Mussa Juma, Arusha na Salim Said
MAELFU ya wakazi wa Arusha na miji ya jirani jana walijitokeza katika maombolezo makubwa ya watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano ya Chadema yaliyofanyika Januari 5 mwaka huu.Katika maombolezo hayo, maelfu ya watu walifanya maandamano ya amani kutoka chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru hadi viwanja vya NMC na kusababisha barabara kadhaa kufungwa.Kuanzia majira ya saa 2:00 asubuhi, umati wa watu ulikuwa umefurika katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mount Meru hadi majira ya saa 7:35 mchana miili ya Denis Shirima na Omar Ismail ilipoondolewa.
Vurugu zaibuka hospitali
Kabla ya kuondolewa miili hiyo chumba cha maiti, vurugu kubwa zilizuka baada ya wananchi kulalamikia uchunguzi wa miili hiyo uliokuwa unafanywa na polisi na madaktari kuchukuwa muda mrefu.
Awali ilipangwa miili hiyo kuondolewa saa nne asubuhi, lakini haikuwezekana kutokana na polisi na madaktari kutokamilisha uchunguzi kwa wakati.
Wananchi hao, wengi wao vijana walikuwa wakiimba: "tunataka miili ya mashujaa wetu... tunawapa dakika tano, tunachukuwa kwa nguvu".
Hata hivyo, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema, walifanikiwa kutuliza ghasia hizo baada ya kuzungumza na wananchi kisha kwenda chumba cha maiti kusimamia zoezi la uchunguzi.
Baadaye miili hiyo, iliondolewa katika chumba hicho na kupitishwa katika barabara za Afrika ya Mashariki, Goliondoi na Sokoine ambako mamia ya watu walikuwa wamesimama kando ya barabara wakiwa na bendera za Chadema na wengine wakipunga mikono.
Katika maandamano hayo, miili hiyo iliyokuwa kwenye gari maalum alilopanda Mbowe na ndugu wa marehemu ilifika Uwanja wa NMC, ambako maelfu ya watu walikuwa wamefurika kuipokea.
CCM, Serikali wakacha ibada
Baada ya kufika uwanjani hapo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila aliongoza wimbo wa taifa wa kupokea miili hiyo ulioimbwa kwa kuongezwa maneno kama "Mungu wabariki Chadema na watu wake na viongozi wake".
Baadaye sala za dini mbalimbali zilianza huku umati wa watu ukiwa kimya na wengine wakijitokeza kutoa sadaka zao na rambirambi kwa wafiwa.
Hakuna kiongozi yoyote wa Serikali na CCM aliyeshiriki ibada ya kuaga miili ya watu hao.
Chadema yatoa masharti
Chadema jana pamoja na kufanya maandamano na mkutano wa hadhara kwa ajili ya kuwaaga waliokufa kwenye vurugu za Arusha ilitoa masharti saba kwa Serikali, ikiwamo kujiuzulu na kufunguliwa kesi za jinai kwa IGP, Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha.
Mbowe alisema alipokuwa akisoma tamko la chama hicho kuwa katika kuhakikisha masharti hayo yanafuatwa na madai kutekelezwa, chama hicho kimewaelekeza viongozi, wanachama na wafuasi wake nchini, kuandaa maandamano ya amani kwa ajili ya kulaani mauaji hayo.
"Chadema taifa itatuma maafisa wa ngazi za juu wa chama, wakiwemo wabunge na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kushiriki maandamano hayo kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuyaongezea nguvu na hamasa," alisema Mbowe na kuongeza: “Ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Tanzania. Ni siku ya kihistoria.”
Kwa mujibu wa Mbowe, masharti mengine katika kulipatia ufumbuzi suala hilo ni kujiuzulu pia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye na kufunguliwa mashtaka ya jinai na kufutwa kwa kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya viongozi na wanachama wa Chadema kwa ajili ya kujihusisha na maandamano hayo.
Mbowe alifafanua kuwa kujiuzulu kwa IGP Mwema, Waziri Nahodha na RPC Andengenye kutapisha uchunguzi huru na wa kina wa matukio yote yaliyosababisha wananchi hawa kuuawa na mamia kujeruhiwa huku wengine kadhaa wakikamatwa bila sababu.
"Kesi walizofunguliwa viongozi na wafuasi wa Chadema, zifutwe bila masharti na kuanzia sasa, viongozi hao hawatahudhuria tena mahakamani kusikiliza kesi hizo za uongo," alisema Mbowe.
Mbowe ataka uchaguzi wa umeya upya
Mbowe pia alisema Chadema imetaka matokeo ya uchaguzi wa umeya Arusha yafutwe na uchaguzi uitishwe mpya na kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kwa ajili ya kuchunguza vurugu za Arusha.
“Damu iliyomwagwa Arusha inalilia haki, roho za wote waliotolewa mhanga na polisi zinahitaji haki ili ziweze kutulia na mizimu yao ipumzike. Wote walioumizwa na ujambazi wa polisi wanalilia fidia ya kuuguza maumivu yao ya kimwili, ya kiroho na ya mali zao zilizoharibiwa,” lilisema tamko hilo lililotumwa kwa vyombo vya habari muda mfupi kabla Mbowe hajalisoma akiwa Arusha.
Tamko hilo limeongeza “Sheria za nchi yetu zilizokanyagwa chini kana kwamba hazipo zinahitaji kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine wa aina hii.”
“Sisi sote tuliokusanyika hapa leo, na wale wote wanaotusikiliza na kutuangalia mahali popote nchini na hata nje, tuna jukumu la kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wale ambao tunaomboleza vifo vyao,” linaendelea tamko hilo.
Kwa mujibu wa Mbowe, Chadema ina jukumu la kuhakikisha haki inapatikana kwa wale wote walioumizwa kwa risasi na mabomu na virungu.
“Tuna jukumu la kuhakikisha wale wote ambao waliharibiwa mali zao kwa sababu ya uhalifu huu wa polisi wanafidiwa kwa kiasi chote cha hasara waliyoipata na kwamba polisi hawarudii tena ujambazi wa aina hii dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia yoyote kwa kuwawajibisha wale wote walioshiriki,” alisema na kuongeza:
“Fidia stahili ilipwe kwa mujibu wa sheria husika za nchi kwa ndugu na jamaa wa waliouawa kutokana na polisi na walioumizwa kwa namna yoyote ile au kuharibiwa mali zao kutokana na vurugu hizo.”
….Tume huru ya majaji
Mbowe aliitaka Serikali kupitia mahakama, kuunda Tume huru ya uchunguzi ya kimahakama (Judicial Commission of Inquiry) itakayoundwa na majaji wa Mahakama ya Rufani ya nchini ili kufanya uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa matukio yote yaliyosababisha IGP Mwema kupiga marufuku maandamano ya amani na mkutano wa hadhara.
Alisema agizo hilo ndilo lililoambatana na Jeshi la Polisi kufanya vurugu na kusababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia.
“Tunapenda kusisitiza kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kwa sababu historia ya tume nyingine ambazo zimeundwa kwa utaratibu wa Rais kuteua watu anaowataka inaonyesha zimefanya kazi zao za uchunguzi mafichoni bila kushirikisha wadau wengine na bila wananchi kufahamu kitu kinachoendelea,” alisema Mbowe na kusisitiza:
“Matokeo ya tume nyingi za namna hii ni kwamba ripoti zake zimepuuzwa au kufichwa na watawala, lakini tume ya uchunguzi ya kimahakama hufanya kazi zake kwa uwazi, uhuru na huruhusu wananchi kuhudhuria au kushiriki moja kwa moja kwa kutoa ushahidi au kuhoji mashahidi wengine wanaotoa taarifa kwenye tume hiyo.”
Alisema mauaji ya Arusha yanathibitisha wazi mahitaji ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na marekebisho ya dhati ya sheria nyingine za nchi ikiwa ni pamoja na ya Jeshi la Polisi na ya vyama vya siasa.
Hotuba hiyo ndefu ya Mbowe ilpangwa kwa utangulizi, siku ya historia, maandamano halali, jeshi la wahalifu, mauaji ya kupangwa, kisasi cha Uchaguzi Mkuu, haki lazima itendeke na mauaji ya Arusha na mahitaji ya katiba mpya.
Askofu amshukia Makamba
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Arusha, Thomas Laizer amesema Katibu wa CCM, Yusuph Makamba ana uelewa finyu wa Biblia.
Akizungumza katika ibada ya kuwaaga watu wawili waliofariki dunia kwa kupigwa risasi na polisi Uwanja wa NMC jana, Askofu Laizer alisema tafsiri ya Makamba toka katika biblia ya kuwataka viongozi wa dini kuheshimu mamlaka ya viongozi waliopo madarakani, inapotosha.
"Miaka yote viongozi wa dini wamekuwa ni washauri wa Serikali hivyo Makamba kutumia Biblia kutaka kuwafumba midomo ni jambo lisilowekezana na ana uelewa finyu wa Biblia,"alisema Askofu Laizer.
Alisema maaskofu wamesikitishwa na kauli yake na pia kauli ya Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda kuwataka wavue majoho na kuingia katika siasa kwani huku ni kuwavunjia heshima.
Askofu Laizer alisema migogoro ya kisiasa Arusha, imeanza siku nyingi tangu katika mchakato wa kura za maoni ya ndani ya CCM katika nafasi za ubunge na udiwani.
"Hapa kuna migogoro, haijaanza leo, imeanzia CCM wamegawanyika na ikaendelea katika wakati wa kutangaza ushindi wa mbunge na sasa kupata Meya wa Jiji la Arusha,"alisema Laizer.
Askofu Laizer alisema anaamini mgogoro huo utamalizika katika kufutwa kwa matokeo ya meya na kurudiwa upya kwa uchaguzi huo na maaskofu hawana tatizo na mgombea aliyeshinda kihalali.
…Naibu meya aliyejiuzulu apongezwa
Askofu Laizer alimpongeza Naibu Meya, Michael Kivuyo kwa kujiuzulu kwake nafasi hiyo kutokana na utata katika uchaguzi uliomweka madarakani.
Hata hivyo, Askofu Laizer alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusema yaliyotokea Arusha hayatarejewa na pia akawapongeza, Mawaziri, Shamsi Vuai Nahodha, Bernard Membe na Steven Wassira kwa kutambua mgogoro wa Arusha na kushauri kumalizika haraka.
"Pia tunampongeza Mbunge wa Monduli Edward Lowassa aliposhauri mgogoro wa Arusha umalizwe kwa mazungumzo ili Arusha isiwe Ivory Coast,'' alisema Askofu Laizer.
Sheikh ataka marehemu
wakumbukwe kwa maombi
Sheikh Alawi Alawi akisoma dua aliwataka wakazi wa Arusha, kuwaombea marehemu Omar Ismail na Denis Shirima kwani wamefariki kishujaa.
Sheikh Alawi alisema marehemu hao, walifariki wakati wakipigania haki yao ya kikatiba na hivyo kuwaombea na kuwaaga ni jambo la busara sana.
Marehemu, Shirima anatarajiwa kuzikwa kesho wilayani Rombo ambapo, Ismail alitarajiwa kuzikwa jana katika mji mdogo wa Usa River.
Hadi jana mwili wa raia wa Kenya, Paulo Njuguna ulikuwa bado haujachukuliwa chumba cha maiti hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake