KANISA Katoliki Parokia ya Familia Takatifu Jimbo la Sumbawanga, limegoma kuendesha ibada ya maziko kwa marehemu wawili wakidai ibada haitaendelea mpaka pale waumini ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotengwa na kanisa hilo, watakapoondoka ndani ya kanisa hilo.
Marehemu hao ni aliyekuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Msua iliyopo Manispaa ya Sumbawanga, Mekitrida Maufi ambaye ni mke wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Rukwa ambaye pia kwa sasa ni Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Patrick Maufi.
Maiti nyingine ambayo jina lake halikuweza kupatikana mara moja, ni ya mtoto wa darasa la nne ambaye pia shule aliyokuwa akisoma haijajulikana.
Tukio hilo lilitokea jana saa 8 mchana na lilidumu kwa saa tatu pale waombolezaji walipoleta miili ya marehemu hao kanisani hapo kwa ibada ya maziko.
Wengi wa waombolezaji hao walikuwa ni wanaCCM wakimsindikiza mfiwa na wengi wao walikuwa wameshatengwa kwa kinachodaiwa kuwa waliisaliti imani yao ya dini wakati wa Uchaguzi Mkuu kwa kumshabikia mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aesh Hilaly.
Baada ya waombolezaji kufika na majeneza ya miili hiyo mbele ya milango ya kanisa wakiwa tayari kuingia ndani, yalisomwa matangazo yaliyodai kuwa ibada ya kuombea marehemu haiwezi kufanyika hadi waumini waliotengwa (wanaCCM), watawanyike na wasionekane nje wala katika maeneo ya karibu na kanisa hilo.
Miongoni mwa waumini hao waliohudhuria, lakini wametengwa ni pamoja na mwenyekiti wa CCM Mkoa, Hypolitus Matete, Mwenyekiti CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Charles Kabanga, Katibu wa CCM Mkoa, Fraten Kiwango, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini aliyefahamika kwa jina moja la Tumombe na Diwani wa CCM Viti Maalumu Kata ya Sumbawanga, Aurelia Kanyengele.
Hali hiyo iliibua dhahama na kusababisha vurugu ya makundi mawili kati ya waliyotengwa na wanaounga mkono maamuzi hayo ambayo yalitiliwa nguvu na Paroko wa Parokia ya Kristu Mfalme, Pambo Mlongwa aliyefika maeneo hayo na kuwashinikiza mapadri waliokuwepo pale kuendelea na msimamo huo huo na kuwafanya waumini kuwataka waliokataliwa waondoke ili ibada ifanyike.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mjini, John Mzurikwao aliwataka waumini hao kwa kuwa wametengwa, watii maamuzi hayo na kuwasihi kuondoka hapo ili utaratibu wa ibada ya mazishi uendelee.
Viongozi hao baadhi walikubali na kurejea msibani, lakini baadhi ya waliotengwa walitoka nje ya uzio na kusubiri miili ya marehemu ili waungane na wenzao ili kwenda mazikoni. Ibada ya mazishi iliendelea.
Francis Chale ambaye ni Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM Wilaya ya Sumbawanga akizungumza na gazeti hili, alikiri si kutengwa tu, bali alivuliwa ukatoliki wake, akituhumiwa kumshabikia Hilaly ambaye ni Muislamu, aliyetuhumiwa na kanisa hilo kwa kuukufuru utatu mtakatifu katika moja ya mikutano yake ya kampeni alipojifananisha na Yesu Kristo kwa kuelezea dhana nzima ya mafiga matatu yaani Rais, Mbunge na Diwani.
“Kitendo hiki kimetusikitisha sana, tulidhani kwamba tumezuiwa tu kuhudhuria ibada za misa takatifu kumbe hata ibada za mazishi. Sasa kama hali ndio hiyo na kanisa linajitambulisha kwamba ni wakala wa Chadema, basi na sisi tuliotengwa tunajipanga tupandishe bendera ya Chadema kwa kila Parokia iliyopo katika jimbo hili,” alidai Chale.
Hivi karibuni, Parokia kadhaa za Jimbo Katoliki limewasimamisha waumini wake kwa madai ya kuisaliti imani yao kwa kutotii imani ya kanisa ambayo yaliwataka wasishabikie mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Katika msuguano huo wa kiimani, tayari kanisa hilo limewasimamisha na kuwatenga makatekista kwa madai wamelisaliti kanisa kwa kuwahamasisha waumini wao kumshabikia mgombea wa CCM.
Hata hivyo, kutokana na mchakato huo, kanisa hilo linajiandaa kutangaza orodha ya mapadri waliolisaliti hadharani ili nao waadhibiwe kama walivyoadhibiwa waumini hao.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake