Monday, December 13, 2010

CUF sasa wapanguana madarakani

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
Joyce Mmasi na Sadick Mtulya
CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimewaondoa katika nafasi za uongozi, baadhi ya wakurugenzi na manaibu wao, hatua iliyoambatanana kupunguza idadi ya kurugenzi za chama hicho.

 CUF  pia imefanya mabadiliko katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu.

Maamuzi hayo yalipitishwa juzi katika kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, kilichofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.
Maalim Seif pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba jana aliliambia gazeti hili kuwa hatua hiyo,  inalenga katika kukiimarisha chama hicho kiutendaji .

Alisema kupunguzwa kwa idadi ya kurugenzi, pia kumetokana na baadhi ya wakurugenzi, kutaka kupumzika.

“CUF imefanya mabadiliko kadhaa katika kurugenzi zake na katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu. Tumepunguza kurugenzi kutoka sita hadi nne,’’ alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alizitaja kurugenzi mpya kuwa ni  Kurugenzi ya Utawala na Ulinzi, pamoja na Kurugenzi ya Uchumi na Fedha.

Nyingine ni Kurungezi  ya Haki za Binadamu, Habari na Uenezi  na Kurugenzi ya Oganaizesheni ya Siasa, Uratibu wa Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo hakuwa tayari kutaja majina ya viongozi walioteuliwa kushika  nafasi hizo na wale waliotemwa. 

Lakini kwa upande mwingine, chanzo chetu kilidokeza kuwa walioondolewa katika nafasi za uongozi ni Naibu Katibu Mkuu,  Mkurugenzi wa Habari na Uenezi na naibu wake.

Hali kadhalika, Mkurugenzi wa Siasa na naibu wake, na Mkurugenzi wa Blue guard na naibu wake. 

Habari za uhakika ziliema  Profesa Lipumba kwa kushauriana na katibu Mkuu wake, walilazimika kufanya madiliko ya wakuu hao wa idara. 

Kikao hicho cha siku mbili kilichofanyika Desemba 10 hadi 11,  kilikuwa kikijadili na kutathimini uchaguzi mkuu uliomalizika Oktoba 31 mwaka huu.

Habari zilisema mabadiliko hayo yalifikiwa baada ya kugundulika kuwa kuna mapungufu mbalimbali katika utendaji wa baadhi ya wakurugenzi.


Wakurugenzi waliopoteza nafasi zao ni pamoja na Mkurugenzi wa Siasa Mbarara Maharagande na naibu wake Salim Masoud, Ashura Mustapha, (Habari na Uenezi) na Mkurugenzi wa Blue Guard, Dk Juma Muchi na naibu wake Rajab Mazee. 

Habari zilisema kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi kumetokana na  aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kutokuwa na mahusiano ya kutosha na  vyombo vya habari. 

“Wajumbe wengi wa mkutano huo walionekana kukerwa na utendaji wa wakurugenzi hao na kumnyooshea vidole Mkurugenzi wa Idara ya Habari kwa madai kuwa mahusiano yake na waandishi wa habari, yamesababisha chama kufanya vibaya” kilieleza chanzo hicho.

Mabadiliko mengine yaliyofanywa na kikao hicho cha Baraza Kuu la CUF ni pamoja na nafasi ya unaibu katibu mkuu wa chama hicho kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Upande wa Tanzania  visiwani nafasi ya Naibu Katibu Mkuu  ilikuwa wazi baada ya Juma Duni Haji, kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya wa Zanzibar.

Nafasi hiyo sasa inashikiliwa na Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jusa Ladhu, wakati kwa upande wa Tanzania Bara, nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Joram Bashange, sasa itaongozwa na Julius Mtatiro.

Mtatiro aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria wa CUF. Mtatiro pia anashikilia kurugenzi zingine tatu za utawala, Ulinzi na Maadili. 

Wakurugenzi wapya ni Salim Hemed ( Mkurugenzi wa Maandalizi ya Uchaguzi na oganizesheni) na Naibu wake ni Shaweji Mketo, Salim Mandari (Fedha Mipango na Uchumi) na naibu wake ni, Zakia Omari.

Kwa upande wake, Salim Bimani anakuwa Murugenzi wa Habari Uenezi, Haki za Binadamu na Sheria na Naibu wake ni, Amina Ndovu. 

Baraza kuu pia lilipitisha jina la Mbunge wa Jimbo la Mtoni Zanzibar, Faki Haji Makame, kuwa msaidizi wa katibu Mkuu, kufuatia ombi lililotolewa na Maalimu Seif kutaka apate msaidizi.
                                          CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake