ASKARI Polisi wa Kituo cha Mahembe Kigoma Vijijini, Oscar Maliki ametiwa mbaroni akituhumiwa kumuua kwa kumpiga risasi mtuhumiwa aliyekuwa akitafutwa kwa tuhuma za shambulio la kudhuru mwili.
Maliki mwenye cheo cha Konstebo, anatuhumiwa kumpiga risasi Barenga Saidi (28) mkulima na mkazi wa Mahembe katika tukio lililotokea jana asubuhi ambako mtuhumiwa anadai alitumia bunduki aina ya SMG.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, George Mayunga alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa Maliki anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kusubiri hatua za kumfikisha mahakamani kujibu mashitaka yake.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, Kamanda Mayunga alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo baada ya Said awali kumtishia kumkata kwa panga mara tatu na mara ya mwisho alikamata bunduki kwa nia ya kumnyang’anga askari huyo.
Hata hivyo, maelezo hayo yalipingwa na watu waliokuwepo eneo la tukio na kudai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa akijua analolifanya na hakukutokea purukushani yoyote ya kunyang’anyana bunduki.
Kutokana na mauaji hayo, wanakijiji walivamia Kituo cha Polisi Mahembe kwa nia ya kukichoma moto, lakini viongozi wa kijiji, diwani na Ofisa Tarafa walifika na kutuliza munkari wa wananchi wasichukue hatua zaidi.
Ilibidi Kamanda Mayunga kwenda eneo la tukio na baadaye kufanya mkutano wa hadhara na wananchi kijijini hapo mkutano ambao unaelezwa kuwa umesaidia kupunguza hasira za wananchi kwa jeshi hilo.
Wakisimulia mkasa wa tukio hilo, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walidai mtuhumiwa alitenda kosa hilo akiwa amedhamiria kutokana na maneno aliyokuwa akitoa kwa Said kabla hajachukua hatua hiyo.
Akielezea chanzo cha tukio hilo, Dunia Hamadi anayeishi Kitongoji cha Nderembe A yalipotokea mauaji hayo, alidai Said aliuawa baada ya kupigwa risasi ya kifuani iliyotokea kwenye moyo na kufa hapo hapo.
Alidai awali polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa wakimtafuta kutokana na kufunguliwa kesi Februari 21, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Mahembe akituhumiwa kumpiga mama yake mdogo baada ya kutokea ugomvi wa kifamilia nyumbani kwao wakigombea mashamba.
Inadaiwa ugomvi huo ulitokana na wake wawili wa Mzee Moshi Mashaka kurushiana maneno ambapo mmoja wao, mke mkubwa ni mama wa marehemu.
Katika mabishano hayo, Said inadaiwa hakuridhika na jinsi mama yake mdogo alivyokuwa akitoa maneno kwa mama yake mzazi na ndipo akampiga.
Baada ya tukio hilo na kupata taarifa za kuripotiwa polisi, Said alikimbia nyumbani hapo hadi jana asubuhi wakati mlalamikaji Tabu Mussa alipomuona nyumbani na kutoa taarifa polisi waliofika kumkamata.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahembe, Miradji Shaban alisema askari huyo anayetuhumiwa kwa mauaji alifika nyumbani kwa Said akiwa ameongozana na askari mwenzake na mwanamgambo mmoja.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni ambako ulitarajiwa kufanyiwa uchunguzi jana mchana.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment