Thursday, January 6, 2011

Familia mbaroni kwa kujifanya maofisa wa uhamiaji

IDARA ya uhamiaji mkoani Kigoma imewakamata watu watano wa familia moja wakazi wa Ujiji mkoani hapa, wakituhumiwa kujifanya maofisa wa uhamiaji na kutengeneza nyaraka 
zinazowaruhusu watu kuingia na kutoka nchini.
 

Kaimu Kamanda wa Uhamiaji mkoani hapa, Adirati Millinga alisema jana kwamba idara hiyo imemkamata Jumanne Baya, akiwa na mihuri na nyaraka alizotengeneza kwa ajili ya kusaidia kazi hiyo. 

Millinga alisema Baya ambaye ni mtuhumiwa namba moja wa sakata hilo, alikutwa na mihuri miwili inayoruhusu wasafiri kuingia na kutoka nchini na fomu ambazo msafiri anapaswa kujaza apate ruhusa ya kutoka nchini. 

Wengine waliokamatwa ni pamoja na mke wa mtuhumiwa huyo, Pili Shahibu, mama mkwe wake, Mariam Ruhasha na watoto wake wawili, Shahibu Jumanne na Ahmed Ponda. 

Awali Kamanda Millinga alisema maofisa wa idara hiyo walimkamata nahodha wa boti moja katika mpaka wa Tanzania na Burundi eneo la Kagunga, akiwa na hati inayoonesha kuwa aliingia nchini akiomba kugongewa muhuri wa kumruhusu. 

Kamanda Millinga alisema baada ya kuikagua hati hiyo, waligundua haikuwa halali na baada ya kumkamata na kumhoji kwa muda, nahodha huyo alimtaja Baya kuwa ndiye aliyetengeneza hati hiyo na kuigonga mihuri. 

Baada ya kumkamata nahodha huyo, jitihada za kumtafuta Baya zilianza na inadaiwa alipata habari za kutafutwa kwake na kukimbia lakini maofisa wa idara hiyo walimkamata katika mpaka wa Tanzania na Burundi katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo. 

Hiyo ni mara ya pili kwa mtuhumiwa huyo kukamatwa kwa tuhuma hizo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 na alifikishwa mahakamani ambako alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 20,000 ambayo aliilipa na kuachiwa huru. 

Katika kesi hiyo, alikuwa akidaiwa kuingiza nchini maiti ya mtu mmoja aitwaye Rehani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. 

Akizungumzia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Ofisa Upelelezi Mfawidhi wa idara hiyo mkoani hapa, Bulugu Edward alidai mtuhumiwa amerudia kosa hilo kunatokana na adhabu dhaifu inayotolewa ambayo kifungo cha juu ni mwaka mmoja au faini ya Sh 100,000 ambazo watuhumiwa wengi wanao uwezo wa kulipa.


                                                                                             CHANZO:HABARI LEO



No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake