbele ya Hakimu Kihawa, akituhumiwa kujaribu kumbaka mwanafunzi wake darasani anayesoma Darasa la Sita.
Mtoto wa miaka sita anayedaiwa kubakwa akiwa na mama yeke wote wakilia.
Akisomewa shitaka hilo na mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Mohamed Kilongo, Mwalimu Mgaza alidaiwa kuwa mnamo siku tofauti katika tarehe za Septemba mwaka huu, alijaribu kumbaka mwanafunzi huyo.

Mwalimu huyo aliyeingia kizimbani hapo akitokea mahabusu huku akiwa amejifunika uso kama mwari kukwepa aibu ya umati uliofurika mahakamani hapo kumshuhudia, alikana shitaka hilo.

Baada ya kukana, hakimu anayesikiliza kesi hiyo alimtaka mwalimu huyo kutafuta watu wawili wa kumuwekea dhamana ambapo aliahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba 26, mwaka huu.
Habari kwa hisani ya GPL

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake