Thursday, December 23, 2010

Krismasi, Mwaka mpya zinavyoweza ‘kulipaka rangi’ penzi lenu!

Ni kweli kabisa kwamba, kwa wapenzi walioshibana kila siku ni sikukuu kwao. Hata hivyo, sina budi kuwakumbushia baadhi ya mambo ambayo ni vyema wakafanyiana katika siku hizi za sikukuu nikiamini kwamba, wakiyafanya watakuwa katika nafasi nzuri ya kulifanya penzi lao lionekane jipya.


Tokeni muende kokote
Yawezekana katika kipindi chote cha uhusiano wenu hamjawahi hata siku moja kutoka pamoja kwenda kwenye ukumbi wa starehe ama sehemu yoyote tulivu.

Kimsingi kutoka na mwenza wako kuna faida kubwa sana, hivyo basi si vibaya katika sikukuu hizi zinazokuja mkajiandaa kwa kutenga fedha ambazo zitawafanya siku hiyo muende sehemu ambayo hamjawahi kwenda pamoja.

Kama wewe na mwenza wako mlikuwa na utaratibu wa kwenda ‘out’ kila wikiendi, safari hii mnaweza kupanga kwenda sehemu tofauti, ikiwezekana hata kutoka nje ya mji mnaoishi.

Kuna mengi ya kufanya mnapotoka ‘out’, mojawapo ni kubadilishana mawazo juu ya maisha yenu, kuombana msamaha pale ambapo mlitokea kutofautiana. Yaani ni kipindi cha kulikarabati penzi lenu na hata pale mtakapokuwa mnarudi itakuwa ni kama vile mmefungua ukurasa mpya.

Kununuliana zawadi
Siku zote zawadi ni chachandu katika penzi. Kumbuka kwamba katika suala la uhusiano, zawadi ni zawadi bila kujali ukubwa wake. Hii itategemea tu na uwezo wako.

Kwa maana hiyo basi ni vizuri ukamwandalia zawadi nzuri mwenza wako ambayo itamfanya afunge na kufungua mwaka mpya kwa matumaini kwamba kweli unampenda.

Kadi za Sikukuu
Hili kwa wengine ni kama kuwakumbushia. Unapaswa kumwandalia mpenzi wako kadi ya kumtakia Krismasi njema na mwaka mpya wenye furaha.

Kumbuka kadi utakayomnunulia mwenza wako inatakiwa kuwa tofauti na ile utakayompelekea rafiki yako wa kawaida au mzazi wako. Ni muhimu sana kulizingatia hili. Angalia rangi za kadi, ujumbe na ukubwa wa kadi.

Hakikisha kadi utakayompelekea laazizi wako inamvutia na kumfanya atamani kuisoma kila mara kutokana na jinsi ilivyo.

Mfanyie ‘surprise’
Rafiki yangu mmoja amenieleza kwamba, katika Sikukuu ya Mwaka mpya anatarajia kumshangaza mpenzi wake ‘surprise’ kwa kumtamkia kwamba, wakati umefika wa wao kufunga ndoa. Wewe umejiandaa kumfanyia ‘surprise’ gani mpenzi wako?

Ni siku za furaha
Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba, hakuna kitu kibaya kama wapenzi katika siku hizi kununiana ama kuudhiana. Hizi ni siku za furaha hivyo basi, hakikisha unafanya kila uwezalo kumfanya mwenza wako awe na uso wa tabasamu muda wote.

Hivi itakuwaje pale mtakapokuwa mnaposherehekea Sikukuu ya Mwaka mpya kisha mpenzi wako akababatiza ujumbe wa mapenzi katika simu yako kutoka kwa mtu mwingine? Ikitokea hivyo itakuwa ni nuksi kwa mwaka mzima.

Ndio maana nasema jitahidi sana katika sikukuu hizo kuyaondoa yale makovu yaliyokuwa katika penzi lenu ili muingie katika mwaka mpya penzi lenu likiwa na uhai mpya. Hakikisha tu unajiandaa vizuri na ndiyo maana nimeamua kuandika makala haya mapema kabisa.

Labda kwa kumalizia niseme tu kwamba, kila atakachokufanyia mwenza wako, kiwe kidogo ama kikubwa ni vyema ukakithamini.
Ni hayo tu, nawatakia Krismasi njema na mwaka mpya wenye mafanikio.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake