Friday, January 14, 2011
Makamba amjibu Askofu Laizer.
KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, amesema kuwa na uelewa finyu wa biblia si jambo la ajabu kwake kwa sababu yeye siyo askofu.
Makamba aliliambia Mwananchi jana kwa simu, kuwa licha ya uelewa finyu wa biblia, lakini amekuwa akitoa vifungu hivyo kwenye biblia.
Makamba alisema hayo kufuatia, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Thomas Laizer kusema Makamba ana uelewa finyu wa biblia.
Laizer alisema hayo juzi mjini Arusha wakati wa kuwaaga watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano na Chadema yaliyofanyika Januari 5 mwaka huu.
“ Ni kweli ninauelewa finyu wa biblia kwa sababu mimi siyo askofu, hata Qurani naweza kuwa siifahamu vizuri kwa sababu mimi siyo Sheikh, ndiyo maana kila ninachozungumza kuhusu dini hizo nakariri vifungu kutoka katika vitabu hivyo,” alisema. Makamba alisema alimweleza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutoandamana kwa sababu serikali ilipiga marufuku maandamano hayo, wao wakapuuza.
Alimtaka Laizer kutoa tafsiri ya kitabu cha Warumi 13 sehemu ya kwanza hadi ya saba, inayosema kuwa kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.
Alisema kwa hiyo anayepinga mamlaka inayotawala anapinga chombo kilichowekwa na Mungu na watu wanaoasi hujiletea hukumu.
“ Kwa maana watawala hawatishi watu wanaotenda mema bali wale wanaotenda maovu, kama hupendi kuishi kwa kumwogopa mwenye mamlaka basi tenda mema naye atakusifu,” alisema.
“ Laizer anieleze ufinyu wangu katika uelewa wa biblia upo wapi ikilinganisha na tukio lililotokea mkoani Arusha,” alisema.
Source: Mwananchi.

No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake