Friday, December 24, 2010

Zijue faida, hasara za kupenda kwa hisia

Uhali gani mpenzi wa kona ya mahaba popote ulipo, kuchangia kwako mada imeonyesha jinsi gani kona hii inavyosomwa na watu wengi na kuelewa kinachoandikwa kwa hilo nasema asante sana. Sitapenda kula muda wenu kwa mazungumzo mengi ila hapa ni kazi tu.

Nina imani somo la wiki hii linasomeka vizuri hapo juu, nimeamua kuandika mada hii nikiwa na maana maalumu kutokana na maswali mengi kutoka kwenu. Najua utajiuliza mtu hupenda vipi kwa hisia?
Kupenda kwa hisia ni kupenda kitu usichokijua bali kukikisia kwenye mawazo yako.

Mtu anapendaje?
Kwa mfano kutokana na ulimwengu kupiga hatua ya masiliano watu wamekuwa wakipata marafiki kwa njia ya mawasiliano. Kwa mtu kutafuta marafiki kwa njia ya magazeti au barua pepe na sasa kuna ‘face book’.

Baada ya mtu kupata ujumbe toka kwa mtu asiyemjua kwa kusikia sauti yake, basi hapo mtu hujenga hisia mtu huyu yupo vipi. Sauti huwa haibebi uhalisia wa mtu. Sauti siku zote haiambatani na umbile au sura.

 Kutokana na mtu kujenga hisia kichwani mwake kuwa anayezungumza naye yupo vipi hapo kila mmoja huonyesha mapenzi mazito kwa mwenzake kufikia hatua ya kuahidiana hata ndoa bila bila kujuana. 

Nini faida na hasara zake?
Japo mapenzi ni bahati nasibu ni kosa kuitengenezea akili yako kiumbe ambacho hujakiona na kuamini vile uwazavyo ndivyo kweli. Tatizo linakuja kwa upande mmoja pale mnapokubaliana mkutane na kufanikiwa kukutana. 

Faida yake:
 Kumpata yule uliyemfikiria akilini mwako, lakini hasara ni kukuta tofauti na jinsi ulivyomuwazia akilini mwako.

Nini kinafuata:
Moyo wako hukata tamaa na mapenzi huyeyuka ghafla wakati mwenzako huenda amevutiwa na wewe. Sehemu hii huwa mbaya kwa yule aliyependa na kulikosa lile penzi alilolitalajia.

Hukatazwi kupata mpenzi wa mbali kwa njia ya mawasiliano lakini nafikiri si vizuri kutangaza mapenzi hata kufikia hatua ya kuvunja mapenzi na rafiki yako wa zamani kwa vile sauti tu imekuchanganya na kumuumba akilini jinsi atakavyokuwa.

 Unapopata rafiki wa mbali ni vizuri kama kweli mna nia ya  kutaka kujenga uhusiano wa kudumu. Mjitahidi mkutane ili kujuana na kuweza hata kuchunguzana tabia. Hii itawasaidia watu kukipata kitu cha kweli si cha kukihisia.

Vile vile lazima tuwe makini kuanzisha uhusiano na mtu wa mbali kwa kuweza kuijua historia yake ili usijiingize kwenye mateso ya kujitakia. Huenda yule mpenzi wako ni mke au mume wa mtu, lakini kwa vile kuna kitu kimemvutia kwako ameamua kukuficha hasa sauti.

Ni makosa kuufungua moyo wako kwa mtu usiyemjua vizuri usiwe mtumwa wa mapenzi wa kupenda bila kufikiri. Hiki ninachokipenda kina faida na hasara zipi. Hili limekuwa tatizo kubwa kwa watu pale penzi linapokosa muelekeo.

La muhimu ni kukutana kila mmoja kujaribu kuijua historia ya mwenzake kuliko kukurupuka bila kujua mwenzako yupo vipi. Hii itasaidia mtu kuepusha kupenda kwa hisia na kumpata yule anayemjua vizuri.

Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo. Nawatakia sikukuu njema ya Krismasi. Kwa maoni maswali au ushauri tuwasiliane kwa anuani zilizo katika ukurasa huu.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake