Tuesday, March 29, 2011

Dowans yatesa Tanesco, Wizara

Mvutano mkubwa umeibuka kati ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Wizara ya Fedha na Uchumi kuhusu nani kati yao anayepaswa kubeba mzigo wa deni la Sh. bilioni 94, ambazo Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) iliiamuru Tanesco kuilipa Kampuni ya Dowans Tanzania Limited kwa kosa la kuvunjiwa mkataba wake.
Mvutano huo ulidhihirika katika kikao kati ya uongozi wa Tanesco, wizara hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana. 

Chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho kilichoongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Murtaza Mangungu, zinaeleza kuwa mvutano huo uliibuka baada ya menejimenti ya Tanesco kupinga maelekezo yaliyotolewa na wizara hiyo kwamba, deni hilo liingizwe kwenye vitabu vya shirika hilo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, maelekezo hayo yanadaiwa kutolewa na wizara hiyo kupitia barua waliyomwandikia Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Chanzo hicho kimeeleza kuwa menejimenti ya Tanesco kupitia taarifa yake iliyowasilishwa katika kikao hicho, ilipinga na kutaka deni hilo liingizwe kwenye vitabu vya Serikali Kuu.
Katika taarifa yake, Menejimenti ya Tanesco inadai kuwa anayepaswa kubeba mzigo wa deni hilo ni Serikali Kuu kwa vile mkataba kati yao na Dowans ulitekelezwa na shirika chini ya maelekezo ya Serikali Kuu.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa hoja hiyo ilizua mjadala mkali na kusababisha wajumbe wa kamati kugawanyika katika makundi mawili.
Kundi moja linadaiwa kuunga mkono msimamo wa Tanesco wakati lingine liliupinga msimamo wa shirika hilo na kuunga mkono melekezo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Uchumi kwa CAG kuhusu deni la Dowans.
Kutokana na hali hiyo, POAC iliamua kutopitisha hesabu za Tanesco jana hadi hapo mwafaka kuhusu mvutano huo utakapofikiwa.
Taarifa zinasema wakati mjadala huo ukiendelea, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, aliingia ndani ya ukumbi, ambao kikao hicho kilikuwa kikifanyika kwa ajili ya kushiriki mjadala huo.
Baadhi ya wajumbe wa POAC walitoa hoja za kumzuia kushiriki kikao hicho kwa madai kwamba, si mjumbe wa kamati hiyo na kwamba, ndani ya kikao kulikuwa kukijadiliwa mambo nyeti.
Hata hivyo, Kafulila, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), aligoma kuondoka kwa maelezo kwamba, kanuni za Bunge zinamruhusu mbunge yeyote kuingia kwenye kikao cha kamati yoyote isipokuwa haruhusiwi tu kupiga kura.
Baada ya kutoa hoja hiyo, Kafulila aliruhusiwa kubaki ndani ya kikao hicho na baadaye akaruhusiwa kuchangia mjadala uliokuwa mezani wakati huo.
Akitoa mchango wake, Kafulila alisema haungi mkono mjadala huo kwa vile deni la Dowans si la halali na kwamba mjadala kuhusu kampuni hiyo ilipwe au isilipwe fedha hizo bado haujaisha.
Mzozo mkubwa kati ya baadhi ya wajumbe wa kamati na Kafulila uliibuka baada ya mbunge huyo wakati anaondoka ndani ya ukumbi wa kikao hicho, kuchukua nyaraka za Tanesco.
Wajumbe hao walipinga kwa madai kwamba, yeye si mjumbe wa POAC, hivyo akanyang’anywa nyaraka hizo.
Kafulila alipoulizwa kuhusu masaibu yaliyomkuta ndani ya kikao cha POAC jana, hakukiri wala kukanusha, badala yake aliishia tu kucheka.
Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, alithibitisha Kafulila kunyang’anywa nyaraka hizo.
Ni kweli Kafulila alinyang’anywa documents (nyaraka) kwani si mjumbe wa kamati (POAC). Ana haki kuingia, hana haki kuchukua documents,” alisema Zitto, ambaye alithibitisha pia kuwa katika kikao cha jana cha kamati yake kulikuwa na suala linalohusu Dowans.
Ni kweli pia kuna  suala la Dowans. Kamati imemuita Katibu Mkuu wa Hazina na Nishati. Kwa sasa hakuna  mzozo wowote,” alisema Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Kabla ya Zitto kuthibitisha mambo hayo, Mangungu alizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa kikao hicho na kusema kamati yake jana ilishindwa kupitisha hesabu za Tanesco.
Kwa sababu kuna masuala yanapaswa kupatiwa majibu kutoka Tanesco, Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Fedha na Uchumi,” alisema Mangungu, ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM).
Tutawaandikia barua makatibu wakuu wa wizara hizo, CAG na Tanesco ili tukutane tarehe 30 (kesho) tujadili muafaka upatikane kuhusu suala hilo,” alisema Mangungu.
Alisema mambo, ambayo yanatakiwa yapatiwe majibu ni pamoja na madeni ya Tanesco na mvutano kati yake na wizara hiyo. Mangungu alisema madeni hayo ni kati ya Sh. bilioni 67 na Sh. bilioni 96, ambayo alisema Tanesco wameamua kuyapeleka kwa kamati baada ya kushindwa kuyatolea uamuzi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake