SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limetupia lawama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa madai kuwa mkakati walioanzisha wa kukagua uingiaji bidhaa bandia, haujazingatia taratibu zinavyotakiwa.
Akitoa taarifa kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyrill Chami, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, alisema mkakati huo umekuwa hauzingatii alama za ukaguzi wa bidhaa nchini.
Ekelege alitoa mfano kuwa, rangi zinazotumiwa kufanya ukaguzi wa bidhaa pindi zinapoingia nchini, hazizingatii utaratibu na kwamba rangi ya kijani inapowaka, gari huruhusiwa kupita bila kufanyiwa ukaguzi jambo linalochangia bidhaa bandia kuongezeka.
“Mkakati huo bado, haujazingatia utaraitibu ipasavyo na wizara inahitaji kuliangalia kwa kina pamoja na TRA, ili kuweza kuthibiti hali ya uingiaji bidhaa bandia nchini,” alisema Ekelege.
Hata hivyo, Ekelege alisema baadhi ya viongozi na wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamika kutokuwapo kwa shirika la viwango visiwani, kimekuwa chanzo cha wafanyabiashara kupata upenyo wa kutumia njia za panya kuingiza bidhaa bandia.
Alisema kwa kuliona hilo, wanaomba wizara husika kulingalia kwa kutafuta njia mbadala ya kulitatua.
“Kwa kweli waziri tatizo hili linapaswa kuangaliwa kwa kina hata unapokaa na wenzako kwenye vikao, ni vema mkalizungumzia ili tuweze kuthibiti uingiaji bidhaa bandia,” alisema na kuongeza:
“Kwa sababu njia hizi za panya zinaonyesha ni mwanya mkubwa kwa wafanyabiashara wakubwa kupitisha bidhaa bandia na inaathiri afya ya walaji.”
Hata hivyo, Dk Chami alisema malalamiko ya Zanzibar kutokuwa na shirika la viwango, ameyapokea na kuahidi kuyafikisha kwenye kamati ya makamu wa rais ili kutafutiwa ufumbuzi.
“Nimesikia malalamiko hayo na ninaahidi nitahakikisha ninayafanyia kazi, kwa kulipelekea kwenye Kamati ya Wizara ya Makamu wa Rais (Muungano),” alisema Dk Chami.
Dk Chami alisema serikali inapaswa ikubali kwamba suala la uingiaji bidhaa bandia limekuwa sugu nchini na kwamba, kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha TBS, TRA, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Wizara ya Chakula, Kilimo na Ushirika, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Maji na Mambo ya Ndani, wanapanga mkakati wa kuondoa tatizo hilo.
“Ninachoomba hapa ni TBS, itoe maelezo ya kuomba ushirikisho wa wizara zote, ili kujadili bidhaa mtambuka zinazoingia sokoni bila kufanyiwa ukaguzi,” alisema.
Dk Chami alitaka wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa bandia kubadilika na kuondoa visingizio vya bidhaa zenye ubora zina gharama.
“Ni vema wakabadilika na kuacha kuendekeza kununua bidhaa bandia ambazo zina athari kwa watumiaji, wasidhani tunafanya utani kwani hatua tutakayochukua wasije kulaumu baadaye,” alisema.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake