Shinikizo kutoka jamii ya kimataifa inazidi kuongezeka ili kumlazimisha rais wa sasa wa Ivory Coast Laurent Gbagbo kukubali kuwa alishindwa katika uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita.
Umoja wa mataifa ambao unamuunga mkono mpinzani wa bwana Gbagbo, Alassane Ouattara, kwa sasa umeripotiwa kukubali stakabadhi za mjumbe anayemwakilisha bwana Ouattara kuwa ndiye mwakilishi wa Ivory Coast katika umoja huo.
Hatua hiyo imejiri baada ya benki ya dunia kutangaza kuwa imefutilia mbali misaada yote ya kifedha kwa Ivory Coast.
Serikali ya Marekani imesema inajadili kuhusu njia za kuimarisha kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa nchini Ivory Coast, ambacho kwa sasa kinamlinda bwana Ouattara na serikali yake ya mpito.
Matumizi ya nguvu za kijeshi
Wakati huo huo waziri mkuu aliyeteuliwa na Alassane Ouattara, Guillaume Soro, ametowa wito kwa jamii ya kimataifa kutuma wanajeshi nchini humo ili wamwondoe Laurent Gbagbo madarakani.
Bwana Soro amekiambia kituo cha televisheni cha Ufaransa kwamba vikwazo vinavyotolewa na jamii ya kimataifa vimeshindwa kumshawishi bwana Gbagbo kuondoka na kwamba njia ya pekee iliyosalia kusuluhisha mgogoro wa Ivory Coast ni kutumia nguvu.
No comments:
Post a Comment