WAKATI matokeo ya uchunguzi wa ubora wa dawa inayotolewa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile yakisubiriwa kwa hamu, mchungaji huyo amezuia kwa muda ripoti ya serikali, akitaka ikasomwe kijijini kwake Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro anakoendesha shughuli zake za tiba.
Awali, serikali ilikuwa itoe ripoti rasmi Machi 26 asubuhi, lakini taarifa iliyopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali inasema kwamba,
Mchungaji Mwaisapile maarufu kama Babu wa Loliondo, ametaka ripoti hiyo isomwe kijijini Samunge.
Kutokana na kauli hiyo ya Mchungaji Mwaisapile, shughuli za utoaji wa taarifa ilisitishwa na waandishi kuamriwa kuelekea Samunge kwa ajili ya kusikiliza ripoti hiyo ya serikali.
Akizungumzia juu ya kuahirishwa kutolewa kwa taarifa hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alisema wao kama viongozi wa serikali hawakuwa na tatizo juu ya ombi la mchungaji huyo anayedaiwa kuponya magonjwa sugu, ukiwamo ukimwi kwa kunywa kikombe kimoja tu cha dawa yake.
‘’Tumekubaliana na ombi lake na kwa sasa, mimi kama kiongozi mkuu wa serikali katika wilaya ya Ngorongoro nitamwakilisha Lukuvi (William, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, katika kutoa taarifa hiyo katika kijiji hicho cha Samunge,’’ alisema Lali.
Lakini kabla ya kutolewa rasmi kwa taarifa ya uchunguzi huo uliofanywa na Mkemia Mkuu, Serikali iliwahi kusema kuwa hadi sasa hakuna madhara yoyote yaliyoripotiwa kutokana na dawa hiyo na kuwataka wananchi kuendelea kuitumia kulingana na imani zao.
Tiba ya dawa hiyo ya Babu wa Loliondo inayodaiwa kutibu magonjwa sugu kama kisukari, moyo, saratani na Ukimwi kwa gharama ya Sh 500 tu, imeendelea kuvuta maelfu ya watu wanaokwenda kijijini Samunge wakitokea ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa uchunguzi huo umeshakamilika na taarifa ya mwisho ingetolewa wakati wowote wiki hii.
Alisisitiza kuwa wataalamu wameshafanyia uchunguzi dawa hiyo, lakini alikataa kutoa matokeo ya uchunguzi huo hadi hapo yatakapotangazwa rasmi.
Lakini kabla ya taarifa ya Dk. Nkya, Waziri mwenye dhamana ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini, Dk. Haji Mponda alisema kutokana na hofu ya hali ya usalama wa kiafya katika eneo hilo, serikali ilishachukua hatua za awali ikiwamo ya kupeleka wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kwa ajili ya kufanya uchunguzi.
Kwa mujibu wa Dk. Mponda, utaratibu wa kisheria wa utoaji wa dawa unamtaka atakayegundua dawa ya aina yoyote kufuata taratibu zilizopo ikiwamo kuthibitishwa na TDFA ili kuangalia ubora na madhara yake kwa watumiaji.
Hata hivyo, uchunguzi huo utakabiliwa na changamoto mbalimbali kwani kwa mujibu wa Mchungaji Ambilikile, dawa hiyo alioneshwa na Mungu na inahitaji imani ili ifanye kazi, jambo ambalo siyo rahisi kuthibitishwa kitaalamu kwa njia ya maabara.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment