Tuesday, January 11, 2011

BRIGEDIA JENERALI RAMADHAN HAJI FAKI:“ Nilikuwa mwanzilishi wa wazo la mapinduzi "


Image
Brigedia Jenerali Ramadhan Haji Faki akiwa nyumbani kwake Zanzibar.

“Ilihitaji ujasiri wa hali ya juu kustahimili maumivu makali ya kidonda cha kisu na kugeuka 
kuwapa moyo wana mapinduzi waliolizingira boma la Sultani Jamshed Al-Said lililokuwa kwenye eneo la darajani, ili waibe silaha zote na kuhakikisha wameumaliza nguvu utawala wa Sultani,” anasimulia Brigedia Jenerali Faki. 


Akiwa ametangulia mbele na kuingia bomani pale huku wananchi na baadhi ya vijana wenzake 
wanaounda kundi machachari la Umoja wa Vijana 14 wa chama cha Afro Shiraz (ASP) wakimfuata nyuma. 

Akiwa mstari wa mbele alihisi kushtukiwa na mlinzi wa boma hilo la darajani kwa kuwa macho yao yaligongana na hivyo kuamua kuwajulisha wanamapinduzi alioandamana nao kwamba uwepo wao kwenye eneo lile ulikuwa umegunduliwa na askari wa ulinzi. 

Akiwa ameketi kwenye kiti kilichotengenezwa kwa mbao ngumu nyumbani kwake, Brigedia Jenerali Faki (81) anasema, alimuona askari huyo akitingisha tingisha kisu kikubwa alichokuwa 
nacho kama silaha na hivyo kuamua kumtia moyo mwenzake aliyeonekana kukihofia, kwa 
kumwambia kuwa hakikuwa na uwezo wa kuua bali kuchoma na kuacha alama tu. 

Kwa maelezo yake, lengo la kusema hivyo lilikuwa kumtia moyo mwenzake huyo pamoja na wananchi waliofuatana nao ili kuzuia wasibadili mawazo na kurudi nyuma, kwa kuwa 
walikuwa wamekwisha onekana na dhamira yao kujulikana. 

Wakati akizungumza na mwenzake huyo ambaye ni miongoni mwa vijana wanaounda kundi la watu 14 walioshiriki kupanga na kutekeleza mapinduzi hayo, ghafla alichomwa kisu kifuani na mlinzi huyo, jambo lililomkasirisha na kuamua kulipiza kisasi muda huo huo kwa kumchoma 
askari huyo kwa kisu na kufa papo hapo. 

“Nilipomchoma kisu nilijua nimemaliza kazi, sikugeuka nyuma kujua jina lake wala sikutaka kujua mengi kumhusu”, anaeleza Brigedia Jenerali Faki. “Sikuwa na muda wa kusubiri, 
niliwajulisha wenzangu kuwa amekwisha kufa nao wakaingia bomani na kuchukua silaha zote zilizokuwemo”. 

Wakati hilo likitendeka na kwa sababu alikuwa akivuja damu nyingi zilizoelekea kummaliza nguvu, aliamua kukimbilia hospitali ambapo alitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani 
siku hiyo hiyo. 

Vijana saba walivamia boma la Darajani, wenzao wasiopungua saba kutoka kwenye umoja huo wa vijana wa ASP walivamia boma la Ziwani na kufanikiwa kuchukua silaha zote, jambo 
lililowapa nguvu na matumaini mazito kuwa mapinduzi ya Unguja Zanzibar yalikuwa yamefanikiwa. 

“Nilikwenda kupumzika nyumbani kwa wazazi wangu baada ya matibabu huku nikiwa na mawasiliano yote ya kilichokuwa kikiendelea baba yangu hakuwa na taarifa zozote wala hakujua kuhusu mapinduzi hadi nilipomwambia kuwa Sultani hana lake tena Zanzibar... nashukuru hakunikaripia wala kunipongeza alikuwa kimya akitafakari tu ninachomueleza”. 

“Mwenyekiti wa kamati ya mapinduzi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wetu wa Vijana, Seif Bakari Omari alimtuma kijana mwingine wa kundi letu aitwaye John Okello kwenda 
redioni kutangaza habari ya kupinduliwa kwa utawala wa Sultani Jamshid ambaye muda mfupi baada ya mageuzi hayo alikimbilia Ulaya na kutokomea huko hadi leo hii,” anasena Brigedia Jenerali Faki . 

Anasema Okello aliweza kudhibiti redio ile ya Sultani kwa sababu alikuwa amesomea masuala ya habari na hivyo kufanikisha kwa asilimia kubwa kusambaza habari za mapinduzi hayo kwa wananchi. 

Faki anasimulia namna alivyofikia uamuzi wa kutoa wazo la mapinduzi na kusema wakati wakiwa kwenye eneo lao la kukutania la gulioni au sokoni, palitokea mabishano kati yao 
kuhusu uwezekano wa wao (watu weusi) kushinda uchaguzi na kushika madaraka ya nchi yao. 

Anasema, “bila kusita niliwahakikishia wenzangu kwamba ASP isingeshinda uchaguzi mkuu wowote hapa duniani na kwamba labda Mbinguni kwamba ushindi wa ASP wasingeweza kupata ushindi kwenye uchaguzi wowote visiwni humu kutokana na mfumo wa uchaguzi 
ulivyokuwa. 

“Mimi niliwaambia wenzangu kuwa ushindi wa ASP usingeweza kupatikana kamwe kwa njia ya kura na kwamba kama walitaka kuusubiri wangeupatia Mbinguni….walipouliza sasa itakuwaje nikawaambia tufanye mapinduzi na ndivyo ilivyokuwa”. 

Anaongeza kusema kuwa utaratibu wa uchaguzi wa kura ulikuwa sio sawa kwa sababu utawala wa sultani uliendekeza ubaguzi wa rangi ambao uliwagawa wazanzibari kwa rangi zao. 

“Mwarabu mmoja alihesabiwa kura tatu wakati Mzanzibari alihesabiwa kura moja sasa hata tungefanya vipi kura zetu zisingetosha kutupa ushindi kwa sababu hapakuwa na uwiano wa 
kimahesabu wakati mwarabu ana kura sita sisi tulikuwa tukihesabiwa kuwa tuna mbili,” amesema Faki. 

“Mambo haya yalituchosha ndio maana tukataka tujitawale wenyewe kwenye nchi yetu, hatukutaka mambo ya kisultani tena, tulipewa uhuru wetu na Waingereza Desemba 09, 1963 lakini tukaendelea kunyonywa na wafalme wa Kiarabu hatukuwa tayari kuvumilia ndio maana tukatekeleza mapinduzi haya,” anasisitiza. 

“Utamaduni wa ngoma za Wazanzibari ulichangia kufanikisha mapinduzi na hicho ndicho kilichotokea, Sultani alikuwa nyumbani kwake Forodhani wakati mapinduzi yanatokea na wengi wa askari wake walikuwa wakishangaa ngoma wakati sisi tunafanya vitu vyetu,” anaongeza kusema Faki. 

Kwa mujibu wa Faki, mkutano wao wa kwanza baada ya mapinduzi ulifanyikia katika nyumba 
moja iliyopo kwenye eneo lao la siku zote la gulioni na kwamba hali haikuwa shwari kwa siku hizo kutokana na vita vilivyotokea baina yao na walioumizwa na mapinduzi hayo (waarabu). 

Faki anasema katika harakati hizo hakutoka mikono mitupu bali alijichukulia mlango wa thamani kubwa kutoka kwenye boma lile la Sultani ambao ameuweka kwenye nyumba anamoishi sasa, upande unaotumiwa na wageni pamoja na wenyeji kwa kuingia na kutoka 
kuelekea nje kabisa ya eneo la nyumba yake. 

Anaeleza kuwa aliuchukia utawala wa masultani toka akiwa askari wa kawaida na hata kufikiria 
kukimbilia ughaibuni baada ya kustaafu kazi ya uaskari aliyoifanya kwa miaka 12 mfululizo na kulipwa kiinua mgongo cha shilingi 4,360 mwaka 1963. 

Hata hivyo, wazo la safari hiyo liliyeyuka ghafla baada ya kuingiwa na lile la kupindua nchi. 
“Nilikuwa koplo wakati huo nikiwa na namba 67 ya aliyekuwa mtu wa bara aitwaye Omari Misati aliyeacha kazi na kurudi Bara kwao nilipojiwa na wazo la mapinduzi sikwenda tena ulaya bali nilitumia fedha hizo kujengea nyumba yangu ya kwanza,” ameendelea kusema. 

Baada ya Rais Karume kuuliwa kwa risasi na Mwarabu aitwaye Humud, Rais aliyefuata, Aboud Jumbe alimteua Faki kuwa Waziri Kiongozi, cheo alichokishika kwa miezi sita tu na kujiuzulu kwa sababu ambazo hakupenda kuzizungumzia.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake