ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 22, 2011

Phiri apewa rungu kuua TP Mazembe

Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, umempa kocha wake mkuu, Patrick Phiri, majukumu ya kupendekeza majina mawili ya makocha anaowahitaji ili kuimarisha benchi lake la ufundi wakati klabu hiyo ya Msimbazi ikijiandaa na mtihani mkubwa dhidi ya mabingwa watetezi mara mbili wa Afrika, TP Mazembe kwenye Ligi ya Klabu Bingwa mwezi ujao.





Kwa mujibu wa habari zilizopatikana juzi katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba na Phiri, walifikia maamuzi hayo baada ya kumueleza kocha huyo kwamba wana malengo ya kuboresha benchi la ufundi ili waweze kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na mechi za ligi ya Bara zilizobakia.
Chanzo hicho kilisema kuwa Phiri alipewa jana na leo ili kupeleka majina ya makocha anaowahitaji lakini endapo atashindwa uongozi utakuwa tayari kumsaidia.
"Katika kikao cha jana (juzi) tuliamua mambo mbalimbali na hayo yote yalitokana na kumsikiliza Phiri mipango yake juu ya mechi zinazotukabili mbele yetu, kocha aliomba apewe siku mbili awasiliane na makocha anaowafahamu na alielezwa kwamba akishindwa, uongozi ufanye mawasiliano na makocha inaowafahamu ili waje haraka nchini kuanza kuinoa Simba," alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ya Simba.
Aliongeza kuwa kikao cha kamati ya utendaji kitakachofanyika kesho pia kitaamua kama wawakilishi hao wa bara waende Kitwe nchini Zambia kuweka kambi kujiandaa na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa ya Afrika au wabaki hapa hapa nchini wakifanya mazoezi maalumu.
"Kulikuwa na mawazo tofauti juu ya kuipeleka timu Zambia, kikao cha Jumatano ndio kitatoa maamuzi ya mwisho," aliongeza kiongozi huyo.
Wakati huo huo, habari nyingine kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo zinasema kwamba wameanza mazungumzo na kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda, Cranes, Moses Basena, ili aweze kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo.
Chanzo hicho kilisema kuwa endapo mipango ya kumpata Basena itashindikana, makocha wengine kwa ajili ya makipa na saikolojia kutoka Oman watakuja na mawasiliano nao yanaendelea vizuri.
Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu' hakupatikana kuelekeza lolote kuhusiana na mipango hiyo wakati Afisa Habari, Clifford Ndimbo, hakuwa tayari kusema yaliyopangwa na viongozi wake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: