ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 25, 2011

Dowans yaibua mapya TANESCO

Na Rabia Bakari

KAMPUNI ya Mawakili ya Rex iliyoiwakilisha TANESCO katika kesi dhidi ya Dowans imetajwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa
ilihusika katika kesi hiyo ikiwa na mgongano wa kimaslahi.

Hayo yalifahamika jana baada ya kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Januari Makamba ilipotembelea mitambo ya Dowans, na katika maelezo ya mmoja wa wanahisa na Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans Tanzania Limited, Bw. Stanley Munai ilibainika kuwa kampuni ya REX ilikuwa inatoa msaada wa kisheria kwa pande mbili katika kesi hiyo.


Maelezo hayo yalijitokezo wakati Bw. Munai akijibu maswali kuhusu madeni yanayikali kampuni hiyo ambayo imekuwa gumzo la muda mrefu hapa nchini.

Bw. Munai alisema kuhusu madeni hawana cha kuficha, kwamba wanadaiwa dola milioni mbili na benki ya Barclays, na kabla ya deni hilo na benki hiyo, walikuwa wamechukua mkopo katika benki ya Stanbic wa dola milioni 20 ambako walihamishia deni hilo Barclays kutokana na makato ya Stanbic kuwa makubwa.

Alisema wakati wa kuchukua mkopo Stanbic, benki hiyo iliwaonesha orodha ya kampuni za mawakili na kuwataka kuchagua mojawapo kwa ajili ya kuwakagua na kuwathibitisha ili waweze kupata mkopo ambapo walichagua Kampuni ya Mawakili ya REX, ambayo iliwaandikia maoni 'mazuri' na kuwathitisha wapate mkopo huo.

Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge wahoji, iweje mawakili hao wa REX wawathibitishe Dowans kupata mkopo, wakati huo huo ndio walikuwa wawakilishi wa wapinzani wao TANESCO katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa ICC.

Akijibu hilo, Bw. Munai alidai kuwa hofu hiyo hata wao aliiona mapema na kwa ushauri waliwaandikia barua TANESCO kuwajulisha kuwa mawakili hao wana mgongano wa kimaslahi na kuwa haitakuwa vizuri kuwawakilisha TANESCO, lakini hawakuji na matokeo yake mawakili waliendelea kusimamia kesi hiyo, huku akidai kuwa hawakujua kwa nini TANESCO waliamua kukaa kimya.

Kauli hiyo iliwafanya wabunge wengi kutingisha kishwa na kumwambia mkurugenzi huyo kuwa wameshaelewa, na hilo si la kwake yeye.

Akiendelea kubanwa na maswali ya papo hapo kwa hapo ya wabunge hao, ambapo kwa kiasi kikubwa Bw. Makamba ndio alikuwa akiuliza maswali mfululizo, pia alitaka kufahamu sababu kubwa iliyofanya mmiliki wa Dowans, Sulaiman Mohamed Yahya Al Adawi kuja nchini na kutaka kuzungumza na TANESCO.

"Alikuja nchini (Al Adawi) baada ya kusikia malalamiko ya Watanzania kuwa fedha tunazodai ni nyingi, na lengo likiwa ni kuzungumza na TANESCO ili kukubaliana gharama za kupunguza na hatimaye kama inawezekana tuendelee kutoa huduma, lakini hata hivyo TNAESCO hawajajibu barua hiyo ya kutaka tuonane nao na wala hawataki kukaa pamoja nasi," aliongeza Bw. Munai.

Alisema kuwa Bw. Al Adawi alikuwa tayari kupata hasara na kusamehe mambo mengi, lakini TANESCO hawaoneshi ushirikiano katika hilo.

Bw. Mkamba alitaka kujua hasara gani ambayo Bw. Al Adawi yupo tayari
kuipata na kuwasaidia Watanzania, na Bw. Munai alijibu kuwa "Yeye
amewekeza mitambo yake ipo hapa, na inawashwa ili isioze, kuna umeme tunatumia, bima ya tahadhari inalipwa, tunalipa watu wanaokuja kufanya kazi, ni gharama kubwa tunatumia, lakini yupo tayari kupata hasara kwa hilo."

Baada ya wanakamati kuondoka waandishi walimganda Bw. Munai kutaka kujua mambo kadhaa ikiwemo uhalali wa deni na gharama halisi wanazodai kwa TANESCO, ambapo alijibu kuwa ni nyingi mno, kwani hata hizo bilioni 94 zinazosemwa ni nyuma kabla ya hukumu kutoka, ambapo kwa makubaliano TANESCO walitakiwa kuwalipa dola 11,800 kila siku na fedha hizo zilianza kuhesabika kuanzia Juni 14, mwaka jana hadi leo.

Katika hatua nyingine, Dowans imeitupia lawama TANESCO kuwa ndio chanzo cha matatizo baada ya kutotaka kujibu barua mbalimbali walizoandikiwa wala kutotaka kukaa mezani kwa ajili ya kushauriana kuwapa 'unafuu' Watanzania.

Awali, baada ya kamati hiyo kuingia katika eneo la mitambo ya Dowans, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa TANESCO, Bw. Moses Mwandenga alianza kutoa maelezo ya mitambo hiyo jinsi inavyowashwa na kufanya kazi, ambapo alielezea uwezo wa kuzalisha umeme na jinsi unavyoingia katika gridi ya taifa.

Mtaalamu huyo alieleza kuwa tangu mkataba wao na TANESCO uvunjwe, ili
kudhibiti uharibifu wa vifaa mitambo hiyo huwashwa na kila baada ya wiki mbili ili kuhakikisha inafanya kazi lakini bila kuzalisha umeme.

Baadhi ya wanakamati walitaka kujua hali ya mitambo wakati inaingizwa nchini ambapo, Bw. Munai alijibu kuwa ilikuwa mipya, na kuonesha kuchukizwa na kauli za baadhi ya watu wanaodai kuwa mitambo hiyo ni chakavu.

Alisema mitambo yote iliingia nchini ikiwa mipya isipokuwa mmoja, uliokuwa umetumika kwa saa 5,000, muda ambao alidai ni mfupi kwa kifaa kipya.

Baada ya maswali ya kitaalamu ndipo, Bw. Makamba alimpotaka mkurugenzi huyo kueleza ni kwanini hawataki kuondoa mitambo yao ilihali haifanyi kazi yoyote na kung'ang'ania kubaki nchini.

"Hatujang'ang'ania, isipokuwa baada ya TANESCO kuvunja mtakaba, tulitaka kuondoa mitambo, wao wakatuzuia kuwa mpaka kesi iliyopo ICC itakapomalizika ndipo tunaweza kuondoka," alisema Bw. Munai.

Aliendelea kujitetea kuwa kesi hiyo imeisha muda si mrefu, lakini ni mapema mno kwao kueleza hatua za kuondoka kwa sasa.

Baada ya ziara, waandishi walimgeukia Bw. Makamba kutaka maoni yake, ambapo alikiri kuona matatizo mengi, na kudai kuwa hawezi kuongea hapo isipokuwa leo ambapo kamati itakutana na wadau wote wanaozalisha umeme.

"Nadhani ndugu waandishi na nyie mmejionea kila kitu, sasa mimi sina cha kusema kwa leo, isipokuwa kesho tutazungumza baada ya kukutana na wadu wote wakiwemo Songas, Dowans, TANESCO na wengineo," alijibu.


CHANZO:MAJIRA

No comments: