|
MGOGORO wa kisiasa wa kuhusu uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha, unaweza kuzaa mpasuko siyo tu kwa wakazi wa Arusha, bali hata kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba, kutofautiana na mmoja wa makada wake maarufu, Edward Lowassa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Makamba akionesha kutofurahishwa na kauli
ya Lowassa ya kutaka mgogoro huo wa umeya wa Arusha umalizwe kwa amani kwa kuzikutanisha pande zinazohusika, alisema taarifa ya Lowassa iliyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari jana, imemshitua sana.
Pamoja na kuzungumzia amani, Lowassa pia alisisitiza wahusika kuelimishana ili kuunusuru mji huo wa Arusha na Taifa kwa ujumla, usitumbukie katika ghasia.
Lowassa alivitaka vyama hivyo kukaa meza moja kumaliza vurugu zilizotokana na uchaguzi wa
kumpata meya wa jiji hilo ambapo iliripotiwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisababisha vurugu na kukamatwa na polisi ambapo baadaye aliachiwa.
Jana, baadhi ya magazeti yalimnukuu Lowassa akisema juzi katika mkutano mjini Arumeru kuwa, “leo nimekuta Mji wa Arusha ukiwa umezingirwa na askari Polisi na sehemu zingine kulikuwa na gari la maji ya kuwasha kwa ajili yakulinda usalama wa mji na watu wake.
“Hali hii imetokana na uchaguzi uliomalizika hivi karibuni, nawaomba viongozi wa vyama
vinavyovutana, wakae haraka ili kuondoa hali hii ili Arusha isije kuwa kama Ivory Coast…Arusha ni yetu sote.” Alisema.
Hata hivyo Makamba kutokana na taarifa za vyombo vya habari alisema:“Nimeshitushwa sana na taarifa hiyo, nimeshituka kwa vile namjua vizuri Mheshimiwa Lowassa.
Ni kiongozi makini, hakurupuki, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na anazijua sana taratibu za Chama.
Hawezi kukikemea Chama chake kupitia magazetini. “Anapo mahali pa kukikosoa kama kimekosea. Ni katika vikao. Nadhani amenukuliwa vibaya.”
Makamba alisema vurugu zinazoendelea Arusha haziwahusu na wanaopaswa kukemewa kwa kutaka kuigeuza Arusha kuwa Ivory Coast, siyo CCM kwani wao wanaamini uchaguzi uliendeshwa vizuri na mgombea wa chama chao ndiye Meya wa Arusha kwa sasa.
Makamba alisema hoja ya Lowassa kuwataka wakae meza moja na Chadema, haina msingi
ambapo alisisitiza “hatuna ugomvi na Chadema na mgombea wetu ameshinda, upande usioridhika na matokeo unapaswa kuyapinga kwa mujibu wa taratibu zilizopo.”
Alisema uchaguzi huo haukusimamiwa na CCM, bali Mkurugenzi wa Jiji la Arusha hivyo kasoro kama zipo, CCM haipaswi kulaumiwa, akifafanua kuwa “upande ambao hauridhiki na matokeo hayo, unapaswa kuyapinga kwa mujibu wa taratibu zilizopo.”
Lakini akizungumza kwa simu jana jioni kutoka nyumbani kwake Monduli, Lowassa alisema hajayaona magazeti ya jana yalivyoandika, lakini alichokisema juzi ni kwamba vyama husika vikae na kuzungumza namna ya kumaliza tofauti zao kwa sababu vurugu hazina maslahi kwa Arusha na Taifa kwa ujumla.
“Niko Monduli, sijaona magazeti ya leo (jana), lakini nilichokisema juzi ni kwamba vyama husika, vikae na kuzungumza kwa nia ya kumaliza tofauti zao. Sijamkemea mtu, sijasema nani mshindi, nani ameshindwa. Nimetoa ushauri, kwa sababu sitaki amani ivurugwe,” alisema Lowassa.
Alisema katika ushauri wake, hakutaja jina la chama chochote, na anaweza kuwa amenukuliwa
vibaya, lakini la msingi alilosisitiza ni kuwa suala la kuelimishana.
“Pengine hawajui utaratibu, ni suala la kuelimishana. Tusipigane mitaani, tuwaelimishe wenzetu. Nisingependa kuona Arusha inakuwa na vurugu, tunahitaji mji wetu uwe na amani,” alifafanua Mbunge huyo wa Monduli.
Chadema juzi iliandaa maandamano na vijana wa chama hicho kuingia mitaani na kulifanya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kuwatawanya kwa maji ya kuwasha.
CHANZO:HABARI LEO
Nadhani Lowasa anaona mbali kuliko Makamba!
ReplyDeleteHuo ni ushauri wa bure na wabusara..safi sana bwana Lowasa kwa ushauri wa bure na wa hekima na busara. Mungu akubariki sana kuona hilo.
ReplyDelete