Tuesday, October 19, 2010

Hatma ya Rooney Man United mashakani

Klabu ya Manchester United imefahamishwa Wayne Rooney hatatia saini mkataba mpya na klabu hiyo, hayo ni kwa mujibu wa shirika la Press Association.
Wayne Rooney
Wayne Rooney
Rooney mwenye umri wa miaka 24, mkataba wake unamalizika mwaka 2012 na imefahamika mazungumzo juu ya mkataba mpya yamevunjika.

Kumekuwa na tetesi kwamba Rooney atauzwa mwezi wa Januari wakati wa usajili mdogo, huku Real Madrid wakimuhitaji.

Hata hivyo klabu ya Manchester United ikajibu kwamba hayo yote ni "upuuzi mtupu".

Uhusiano wa Rooney na meneja wake Sir Alex Ferguson kwa wiki za karibuni sio mzuri.

Mshambuliaji huyo mwezi uliopita hakuweza kucheza pambano la ligi dhidi ya Everton kwa madai yaliyohusisha maisha yake binafsi na hakupangwa na Ferguson, aliyedai ameumia kifundo cha mguu.

Hata hivyo siku ya Jumanne iliyopita, baada ya England kwenda sare ya 0-0 na Montenegro katika mchezo wa kufuzu kwa mashindano ya Euro 2010 kwenye uwanja wa Wembley, Rooney aliipinga taarifa ya Ferguson na kusisitiza hakuwa ameumia na hana matatizo yoyote ya kifundo cha mguu.

Siku ya Jumamosi, Rooney, ambaye hadi sasa amefunga bao moja tu katika michezo mitano ya Ligi Kuu ya England aliyocheza msimu huu, hakuanza mchezo dhidi ya West Brom ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2.

Ferguson, ambaye hadi sasa hajatamka lolote hadharani juu ya uhusiano wake na Rooney, alimuingiza mshambuliaji huyo zikiwa zimesalia dakika 20, baada ya Manchester United kushindwa kulinda mabao yao mawili na akamuamuru acheze nafasi ya ushambuliaji wa kushoto.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake