UPANDE wa mashitaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Gray Mgonja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona umemaliza kutoa ushahidi kwa upande wao.
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Frederick Manyanda alidai wamemaliza ushahidi wao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana kuwa baada ya kumaliza maswali kwa shahidi wao wa mwisho, Godwin Nyelo.
Alidai kuwa ushahidi wote uliotolewa kwa upande wao ni wa mashahidi 13 na vielelezo 28 hivyo wanaiachia Mahakama kufanya uamuzi wake.
Hata hivyo, mahakama hiyo inayosikiliza kesi hiyo mbele ya Mahakimu Wakazi, Saul Kinemela, Sam Rumanyika na John Utamwa, ilitamka kuwa mwenendo mzima wa kesi hiyo mpaka kesi hiyo ilipofikia, utaandaliwa.
Baada ya kukamilika kwa mwenendo huo, mawakili wa pande zote mbili watagaiwa nakala zake ili wajiandae kuwasilisha hoja zao za kisheria Februari 18 mwaka huu kama sheria inavyowataka kufanya.
Katika hoja hizo upande wa mashitaka unatarajiwa kuishawishi Mahakama ili washitakiwa wawe na kesi ya kujibu na hatua itakayofuata iwe kuanza kujitetea.
Hata hivyo upande wa utetezi, unatarajiwa kutoa hoja za kujaribu kuishawishi Mahakama kuwa wateja wao hawana hatia ili waachiwe huru.
Katika kesi hiyo, Mramba, Yona na Mgonja wanashitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi ya umma yaliyoisababishia Serikali hasara ya mabilioni.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake