Tuesday, December 21, 2010

Jinsi ya kujisafisha na dhambi ya usaliti - 2

Kama utakumbuka msomaji wangu,  mada hii nilianza kuielezea wiki iliyopita pamoja na kuwepo kwa vipengele vinne vya mwanzo vya njia ya kujisafisha na usaliti, niliweka wazi nia yangu ya kusaidia watu waliokosana kwa usaliti lengo likiwa ni kumaliza tofauti zao.


Nashukuru mada hii imeweza kuchangia upatanisho wa wapenzi 26 ambao walikuwa wamesalitiana. Binafsi nimefarijika na jinsi watu walivyoheshimu ushauri wangu hata kwa njia ya simu na kuwa tayari kusamehe na kuanza upya maisha yao ya mapenzi yaliyokuwa yamevurugwa na  dhambi ya usaliti.
Naomba baada ya kusema hayo tuingie kwenye somo letu kwa kumalizia vipengele vilivyosalia.

TANO: Moja kati ya vitu vinavyoharibu au kuchochea migogoro au kuharibu uhusiano wa kimapenzi na kutokufikiwa kwa msamaha wa kweli ni kwa wapenzi wenyewe kuendelea kukumbuka mambo yaliyopita. Unapokuwa umeomba msamaha hebu lenga zaidi kujenga maisha mapya.

Mweleze mkeo jinsi unavyopanga kujenga nyumba ya familia au kumfungulia biashara, unavyojipanga kumuongezea kipato na mambo kama hayo ambayo yatamuonesha mwanga mpya wa maisha uliokuwa umepotezwa na hisia za kusalitiwa.

SITA: Usiombe msamaha kwa kutoa rushwa. “Sawa kanifumania sasa ninachoweza kufanya ni kumpa laki mbili ili yaishe.” Kumbuka kosa la usaliti halimalizwi kwa hongo bali kwa toba.

SABA: Uvumilivu ni suala muhimu kwenye kufikia msamaha wa kweli, ni vema ikafahamika kwamba, mkosaji anaweza kusahau mara moja kosa lake, lakini mkosewa hatarajii kumaliza maumivu yake ya kusalitiwa kwa siku moja, hivyo anatakiwa kuvumiliwa hasa pale anapokuwa na hali fulani ya kukumbuka kilichotokea.

“Nimefanya kosa, nimekuomba msamaha lakini bado huoneshi kunichangamkia leo siku ya sita!” Haifai kauli za namna hii uvumilivu unahitaji kuondoa maumivu.

NANE: Ipo faida ya kuomba msamaha mbele ya ndugu na rafiki wema. Wakati mwingine watendewa hujisikia furaha wanapoona wameangukiwa mbele ya watu. Ndani ya binadamu kuna chembe chembe za ushindi ambazo humletea mtu ukamilifu anapojiona amekuwa zaidi ya aliyeshindana naye.

TISA: Vipi Kuhusu hisia? Sote tunafahamu kuwa mambo kama hayo yanapotokea hali ya kupoteza hisia za mapenzi hujitokeza, ni jukumu la mhusika kuhakikisha kuwa anajenga upya msisimko wa mapenzi, jambo linalotajwa kusaidia kumletea ufafanuzi wa ziada msalitiwa na pengine kutambua kuwa usaliti ulichochewa na upungufu wa hali ya kujali na kujitolea katika mapenzi.

KUMI: Mwisho, kama msamaha wa mlalamikaji unaambatana na gharama au faini fulani, msaliti hana chaguo la ziada zaidi ya kukubali kulipa. Naomba nikomee hapa kwa leo.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake