NA NJUMAI NGOTA
SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kusitisha mkataba na Kampuni ya Udalali ya Majembe ifikapo Ijumaa ijayo. Mbali na hilo, imewataka wapiga debe waondoke mara moja katika vituo vyote vya mabasi kutokana na kuwa kero kwa abiria na wasafirishaji. Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alitoa maagizo hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mapendekezo ya utekelezaji hoja zilizowasilishwa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kutokana na matatizo waliyonayo.
Nundu alisema juzi walikutana na viongozi wa TABOA na Wamiliki wa Mabasi ya Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA) na kujadili matatizo yao, ambapo waliafikiana kuwa yapo mambo yatakayotekelezwa kwa muda mfupi na mengine mrefu. Alisema ili kuondokana na kero za kampuni hiyo, ameiagiza SUMATRA kusitisha mkataba huo, kwani inafanya kazi kwa vitu ambavyo havipo katika mamlaka yake.
“Tumewaagiza SUMATRA wasitishe mkataba kati yake na Majembe ifikapo Desemba 31, mwaka huu, waachane kistaarabu na hawatakuwa wanafanya kazi za SUMATRA,” alisema. Alisema kutokana na utata uliojitokeza kuhusu ukaguzi wa madaraja ya mabasi, SUMATRA wanapaswa kufanya kazi hiyo wenyewe, jambo ambalo wameanza kulitekeleza kuanzia Desemba 9, mwaka huu. Nundu alisema Majembe ilikuwa kero kutokana na kufanya kazi za usalama jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Miongoni mwa kazi hizo alisema ni kufanya ukaguzi wa matairi, vioo na bima.
Waziri Nundu aliitaka SUMATRA itayarishe mfumo wa kazi, ambao utashughulikia mambo yote yanayopaswa kufanywa na mamlaka hiyo kisheria, kwa kuwaandaa wafanyakazi wake na kuwafundisha sheria. Akizungumzia wapiga debe, aliagiza waondoke mara moja vituoni, kwani wamekuwa kero kwa abiria na wasafirishaji. Nundu aliwataka wapiga debe wakatafute shughuli nyingine za kufanya, kwani usafiri unaweza kufanyika bila tatizo pasi na wao kuwepo.
Aliagiza mamlaka zinazohusika ziandae utaratibu wa kuwatambua wafanyakazi na mawakala wa kampuni za mabasi, vikiwemo vitambulisho maalumu vitakavyowasaidia abiria. Alisema utaratibu huo uwe umekamilika Januari 15, mwakani. Kuhusu nauli za mabasi, Nundu alisema suala hilo linapaswa lifanyiwe kazi na ifikapo Januari 31, mwakani liwe limepatiwa ufumbuzi. Alisema kazi hiyo ifanywe na SUMATRA kwa kushirikiana na wamiliki wa mabasi, kabla ya kikao cha wadau.
Waziri Nundu akizungumzia suala la wageni kujihusisha na usafirishaji abiria, alisema wizara itaangalia sheria zilizopo ili kuhakikisha hazikiukwi. Pia ameiagiza SUMATRA kuwa makini na kuhakikisha Sheria za Usajili wa Kampuni zinafuatwa kabla ya kutoa leseni ya usafirishaji. Kuhusu matatizo ya mabasi kuingia kwenye kila kituo na kulipa ushuru wa halmashauri za wilaya, kutembea usiku na kuondolewa matuta barabarani, alisema yataangaliwa ili kuona namna ya kuyatatua.
CHANZO:UHURU
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake