ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 23, 2011

Asilimia 86 ya Watanzania hawajapata umeme

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
Raymond Kaminyoge
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema ni asilimia 14 tu ya Watanzania wanaopata umeme huku wengi wa asilimia 86 wakiona kwa mbali nishati hiyo.
Lakini pia pamoja na uchache wa Watanzania wanaopata nishati hiyo, bado huduma yake haina uhakika kwao.

Ngeleja alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau wa uzalishaji umeme wa Afrika Mashariki (EAPP) na wafadhili.

Alisema changamoto inayoikabili serikali kwa sasa ni upungufu wa nishati hiyo unaotokana na kupungua vya vina vya maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme.

Waziri Ngeleja alisema hadi sasa kuna mahitaji ya megawati 230 hali inayosababisha kuwepo kwa mgao wa umeme kwenye maeneo mengi.

“ Tunajitahidi kutafuta njia mbalimbali zitakazosaidia kukabili upungufu uliopo,”alisema Ngeleja.

Meneja Uzalishaji wa Tanesco, Stephen Mabada, alisema ili kukabiliana na upungufu wa nishati ya umeme, shirika hilo linafanya kila liwezekanalo kuongeza vyanzo vya uzalishaji.
Alisema takwimu zinaonyesha kwamba hadi mwaka jana mahitaji ya umeme yalikuwa megawati 833 hapa nchini, lakini mwaka huu yameongezeka na kuwa 937.

Alisema katika kipindi cha miaka 20 ijayo, mahitaji ya umeme hapa nchini yatafika zaidi ya megawati 5000.
“ Tunahitaji kufanya juhudi za kubaini vyanzo mbalimbali ili viweze kuchangia nishati hiyo kwenye gridi ya taifa,” aliwaeleza wadau na wafadhili.
Alisema mipango ya serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2025, asilimia 75 ya Watanzania watakuwa wameunganishwa na umeme katika gridi ya taifa.
Kwa mujibu wa meneja huyo, mwaka jana Tanesco ilijiunga uanachama wa wazalishaji wa umeme wa Afrika Mashariki (EAPP).

CHANZO:MWANANCHI

No comments: