SIKU tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuonya kile alichokiita ajenda ovu za Chadema kutaka kuvuruga nchi, jana Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa na wabunge wawili wa chama hicho wameitiwa mbaroni na polisi na kuhojiwa kwa saa kadhaa kwa madai ya kufanya mkutano wa uchochezi katika Jimbo la Maswa Mashariki.
Akituhutubia taifa katika utaratibu wake wa kila mwisho wa mwezi, Rais alionya akisema Chadema kimekuwa kikitumia fursa ya kufanya maandamano ya kidemokrasia huku wakiwa na lao jambo ambalo ni kuvuruga amani ya nchi.
Wakati mjadala wa hotuba hiyo ukiwa haujatulia, jana habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani zilisema Dk Slaa alikamatwa mnamo saa 8: 05 asubuhi kwa madai ya kufanya mkutano katika Kijiji cha Malampaka wilayani Maswa kilichopo Jimbo la Maswa Mashariki, linaloongozwa na John Shibuda. Hata hivyo, Shibuda hajashiriki maandamano yoyote ya chama chake yanayoendelea.
Wabunge waliokamatwa pamoja na Dk Slaa ni Rachel Mashishanga na Chiku Obwao ambao ni wa viti maalum. Walikamatwa na polisi mjini Kahama baada ya polisi kuzingira Hoteli ya Pine Ridge walikokuwa wamefikia wakitokea Maswa.
Kamanda Athumani alisema viongozi hao wa Chadema ambao wako kwenye mpango wao wa maandamano ya amani Kanda ya Ziwa walikamatwa wakati wakijianda kwenda Wilaya ya Bukombe kuungana na wenzao kabla ya kuelekea mkoani Kagera kuendelea na mikutano yao.
Kamanda huyo alisema juzi, Dk Slaa na wabunge hao wakiwa wilayani Maswa walifanya maandamano na baadaye kufanya mkutano wa uchochezi katika Mji wa Malampaka bila kutoa taarifa Polisi na baadaye kukimbilia wilayani Kahama ambako waliungana na wenzao.
“Kawaida ukiwa na mkutano ni lazima ufike polisi na kutueleza kuwa unataka mkutano ama maandamano na sisi tutakubaliana na wewe baada ya kuridhishwa na sababu za mkutano wako,” alieleza Kamanda huyo wa Polisi.
Alisema mkutano huo ulikuwa nje ya ratiba na barua yao kwa vile wakati wakitoa taarifa hawakueleza iwapo watafanya mkutano katika mji huo wa Malampaka.
“Walifanya mkutano huo nje ya ratiba ya kibali chao cha kufanya maandamano mkoani Shinyanga ambacho jeshi la polisi linacho hivyo ilikuwa kinyume cha taratibu na sheria, tulimfuata alipolala na kutaka kupata maelezo yake,” alisema Kamanda Athumani.
Wakiongozwa na Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Shinyanga (RCO), Kashindye Hussen polisi waliwakamata viongozi hao wa Chadema na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi ch Wilaya hatua ambayo ilisababisha wafuasi wengi wa chama hicho kumiminika hapo kujua hatma ya viongozi hao.
Kamanda Athumani katika maelezo yake alisema Dk Slaa na wenzake waliieleza polisi kwamba wao wakiwa viongozi wa juu walifanya mkutano wao kwa nia njema na kwamba walisimama hapo wakijua kuwa viongozi wao wa wilaya walikuwa na mawasiliano na polisi.
Viongozi hao wote waliachiwa kwa dhamana na Kamanda huyo alisema jeshi lake linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasaka viongozi wa wilaya ili kujua aliyehusika kuandaa mkutano huo.
Mbowe aliwaambia waandishi wa habari jana wilayani Bukombe kwamba Dk Slaa alifuatwa na ofisa wa polisi akitakiwa kufika kituoni wilayani Kahama ambako alikaa muda wa saa moja akitoa maelezo yake.
“Polisi walikuwa wakimshutumu kwa kufanya mkutano katika eneo ambalo halikupangwa, lakini Dk Slaa aliwaeleza kuwa kazi ya kuandaa mikutano siyo yake ni ya viongozi wa Wilaya ya Maswa hatua mbayo iliwafanya kumuachia na sasa tunaendelea na safari yetu ya Mkoa wa Kagera,” alisema.
Baada ya kuruhusiwa kuondoka mjini Kahama Dk Slaa aliungana na viongozi wenzake wa Chadema na jama mchana walifika katika Mji wa Kemondo mkoani Kagera ambako walipokewa na viongozi wa chama hicho wa mkoa huo na kisha kuelekea mjini Bukoba.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment