
VITA Mwanza, Simba na Yanga kesho Jumamosi zitapambana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mkoani hapa huku zikiwa na wachezaji mahiri wenye hatihati ya kucheza.
Wakati Yanga ikiwa katika hatari ya kuwakosa Abdi Kasim, Nsa Job na Kiggi Makassy ambao ni wagonjwa, Shamte Ally ametajwa kukosa mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi wa muda mrefu.
Simba kwa upande wake, ipo katika hatari ya kuwakosa Mohamed Banka, Mussa Hassan Mgosi huku Hilary Echesa huku Nico Nyagawa, Uhuru Selemani na Salum Kanoni wakiwa katika orodha ya wachezaji wataoukosa mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
Pamoja na hali hiyo, mitaa mbalimbali ya jiji la Mwanza imegubikwa kwa shamra shamra za hapa na pale juu ya mchezo huo, huku bendera na vitambaa nyekundu na nyeupe na zile za njano na kijani zikipepea katika maeneo tofauti.
Huku timu zote zikiwa na majeruhi wanaoweza kutishia uimara wa vikosi vyao, makocha wa timu hizo wameonekana kutokuwa na presha kutokana na hali hiyo.
“Tunakuja Mwanza, tayari kwa ajili ya kupambana na maandalizi mengine yanaendelea vizuri tu,” alisema Kocha wa Yanga Kosta Papic raia wa Serbia, ambaye timu inatarajiwa kuwasili leo Mwanza.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri raia wa Zambia alisema: “Tunafanya juhudi kuwarudisha katika kikosi wachezaji wetu walio majeruhi, hata hivyo lengo letu ni ushindi.”
Mshindi katika mchezo wa leo ndiye atakayekalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo inayoongozwa na Yanga yenye pointi 16 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 15, zote zimecheza mechi sita.
chanzo GPL
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake