ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 25, 2011

Polisi sasa waelewe maandamano ya amani yanawezekana

Jana viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walifanya maandamano jijini Mwanza ambayo yalianza na kumaliza kwa amani. Hakuna taarifa yoyote ya uvunjifu wa amani iliyoambatana na maandamano hayo.
Pia itakumbukwa kwamba Chama cha Wananchi (CUF) nacho kilifanya maandamano yao jijini Dar es Salaam Februari 8, mwaka huu ambayo nayo yalianza na kumalizika kwa amani kama haya ya Chadema ya jana.
Maandamano haya kama yale yaliyokuwa yameitishwa na viongozi na wafuasi wa Chadema mkoani Arusha Januari 5, mwaka huu, hayana tofauti yoyote; washiriki wakuu ni viongozi wa vyama vya siasa wanaojulikana na wafuasi wao, aghalabu ni raia wa maeneo yanakofanyika maandamano.

Ni ukweli pia kwamba kuandamana ni moja ya haki za kikatiba za raia, kwa maana hiyo pale raia wanapojisikia kuandamana kwa nia ya kuwasilisha ujumbe fulani katika nchi yao, iwe kwa nia ya kulaani au kupongeza, au iwe kwa nia ya kutaka mabadiliko au kutaka mambo yabakie kama yalivyo, ni haki yao kufanya hivyo.
Polisi katika maandamano kama haya wana kazi moja tu, kuhakikisha kwama amani inatamalaki wakati wote wa maandamano. Ni wajibu wa polisi kuweka ulinzi ili kila anayetaka kuandamana kwa amani ilimradi hamnyang’anyi wala kuingilia uhuru wa mtu mwingine, anatimiza haja yake hiyo.
Maandamano yote haya, yaani ya Mwanza ya jana na yale ya Dar es Salaam ya Februari 8, mwaka huu yameacha funzo moja muhimu kwa vyombo vyetu vya usalama; kwamba si kweli kwamba wanaotaka kuandamana wanasukumwa na kiu ya kufanya fujo, kuvuruga amani na kuleta bughudha katika nchi kama ambavyo vyombo vya usalama vimejaribu kujenga taswira hiyo potofu.
Ni kwa kutafakari na kuangalia maadamano ya jana ya jijini Mwanza na haye ya Dar es Salaam tunapata hoja ya msingi ya kuwaambia walinda usalama wetu kwamba sasa ni wakati wa kubadilika, kutambua na kukubali kwamba uendeshaji wa mambo yetu ndani ya nchi ni lazima pamoja na mambo mengine utambue uwepo wa makundi kinzani katika mambo mengi.
Kwa kuwa ukinzani huu ni halali, upo kwa mujibu wa sheria na katika kuendesha hakuna anayevunja sheria, ni vema vyombo hivyo vikaweka utaratibu wa kawaida wa kitendaji wa kusimamia makundi hayo yatekeleze kile kinachowawasha nafsini mwao. Haya ni pamoja na maandamano na mikutano ya hadhara, kutoa kauli za kuchambua na kukosoa misimamo ya kiutawala; kuandaa na kutangaza sera mbadala na zile zinazotekelezwa na chama tawala, na kwa ujumla kukubali kwamba kupingana ni haki ya msingi ya raia ilimradi hakuna sheria inayovunjwa.
Kama vyombo vya usalama vikitambua haya, hakika kelele zinazopigwa kila uchao kwamba wapo watu wanaotaka kuvunja amani kwa kuwa tu wameomba kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara, hazitakuwapo, na kwa kweli kila upande utajenga uwajibikaji kwa kile wanachopanga kufanya.
Itakumbukwa kwamba mara nyingi sababu zinazotolewa na walinda usalama wetu juu ya kutokubariki kufanyika ama kwa maandamano au mikutano ya hadhara ya wanasiasa, ni pamoja na ukosefu wa askari wa kutosha kuweka ulinzi na wakati mwingine taarifa kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani.
Imetokea watu wakakaidi maamuzi haya ya wanausalama na hivyo kufanya maandamano au mikutano ya hadhara, matokeo yake ni kutawanywa kwa jeshi kubwa la wanausalama lililojihami kwa silaha zote. Swali linakuja, hawa askari waliopatikana kwa wingi mkubwa kama huo walitoka wapi kama hapo awali ilielezwa kwamba hawapo wa kulinda amani?
Kinachoweza kuelezwa ni kitu kimoja tu, kwamba walinda usalama hawa kwa sababu zao hawapendi kufanyika kwa maandamano au mikutano hiyo; hivyo kutafuta visingizio vyepesi sana kuyakwamisha.
Tunafikiri katika mazingira ya sasa ambayo uwazi unabidi kuchukua nafasi ya usiri katika uendeshaji wa mambo katika nchi yetu, ni vema sana tukajenga utamaduni wa kuvumiliana na kutambua kwamba kila kundi katika jamii lina nafasi yake, na ni wajibu wa vyombo vya usalama kuyahakikishia makundi yote ulinzi na hadhi sawa kwa mujibu wa sheria.
Tunatambua kwamba kuna uwezekano wa kuwapo kwa watu wenye nia mbaya ya kuvuruga amani na kuvunja sheria, hao wangeshughulikiwa kama mtu mmoja mmoja, lakini si haki kuzuia makundi ndani ya jamii kufurahia haki zao za kikatiba kwa sababu ambazo hazina mashiko. Tunaamini maadamano ya Mwanza ya jana na yale ya Dar es Salaam ya Februari 8, mwaka huu yatakuwa yamesaidia kuwafungua wana usalama wetu kwamba kuandamana si kuvunja amani. Kwa maana hiyo sasa wabadilike.
CHANZO: NIPASHE

No comments: