Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na wafuasi wengine wa chama hicho, wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu Ismail Omar juzi, ambaye familia yake inalalamikia kukiukwa kwa taratibu za Kiislamu za kuaga maiti. (Picha ya issamichuzi.blogspot.com).
FAMILIA ya marehemu Ismail Omari (25) aliyeuawa katika vurugu za kisiasa zilizotokea Januari 5 mwaka huu mkoani hapa, imedai kushinikizwa na Chadema kumpeleka marehemu wao katika uwanja wa NMC kuagwa kinyume na maamrisho ya dini yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, baba mzazi wa marehemu huyo Omar Juma,
alisema shinikizo lililowafanya kukubali kitendo hicho lilitolewa juzi usiku baada ya msemaji wa familia yake, Nyerere Kamili, kupokea simu kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Chadema; Diwani wa Elerai, John Bayo, kuwa iwapo hawatakubali kupeleka mwili wa ndugu yao kwenye uwanja huo, chama chake kitajitoa kushughulikia mazishi.
Alidai mbali na shinikizo hilo, pia juzi wakiwa chumba cha maiti, katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru, kuchukua mwili huo, walikuta mazingira yasiyo mazuri kwao kugomea kupeleka mwili huo wakihofia kudhuriwa na wafuasi wa Chadema, ambao walikuwa wamefurika eneo hilo wakitaka miili yote ipelekwe uwanjani kuagwa.
Alisema kutokana na sababu hizo, pia alilazimika kuwapigia simu viongozi hao wa Chadema na alikutana nao siku hiyo, wakakubaliana kuupeleka mwili huo uwanjani hapo, ili kupata msaada wa chama hicho wa mazishi kwa kuwa hawana uwezo wa kuendesha mazishi hayo.
“Sasa baada ya sisi kupokea simu hiyo, tulilazimika kuwapigia simu ili kupata msaada, maana vifo vimetokana na mkutano wao, sasa uwezo hatuna na hali ilivyokuwa pale, tungeweza kupigwa hata mawe na wafuasi wao kwa hiyo ilikuwa hivyo,” alisema Omar.
Pia alisema kutokana na shinikizo hilo, liliipa wakati mgumu familia yake baada ya Waislamu kuchukizwa na kitendo hicho hadi kufikia kunyimwa jeneza la kubebea maiti hali iliyowalazimu kuhangaika katika zaidi ya misikiti mitatu bila mafanikio.
Aliongeza kuwa baada ya hali hiyo, alikwenda kuchukua jeneza kwenye msikiti wa hospitali ya Mount Meru akikodi kwa Sh 5,000 ambayo hadi jana walikuwa wakidaiwa kutokana na kushindwa kulipa.
Kwa hali hiyo na kutambua kuukosea Uislamu na Waislamu kwa jumla, aliwaomba viongozi kuisamehe familia yake kwa kuwa haikuwa dhamira yao kufanya hivyo, bali kwa shinikizo la Chadema.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Baraza la Wazee wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Haruna Fundikira, alipoulizwa kuhusu suala hilo alikiri na kusema hata yeye aliungana na familia ya marehemu, kuwa suala la kupeleka maiti katika uwanja huo halikuwa sahihi kulingana na maamrisho ya dini.
Alisema walichokubaliana ni kupata japo picha ya marehemu Ismail ili ioneshwe uwanjani hapo, lakini maiti achukuliwe na kupelekwa kwa maziko Usa River, lakini alishangazwa na taarifa kuwa mwili huo ulipelekwa uwanjani hapo.
Alisema siku moja kabla ya maziko, alikwenda kwa familia ya marehemu kupanga mipango ya maziko hayo na walipokubaliana juu ya taratibu hizo, aliahidi kutoa sanda, lakini alilazimika kuahirisha kuitoa, baada ya kuona utaratibu tofauti na aliokubaliana na familia hiyo.
"Mimi jana sikwenda uwanjani hapo, nilikuwa na mgeni nyumbani, lakini nilichosikia ni kwamba walipeleka mwili huo uwanjani tofauti na nilivyokubaliana nao na sikutoa tena sanda, maana walikuwa na uamuzi wao kama familia,” alisema Fundikira.
Aliongeza kuwa, baada ya kuahirisha kutoa sanda, alipokea simu kutoka kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akisema ameshakubaliana na familia kuhusu taratibu zote za maziko na asihangaike kutoa sanda, kwani chama kitatoa.
Shehe wa Msikiti wa Bondeni, Shaaban Juma, alisema familia hiyo haina haja ya kuomba radhi, kwa kuwa alishirikiana nayo kwa hali na mali, lakini akashangazwa alipoambiwa na
mmoja wa wanafamilia, aondoke kwenye chumba cha maiti na angempigia simu baadaye, kwa kuwa suala hilo lilikuwa likiihusu familia pekee.
Alisema kamwe hawezi kuiomba radhi familia hiyo wala kutoa msamaha yeye, kwani familia imemkosea Mwenyezi Mungu na si Waislamu, kwa kukiuka misingi na taratibu za dini hiyo na iwapo iliona inazidiwa nguvu, ilipaswa kukabidhi jukumu hilo kwa viongozi wa kiislamu ili walisimamie.
“Mbali na Qur’an na Hadithi za Mtume kukataza, lakini kitendo cha kumpeleka marehemu wa
kiislamu uwanjani pale, ambao uligubikwa mapambio ni kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na ni moja ya sababu iliyosababisha yeye asihudhurie maziko hayo,” alisema Shehe Shaaban.
Juzi Chadema iliendesha ibada maalumu ya kuaga miili ya marehemu wawili waliopoteza maisha katika mapambano baina ya wafuasi wa Chadema na Polisi kutokana na kufanya maandamano yaliyozuiwa kwa kuhofia uvunjifu wa amani ambapo watu watatu walipoteza maisha.
Katika hatua nyingine mwili wa marehemu Denis Shirima, nao ulihamishwa kutoka sanduku ambalo lilionekana kuwa duni na kuingizwa katika sanduku la kifahari, ambalo lilinunuliwa na Chadema.
Awali marehemu alikuwa kwenye sanduku la kawaida la rangi nyeupe wakati mwili ukiwa hospitalini tayari kupelekwa kwenye uwanja wa NMC kuuagwa, lakini baadaye ukabadilishiwa kwenye sanduku hilo jipya na la zamani haikujulikana lilikopelekwa.
Chanzo:HabariLeo |
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake