ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 22, 2011

Mitambo ya Dowans yawashwa - Mwananchi.


MITAMBO ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans ambayo mjadala wake bado unapasua vichwa vya Watanzania imewashwa, Mwananchi limebaini.


Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa mitambo hiyo imewashwa kwa mkataba mpya na kampuni ya Songas kwa ajili ya kufua umeme utakaosaidia kupunguza tatizo la mgawo unaoendelea sasa nchi nzima.

Kuwashwa kwa mitambo hiyo kumekuja siku chache tangu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba apendekeze kuwashwa kwa mitambo hiyo kama njia ya kuliokoa taifa na mgao wa umeme unaoendelea kote nchini.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika eneo inakohifadhiwa mitambo hiyo, Ubungo jijini Dar es Salaam ulibaini kuwa baadhi ya mitambo ya Dowans ilikuwa ikiendelea kufanya kazi.




Mfanyakazi aliyekutwa katika eneo la mitambo hiyo alimweleza mwandishi kuwa mitambo hiyo imewashwa tangu juzi lengo likiwa kukabiliana na mgawo wa umeme.

“Kwa sasa tatizo la mgawo litapungua kwani mtambo mkubwa ulioko nyuma ya Jengo la Makao Makuu ya Shirika letu umewashwa, bado huu hapa mdogo,” alisema mfanyakazi huyo huku akionyesha mtambo huo mdogo ambao ulikuwa haujawashwa.

Aidha, mfanyakazi huyo alimtaka mwandishi wa habari kuzunguka nyuma ya majengo na kwamba angejionea mwenyewe juu ya kweli wa kauli hiyo.

“Ndugu yangu si unataka kuona mitambo hiyo, hapa huwezi kuiona zunguka nyuma ya ile mtambo ndio utanona vizuri,”alisisitiza.

Katika eneo la karibu ya mitambo Mwandishi alishuhudia mitambo hiyo ikifanya kazi na alipouliza majirani juu ya lini imewashwa alijibiwa kuwa mara kwa mara mitambo huyo huwashwa, lakini kwa sasa imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu zaidi.

“Unajua hii mitambo bwana haileweki, mara kwa mara huwa inawashwa, lakini kwa leo naona imechukua muda mrefu zaidi, sina uhakika kama ndiyo imewashwa moja kwa moja,” alisema mkazi huyo anaishi jirani na eneo ilikohifadhiwa mitambo ya umeme.

Taarifa nyingine kutoka vyanzo huru vya habari zilieleza kuwa mitambo hiyo ya Dowans iliwashwa juzi usiku kwa makubaliano baina ya Songas na Dowans, baada ya mitambo ya Songas kukorofisha hivyo kuhitaji nyongeza ya megawati 37 katika gridi ya taifa.

Kauli ya Tanesco

Meneja mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud alikanusha shirika hilo kuingia mkataba na Dowans ili kuwasha mitambo hiyo.

“Sina taarifa kuwa mitambo ya Dowans imewashwa... ni kweli ipo hapa nyuma ya ofisi zetu, lakini hatujawa na mazungumzo na kampuni hiyo kuhusiana na kuwashwa kwa mitambo hiyo,” alisema.

Alibainisha kuwa iwapo kutakuwa na jambo lolote linalohusiana na mkataba baina ya Tanesco na Dowans, shirika hilo litatoa taarifa kwa umma ili kila mmoja aelewe kinachoendelea.

Ujio wa Al Adawi

Mitambo hiyo imewashwa siku moja baada ya Suleiman Mohammed Yahya Al Adawi, anayedai kuwa ndiye mmiliki wa kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, kuwasili nchini na kuzungumzia sakata la fidia ambayo kampuni yake hiyo inaidai Tanesco kutokana na kukatisha mkataba wake kinyume na sheria.

Hata hivyo, ujio huo wa Al Adawi, ambaye ni raia wa Oman, umewasha upya moto wa sakata la Dowans, baada ya wasomi na wanasiasa kuuita usanii waliodai kuwa umefanywa na wajanja wachache, kuwacheza shere Watanzania.

Juzi Al Adawi aliingia nchini na kukutana na wahariri wa vyombo vya habari akieleza kuwa amekuja kuondoa sintofahamu iliyopo kuhusu suala la Dowans na kuangalia uwezekano wa kutafuta suluhisho kuhusu suala hilo.

"Nimekuja kwa mambo mawili; moja ni kuondoa sintofahamu iliyopo hivi sasa kuhusu kampuni ya Dowans na kuangalia kama kuna uwezekano wa kuwapo suluhisho la kile kilichopo hivi sasa kuhusu Dowans," alisema Al Adawi ambaye ni Mwanajeshi aliyestaafu katika ngazi ya Brigedia Jenerali.

Huku akigoma kupigwa picha, Al Adawi alisema yuko tayari kuzungumza na Tanesco kuhusu fidia ya Sh94 bilioni (hakutaja kiasi), baada ya kuvunjwa kwa mkataba baina ya kampuni yake hiyo na Tanesco.

Maoni kuhusu Al Adawi

Lakini ujio huo umeibua hasira za wasomi na wanasiasa ambao kwa nyakati tofauti jana waliuita usanii huku, mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, akiitaka Serikali imkamate Al Adawi na kumhoji.

“Nilitarajia AlAdawi angekiri hadharani kama wamedanganywa na kampuni ya Richmond, lakini hakufanya hivyo. Sasa naomba kutoa rai kwa vyombo vya dola kwamba vimkamate, vimpige picha na kumhoji kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo kutokana na maelezo tata yaliyotolewa mpaka sasa kuhusiana na kampuni ya Dowans,”alisema Mnyika na kufafanua:

Kauli ya Mnyika iliungwa mkono na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambaye ameeleza kutilia shaka umiliki huo akihoji "muda wote, Al Adawi alikuwa wapi kama huu sio mwendelezo wa utapeli?"

"Kama kweli ni mmiliki halali siku zote alikuwa wapi, na kwa nini ajitokeze baada ya hukumu ya fidia ya malipo ambayo Watanzania wanaipinga,'' aliendelea kuhoji mbunge huyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Ni bora utembee na viraka kuliko mtu kukuvunjia heshima. Huu ni mchezo wa kundi la watu wachache wanaoichezea nchi na kuidhalilisha, huu ni utapeli mtupu,'' alisema Lembeli.

Mwanasheria maarufu nchini Profesa Abdallah Safari amemtaka Al Adawi kutoa nyaraka halisi zinazomtambulisha kuwa mmiliki wa kampuni ya Dowans vinginevyo anafanya ‘usanii’.

"Si suala la kuita vyombo vya habari na kujitangaza yeye ni mmiliki. Atoe nyaraka halisi zinazomthibitisha, kwani anaweza kuwa ni mwarabu wa Kariakoo,'' alisema Profesa Safari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Bashiru Ally alisema kinachofanyika ni mchezo wa kuigiza wenye nia ya kutuchanganya Watanzania.

Alisema jambo la msingi kuhusu utata wa kampuni hiyo na Tanesco ni kwa wote waliohusika kuliingiza taifa kwenye mkataba huo feki kujulikana na kuchukuliwa hatua.

“Kulipa au kutolipa deni hilo la Sh94 bilioni siyo hoja kwa sasa, hoja ni nani wamefikisha taifa hapo tulipo, ni pale tu Serikali kuanzia ngazi ya waziri na kushuka chini itakapotuletea msururu wa wataalamu waliosababisha taifa kuingia kwenye mkataba huo feki ndipo suala la Dowans litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

Habari hii imeandaliwa na Elias Msuya, Sadick Mtulya na Geofrey Nyang'oro

Source: mwananchi

No comments: