Tuesday, October 19, 2010

Atongoza, akataliwa, aua, ajiua Iringa

BAADA ya kukataa kuwa na mahusiano ya kimapenzi, binti wa miaka 16 Laheri Maneno, mkazi wa Kijiji cha Chamdindi, Wilaya ya Iringa Vijijini ameuawa kwa kupigwa na nondo kichwani na Absalum Mbogela (22), Mkazi wa Itagutwa mkoani hapa kabla na kijana huyo naye kujiua kwa kunywa sumu.

Mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo aliliambia Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, tukio hilo lilitokea hivi karibuni na chanzo cha kijana huyo kufanya mauaji hayo ni kutokana na Laheri ambaye ni mwanafunzi kumkataa kimapenzi.




Absalum Mbogela (22).

Alisema kuwa binti huyo alikutwa na mauti akiwa njiani kwenda bustanini kumwagilia mazao ambapo kijana huyo alimvizia njiani akiwa na nondo na kisu na kumpiga nayo kichwani kisha kumchoma kisu shavuni.

Baada ya kufanya ukatili huo inadaiwa kijana huyo alikimbia na alipofikia umbali wa kama hatua mia tano, alikunywa sumu na kufariki muda mchache baadae.

“Absalum kwa muda mrefu amekuwa akimtaka kimapenzi msichana huyo na kuna wakati alikuwa akimtishia kumfanya kitu kibaya na sasa amekitimiza na yeye kujiua,”kilisema chanzo chetu.



Laheri Maneno (16).

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Itagutwa, Bahati Kamilongo alisema kuwa, kijana huyo alikutwa amekunywa sumu na alifariki dunia wakati jitihada za kumpeleka hospitalini zikifanyika.

Naye Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba jeshi lake linaendelea na uchuguzi zaidi .    chanzo:GPL

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake