Monday, December 13, 2010

Profesa Nyang'oro aeleza sababu za kuandika kitabu cha JK

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akitia saini kitabu cha wasifu nakala ya Mama Salma Kikwete wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho. Profesa Julius Nyang'oro (pichani katikati) ndiye mwandishi wa kitabu hicho.

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Viongozi wa Serikali, Waalikwa, Mabibi na Mabwana;



Ni furaha kubwa kwangu kuweza kushiriki katika uzinduzi wa majuzuu mawili ya kitabu juu ya Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya yote, napenda kutumia fursa hii kumpongeza Rais kwa ushindi wake wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni. Kutokana na raghba yangu ya kitaaluma na raghba ya kufanya utafiti juu yake, nilifuatilia uchaguzi huo kwa karibu na ninakiri kwamba nilivutiwa na ushupavu wake alipokuwa anasafiri sehemu mbalimbali za nchi, akiomba kura. Siku ya kuhitimisha kampeni kwenye Viwanja vya Jangwani, nilikuwa miongoni mwa waliohudhuriwa na nilivutiwa sana alipotaja maelfu ya kilomita alizosafiri wakati wa kampeni, mamia ya saa alizotumia angani akieleza kwa nini anataka kuchaguliwa tena na mamia ya hotuba alizotoa. Hongera sana Mheshimiwa.

Aidha, nawatakia wote siku njema ya kusherehekea Uhuru.

Kitabu hiki ni matokeo ya mradi uliochukua miaka mitatu. Namshukuru Rais kwa kukubali ombi langu la kumhoji mara kadhaa, mbali na ratiba yake nzito. Natoa shukrani za pekee kwa wasaidizi wake kadhaa ambao walikuwa muhimu sana katika kuandaa mahojiano na kwa kuandaa uziunduzi huu wa kitabu.

Aidha, natoa shukrani za pekee kwa Profesa Imani Swilla kwa kushiriki katika mradi huu. Yeye aliandaa tafsiri ya Kiswahili ya kitabu hiki. Napenda pia kumshukuru Profesa Severine Rugumamu kwa kukubali kutoa tathmini na maoni juu ya kitabu hiki wakati huu wa uzinduzi. Lakini, napenda kusema kwamba kama mwandishi wa kitabu hiki, nawajibika kwa mapungufu yoyote yaliyomo kwenye kitabu.

Nathamini sana mradi huu kwa sababu kadhaa. Wazo la kuandika kitabu juu ya JK liliniijia kwa mara ya kwanza nilipotambua kwamba hakuna wasifu mkubwa wowote ulioandikwa juu ya rais wa Tanzania tangu wasifu wa Mwalimu Julius Nyerere ulioandikwa na William E. Smith mwaka 1971. Kwa hiyo, niliamua kuanza kuziba pengo lililopo kwa kufanya utafiti juu ya JK. Ingawa William E. Smith alifanya kazi nzuri sana alipoandika wasifu wa Mwalimu, mara nyingi nilisumbuliwa na kitu kimoja: Smith siyo Mtanzania. Niliwaza kuwa kuna watu wengi nchini ambao, kama Smith, wanaweza kuandika vizuri juu ya viongozi wetu. Ndiyo maana niliamua kuandika juu ya wasifu wa JK.

Uamuzi wa kuandika juu ya JK ulisukumwa na sababu nyingine binafsi. Ingawa JK ananizidi kidogo umri, yeye ni rais ambaye kisaikolojia ninahusiana naye kwa sababu tumeishi katika vipindi vinavyofanana na tumekua katika miaka ya 1960, 1970 na 1980.

Nilipofuatilia mabadiliko na maendeleo yake kama mtu, mwanasiasa na mtumishi wa umma, nilikumbuka mambo mengi ambayo mimi mwenyewe niliyapitia nyakati hizo, kwa mfano: matembezi marefu ya kuunga mkono Azimio la Arusha mwaka 1967. Ingawa nilikuwa mdogo mno kuweza kushiriki kwenye matembezi hayo, nakumbuka baadhi ya watu niliosoma nao ambao walitembea mamia ya maili kwenda Dar es Salaam kumpongeza Mwalimu juu ya Azimio la Arusha; Mwongozo wa 1971; Jeshi la Kujenga Taifa ambapo nilikutana na watu ambao wamekuwa ni rafiki wa kudumu; Azimio la Musoma la 1975; mchango wa Tanzania katika ukombozi wa kusini mwa Afrika; kuingia madarakani kwa Rais Ali Hassan Mwinyi na mwishowe, kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kuchaguliwa kwa Rais Mkapa mwaka 1995.

Hatimaye, ushindi wa JK kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka 2005 uliokuwa wa kishindo. Ni nadra ulimwenguni kote kwa mgombea wa chama kilichopo madarakani kushinda kwa idadi aliyoshinda JK: zaidi ya asilimia 80 ya wapiga kura walimchagua kuwa Rais wa Tanzania. Kama mwanataaluma wa siasa, nilivutiwa sana na ushindi wa JK, ulioelezwa wakati huo kuwa ushindi wa tsunami.

Matukio yote haya yalikuwa muhimu sana katika historia ya siasa ya nchi yetu. Nilipokuwa naandika juu ya matukio haya kuhusiana na mabadiliko na maendeleo ya JK kama kiongozi, nilikumbuka mambo mengi ambayo ni vigumu mtu kuelewa kama hakuyapitia. Changamoto kubwa kwangu kama mwanataaluma ilikuwa ni kutofautisha kumbukumbu zangu na tathmini halisi ya vipindi hivyo. Katika maisha, naelewa kwamba huwezi ukachunguza kitu bila kuwa na maoni yako. Ni wazi kwamba uelewa wangu wa siasa za Tanzania unatokana na matukio hayo niliyoshiriki. Lakini ni matumaini yangu kwamba uchambuzi wangu wa vipindi mbalimbali katika kitabu hiki unaonyesha uelewa wangu wa Tanzania, bila kuathiri uchambuzi wangu wa kitaaluma.

Moja ya sababu kubwa ya utafiti wangu juu ya JK ni kwamba naona kuwa urais na uongozi wake umekuja wakati nchi inakabiliana na changamoto kubwa. JK ni rais wa kwanza wa Tanzania ambaye hakushiriki katika mapambano ya kupata uhuru. Alikuwa na umri wa miaka 12 Tanganyika ilipopata uhuru. Vipindi vya urais wa Mwalimu, Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa vilikuwa ni vipindi vya kuimarisha uzalendo na uhuru.

Changamoto za vipindi vya mwanzo ni tofauti na zile ambazo zinaukabili urais na uongozi wa JK. Ingawa moja ya changamoto ya JK ni kuimarisha mshikamo wa kitaifa, lakini changamoto muhimu zaidi kwa wakati huu ni kuleta maendeleo ya uchumi, kwenye mazingira magumu zaidi ya mfumo wa uchumi wa ulimwengu. Mfano mzuri wa swala hili ni kuhusu hali ya vijana wa nchi hii. Ni wazi kwamba vijana ni kundi muhimu sana, ukizingatia ukweli wa masuala ya idadi ya watu nchini.

JK atakuwa mtu wa kwanza kukiri kwamba ni vigumu kumaliza kiu ya ajira ya vijana, elimu yao na masuala mengine. Yeye mwenyewe alisaidia katika kuikuza kiu hii wakati wa kampeni za urais za mwaka 1995 na 2005. Wakati wa kampeni zote mbili, aliyapa umuhimu zaidi maslahi ya vijana.

Aidha, changamoto anazokumbana nazo JK ni ngumu zaidi kuliko za waliomtangulia kwa sababu ya mabadiliko ya kiteknolojia ambayo yamwezesha kila mtu, hata vijijini, kupata taarifa juu ya maendeleo ya kitaifa na matukio ulimwenguni. Kwa hiyo, kila wakati, utendaji wake unalinganishwa na utendaji wa viongozi ulimwenguni kote. Hii ni changamoto kubwa kwa rais.

JK kama kiongozi anapaswa kuelewa matarajio ya wananchi na hapana shaka kwamba anaelewa. Nilipokuwa naandaa kitabu hiki na kumfuata wakati wa baadhi ya ziara zake mikoani, nilielewa kwamba anaelewa fika changamoto hizi na anaweza kukabiliana nazo. Aliwasiliana vizuri na watu aliokutana nao na alioenekana kuelewa changamoto zao za kila siku. Hii inaeleweka kwa sababu yeye mwenyewe alikulia katika mazingira ya kawaida na anaelewa vizuri maisha ya kila siku ya watu wa kawaida. Namtakia mema na kila la heri katika jitihada zake kwa sababu mafanikio yake yataboresha hali ya kiuchumi na kijamii ya wananchi.



Kama wote mnavyojua, kuandika kitabu ni jambo lenye upweke sana. Mradi huu haukuwa tofauti. Mradi kama huu unahitaji muda, umakini, tafakari na uvumilivu. Nilipitia yote haya. Lakini najua kwamba nisingeweza kufanikisha mradi huu bila familia yangu kujitoa: mke wangu Alu na watoto wetu Alma na Yusuf. Walivumilia kutokuwepo kwangu kwa mara nyingi, wakati nikifanya utafiti wa kitabu hiki. Nawashukuru sana kwa kuelewa hali hii. Kwa njia moja au nyingine, wao walinitia moyo na kunihimiza kumaliza kitabu. Kwa hiyo, kitabu hiki nimekiandika kwa heshima yao na kwa heshima ya wazazi wangu ambao mapenzi yao yamekuwa ni faraja kubwa kwangu siku zote.

Napenda pia kuwashukuru marafiki zangu wengi, baadhi yao ambao wapo hapa leo, kwa kuniunga mkono na kunitia moyo wakati nikiandika. Nimewataja baadhi yao kwenye kitabu kwa sababu tumeshirikiana mambo mengi kwenye maisha na kwa sehemu kubwa, tulifurahia mambo mengi hayo.

Bila kutaja majina, nawashukuru watu wengi ambao niliwahoji na baadhi yao wapo hapa nasi. Ni matumaini yangu kwamba tafsiri ya matukio tuliojadili yanalingana na uchambuzi wenu mliofanya nilipowahoji.

Africa World Press, mchapishaji wa kitabu hiki, alifanya kazi nzuri sana kwa kukitoa kitabu katika muda mfupi sana na kushughulikia masuala yote ya itifaki na kitaalamu. Napenda pia kulishukuru Duka la Vitabu la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kukubali kuwa msambazaji pekee wa kitabu nchini. Najua ni jukumu kubwa sana lakini naamini kwamba watafanya kazi nzuri.

Kwa kuhitimisha, napenda kwa mara nyingine, kumshukuru Rais kwa kunipatia muda wakati nafanya utafiti. Kama nilivyosema kwenye utangulizi wa kitabu, hili ni juzuu la kwanza la mradi wangu. Tayari nimeanza kufanya uchambuzi makini wa matokeo ya sera zake kwa ajili ya hatua nyingine ya mradi huu. Naamini kwamba wote mnanitakia mema katika jitihada zangu, kwa sababu kama nilivyosema mwanzoni mwa hotuba hii, tunahitaji aina hii ya utafiti ili kuhifadhi historia ya nchi yetu.

Ni matumaini yangu kuwa watu watapata muda wa kusoma kitabu tunachozindua leo. Nimerahisisha suala zima kwa kutayarisha matoleo ya Kiswahili na Kiingereza ya kitabu hiki. Lililobaki ni kwenu kukisoma.

Asanteni sana.

1 comment:

  1. I am proud of you Professor J Nyango’ro. I am so glad that it is you who did realized that there is a need to write such kind of book. Keep it up Shemeji
    Asha, Dallas.

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake