Saturday, December 18, 2010

Rais wa Fifa aipongeza TP Mazembe

Rais wa Shirikisho la soka duniani-Fifa, Sepp Blatter, amesema kuingia hatua ya fainali kwa timu ya TP Mazembe kutafuta klabu bingwa ya soka duniani, inaonesha namna soka ya Afrika inavyopiga hatua kubwa.
Sepp Blatter
Sepp Blatter
TP Mazembe ambao ni mabingwa wa soka wa Afrika, watamenyana na mabingwa wa soka wa Ulaya, Inter Milan ya Italia leo Jumamosi.

Akizungumza akiwa Abu Dhabi ambapo mashindano hayo yamekuwa yakifanyika, Blatter ameipongeza klabu hiyo ya Afrika .
Amesema: "Mazembe itaandika ukurasa mpya katika historia ya soka siku ya Jumamosi, kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika fainali ya mashindano hayo."
Blatter amebashiri itakuwa mechi kali na ya kusisimua. Mazembe dhidi ya Inter Milan, ambao ni mabingwa wa Ulaya, ni mechi kubwa," aliendelea kufafanua.
Mazembe imekuwa ni timu ya kwanza kutoka nje ya bara la Ulaya na Amerika Kusini, kufuzu hatua ya fainali ya mashindano hayo, baada ya kuwalaza mabingwa wa Amerika Kusini, SC Internacional ya Brazil waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kunyakua kombe hilo.
Wachezaji wa TP Mazembe wakishangilia
Wachezaji wa TP Mazembe wakishangilia
Rais wa Fifa, Blatter amesema mchezo huo unatoa nafasi muhimu na ya pekee kwa Afrika kuonesha ni miongoni mwa vigogo wa kusakata soka duniani.
Baada ya kocha wa Internacional, Celso Roth kuonesha mshangao namna vijana hao wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, walivyocheza dhidi ya timu yake, Mbrazil mwengine anayechezea, Inter, Maicon, amesema timu yake haitawadharau nyota hao wa soka kutoka Lubumbashi.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake