
Kitu ambacho naweza kusema kwenye mfumo huu wa mapenzi ni kwamba, muongozo wa wanandoa unaweza kutumika kwa wapenzi wasiooana, lakini waliooana hawawezi kutumia mfumo wa walio nje ya ndoa.
Nasema wanandoa hawawezi kutumia kwa sababu tendo la ndoa kwenye ndoa si kitu cha kwanza, kwa vile ndoa ni maisha na kamwe kuishi na mtu hakutegemei tendo bali hitaji la kumjali mwenzako na kujitolea.
Lakini tunapozungumzia maisha ya mapenzi nje ya ndoa tunakuwa kwenye suala la starehe zaidi. Hii inaweza kuwa hoja ya msingi na kigezo cha wapenzi wenyewe kujichunguza mfumo wao wa maisha, kama ni wa starehe au wa maisha.
Jambo kubwa ambalo nataka kulizungumza kwenye mada hii ni umri wa ndoa na kuvunjika kwa mapenzi ambapo wengi wamekuwa wakiuliza chanzo na sababu.
Jibu la swali hili limekuwa gumu, lakini kutafuta sababu nyingi nje ya mfumo sahihi wa aina za mapenzi nilioutaja ni kujichosha bure. Nikisema hivi nataka kusema, adui wa ndoa zetu siku hizi ni mpangilio wa sifa za mapenzi ya kweli nilioutaja.
Kama nilivyosema kwenye ndoa kuna Kujaliana+ Kujitolea=Tendo la Ndoa, huku kwenye mapenzi ya kawaida mfumo wake ni Tendo la ndoa+Kujaliana=Kujitolea.
Mpangilio huo ni sahihi sana kwenye aina hizo za mapenzi, kwa vile kuwa na mpenzi kwenye uhusiano wa starehe halafu kusiwepo na kitu hicho ni jambo baya, kadhalika kwenye ndoa mambo ya msingi yanapokosekana pia hukwaza.
Watu walioko kwenye mapenzi wanaweza kuwa watu wa kukutana na kupeana tendo na kuondoka, lakini kwenye ndoa huwezi kufanya hivyo ukaeleweka bila kujitolea na kujali.
Lakini ni vyema kila mdau wa mapenzi akatambua kuwa wapenzi wengi siku hizi hutoka kwenye mfumo wa mapenzi ya starehe na kuyahamishia kwenye ndoa.
Kitaalamu kubadili malengo ya penzi si jambo baya, lakini inashauriwa mnapohama msihame na mfumo wa zamani kwa sababu hautafanya kazi huko muendeko kwenye mapenzi ya ndoa.
Wengi kati ya wale wanaohama na mfumo wa zamani ndiyo wale wanaojikuta wakipoteza msisimko wa penzi katika kipindi kifupi, kwa sababu kwenye ndoa ‘kummisi’ mwenzako, hakutakuwepo, atakuwepo karibu yako kila siku.
Wanandoa wengi waliohama na msukumo wa mwili kwenye mapenzi ya uchumba, hujikuta wakiwaona wenza wao ni wa kawaida kiasi cha kuanza kujiuliza mara mbilimbili kama walikuwa sahihi kukubali kuoana.
Hali hii hutokana na kile kilichokuwa kikiwaongoza, yaani tendo la ndoa kupungua mvuto. Hapo ndipo wengi huanza usaliti na wakati mwingine, kuvutwa na wapenzi wa nje kiasi cha kuona hawana cha kupoteza hata wakitengana na wake au waume zao.
Kama nilivyosema ndoa inataka kujaliana, mtu mwenye kujali hawezi kuchuja, mwenye moyo wa kujitolea, hawezi kuona mzigo kutoa alichonacho kwa ajili ya mwenzake. Hayo ndiyo maisha ya kudumu yanayotakiwa.
Hebu tujiulize sote tulioko kwenye ndoa ni kipi tumetanguliza katika hayo niliyosema? Mwenza wako anapokuwa hayupo unakumbuka nini, tendo la ndoa, kumjali au kujitolea?
Ikiwa utakuwa kwenye fungu la watu wa kustarehe, kitu cha cha kwanza kitakuwa ni tendo na bila shaka ukiona mwenzako kachelewa kurudi mawazo yako yote yatakuwa kwenye kusalitiwa na punde atakapoingia kazi ya kwanza itakuwa ni kupekua simu yake kujua mawasiliano yake.
Nimalizie kwa kusema mume/mke si maalum kwa ajili ya tendo la ndoa bali maisha. Hata msiposhiriki kwa mwezi haiwezi kuwa jambo la kushtaki na kulilalamikia kwa jirani. Asanteni kwa kunisoma.
Ukipenda kujifunza elimu kama hii kwa undani, jipatie Kitabu cha TITANIC- 3 chenye mada, meseji za mapenzi na chombezo mbili za kusisimua. Kinapatika kwa wauza magazeti nchi nzima kwa bei ndogo sana.
No comments:
Post a Comment