.jpg)
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, ameibuka shujaa baada ya wagombea sita wa nafasi hiyo, akiwemo Dk Ali Mohammed Shein wa Chama Cha mapinduzi (CCM), kutoshiriki.
Mdahalo huo uliandaliwa na Mjumuiko wa taasisi za kiraia Zanzibar na kuendeshwa kwa pamoja na vituo viwili vya redio na viwili vya televisheni.
Kutokana na kushindwa kushiriki kwa wagombea wa vyama vya Tadea, NRA, NCCR-Mageuzi, Jahazi Asilia, AFP na CCM, mdahalo huo uliendeshwa kwa kumshirikisha Maalim Seif peke yake.
Kiongozi wa kamati maalum ya mdahalo huo, Kombo Maalim, alisema uliandaliwa kwa kutoa fursa kwa wagombea kuulizwa maswali ya moja kwa moja na wananchi.
"Tumeandaa mdahalo huu baada ya kuzingatia kuwa wananchi wengi hawapati fursa ya kuwauliza mwaswali wagombea katika mikutano ya kampeni", alisema.
Kombo alisema vyama vyote vilivyosimamisha wagombea wa urais Zanzibar vilipewa mualiko.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa NCCR- Mageuzi, Nadir Joseph Nyoni, alithibitisha chama chake kupokea mwaliko huo.
Hata hivyo alisema mgombea wa chama hicho, Haji Hassan Khamis hakuweza kushiriki kutokana na matatizo ya kifamilia.
"Tulipata mualiko lakini mgombea wetu amepata msiba na amesafiri kwenda Pemba", alisema Nyoni.
Mgombea kupitia AFP, Said Soud Said, alisema chama chake kimeshindwa kushiriki katika mdahalo huo kwa sababu hauna maslahi ya kifedha.
"Hatuwezi kushiriki kwa sababu hatupewi pesa na waandaaji, wakati wao wanalipwa", alisema Said.
Viongozi wa CCM hawakuweza kutoa maelezo mara moja juu ya kutoshiriki katika mdahalo huo. Lakini wiki iliyopita akizungumza katika viwanja vya Kibandamaiti, Katibu Mkuu wa CCM Yussuf Makamba alisema chama chake hakitawaruhusu wagombea wao kushiriki midahalo.
Alisema hatua hiyo ilifikiwa kwa sababu fursa ya kuulizwa maswali na kutangaza sera zao wanaipata kwenye mikutano ya kampeni.
Akijibu maswali kwenye mdahalo huo, Maalim Seif aliahidi kuwa iwapo atachaguliwa, serikali ya CUF itaunda kamati maalumu ya kuratibu shughuli za walemavu.
Alisema jukumu la kamati hiyo litakuwa ni pamoja na kuandaa takwimu za walemavu wa aina zote wakiwemo, viziwi, wasioona na wenye ulemavu wa viungo mbali mbali vya mwili.
Maalim Seif alisema takwimu hizo zitasaidia serikali yake kujijengea uwezo wa kuisaidia jamii hiyo chini ya dhana ya CUF, kutoa haki sawa kwa wote.
Zanzibar inakadiriwa kuwa na walemavu 100,000 na hiyo ni idadi ya kukadiria kwa sababu serikali kwa sasa haina utaratibu unaoiwezesha kukusanya takwimu za walemavu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake