ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 25, 2011

Bei ya sukari huenda ikashuka

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyril Chami
Raymond Kaminyoge na Happy Kiula

UHABA wa sukari unaiumiza kichwa Serikali ambayo sasa imeamua kufuta ushuru wa forodha wa tani 37,500 za bidhaa hiyo itakayoingizwa nchini kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ili kukabiliana na tatizo hilo.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa hatua hiyo pia, imelenga kupunguza bei ya sukari inayoendelea kupaa kwa kasi kila kukicha.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyril Chami alisema jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuwa, tani nyingine 12,500 za sukari, zitaagizwa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambako hakuna ushuru wa forodha. 


Kwa mujibu wa Chami, hivi karibuni bei ya sukari imekuwa ikipanda kwa kasi katika baadhi ya maeneo hadi kufikia Sh 2,200 kwa kilo moja na kusababisha baadhi ya wananchi washindwe kumudu bei hiyo.

Hata hivyo, alisema baada ya kuagiza sukari hiyo, itawafikia watu na bei itashuka hadi kufikia Sh 1,700 kwa kilo moja.“Kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua kuagiza tani 50,000 za sukari kutoka nje ili kufidia upungufu uliopo, pia kwa kuwa sukari imepanda katika soko la dunia, tumeamua kufuta ushuru wa forodha ili iweze kuuzwa kwa hapa nchini kwa bei ambayo wananchi watamudu,” alisema Chami.Alisema kiasi hicho cha sukari kitaziba pengo la mahitaji katika kipindi cha  Mei na Juni, 2011.

Takwimu kutoka katika Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), zinaonyesha kuwa, mahitaji ya sukari hapa nchini kwa mwaka ni tani 480,000 wakati zinazozalishwa ni tani 300,000 hivyo kuwepo pengo la tani 180,000 la bidhaa hiyo.
Chami alisema Serikali imeagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), iweke utaratibu wa kutoa kipaumbele kwa meli zinakazokuwa zinabeba sukari ili iweze kuwafikia walaji haraka.Aidha, Waziri Chami aliiagiza Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), kuchukua hatua za haraka kukamilisha taratibu za kutotoza ushuru wa forodha kwa sukari hiyo katika kipindi hiki cha kukabiliana na tatizo hilo.

Waziri Chami alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikutana na wadau wote wa bidhaa ya sukari nchini ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.Alisema katika kikao hicho, ilibainika kuwa bei ya sukari katika soko la dunia imepanda kwa sababu ya kufungwa kwa viwanda kutokana na kukosekana kwa malighafi.“Kwa hapa nchini viwanda hufungwa kati ya Februari na Mei kila mwaka kwa kuwa huo sio msimu wa miwa, wenye viwanda hutumia nafasi hiyo kuvifanyia matengenezo viwanda vyao,” alisema.

Kauli ya Bodi ya Sukari Jana Mchana Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Mathew Kombe, aliliambia gazeti hili kuwa "tunakula zaidi kuliko tunachozalisha."Alisema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa sukari, kuna wawekezaji ambao watajenga kiwanda katika wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani kwa ajili ya kuzalisha tani 100,000 za sukari kwa mwaka.“Wako katika hatua za mwanzo za kuagiza mitambo.

Wakianza kufanya kazi, kiasi hicho cha sukari (tani 100,000) kitasaidia kupunguza mahitaji ya bidhaa hiyo,” alisema.Alitoa wito kwa wafanyabiashara wanaohitaji kuwekeza kwenye viwanda vya sukari kufanya hivyo ili hatimaye upungufu wa bidhaa hiyo uwe historia.
Historia ya uhaba wa Sukari nchini
Historia ya uhaba wa sukari nchini inaturejesha mwaka 2001 wakati Serikali ya awamu ya tatu ikiongozwa na Benjamin Mkapa ilipopata pigo baada ya waziri wake wa Viwanda na Biashara kulazimika kujiuzulu kutoka na kashfa ya sukari.

Waziri huyo, Iddi Simba alijiuzulu Novemba 2001 kufuatia kashfa ya utoaji wa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi. Aliyekuwa naibu wake, Antony Diallo alinusurika katika sakata hilo baada ya kutopatikana na ‘hatia’.

Katika kujiuzulu kwake, Simba alipata shinikizo kutoka ndani ya Bunge, kufuatia ‘bomu’ lililolipuliwa na aliyekuwa Mbunge wa Kwela mkoani Rukwa wakati huo, Chrisant Mzindakaya aliyedai kuwa utoaji wa vibali vya kuingiza sukari ulikuwa umejaa utata na kwamba haukuwa na maslahi ya taifa.Kufuatia hoja ya Mzindakaya, Kamati Teule ya Bunge iliundwa na saa chache kabla ya ripoti ya Kamati hiyo kuanza kujadiliwa bungeni, Simba akajiuzulu wadhifa wake.

Uhaba wa Machi 2010
Mwezi Machi mwaka jana Serikali pia aliagiza kutoka nje ya nchi tani 50,000 za sukari kutokana na kuwapo upungufu katika mzunguko wa soko, hali iliyosababisha kupanda bei ghafla kwa bidhaa hiyo.

Akiwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Chami alinukuliwa akisema kuwa Serikali ilikuwa akiwasiliana na baadhi ya kampuni ili ziweze kuagiza sukari, kama njia mojawapo ya kukabiliana na uhaba huo ambao alisema ulikuwa umeukumba ukanda wa Afrika ya Mashariki.Wakati serikali ikichukua hatua hizo, bei ya sukari ilikuwa imepanda kutoka Sh1,400 hadi Sh1,900.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: