Tuesday, March 29, 2011

Lipumba: CCM yatumia matatizo ya Watanzania kuwanufaisha wachache




Na Benedict Kaguo, Mtwara

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia matatizo yanayowakabili
wananchi kuwanufaisha watu wachache huku Watanzania walio wengi wakiendelea kupata tabu.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Mtwara katika Uwanja wa Mashujaa juzi jioni Prof. Lipumba alisema Serikali ya CCM badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi imekuwa ikitumia mwanya huo kuwanufaisha wachache.

Huku mvua kubwa ikinyesha katika uwanja wa mkutano, Prof Lipumba alisema ni jambo la kushangaza serikali inashindwa kutumia rasilimali zilizopo nchini kuzalisha umeme huku akitolea mfano uwepo wa gesi katika maeneo mbalimbali nchini kama vile Mkuranga, Mnazi Bay ,Pangani na Mto Ruvuma pamoja na makaa ya mawe wa Kiwira ili kuzalisha umeme.


“Badala yake ndugu zangu Serikali ya CCM imekuwa ikitumia matatizo ya umeme kuingia mikataba mibovu ya Dowans na kuwanufaisha vigogo wachach serikalini” alisema Prof. Lipumba.

Alisema kukosekana kwa mipango madhubuti ndio iliyosababisha nchi inaendelea kuwa na matatizo makubwa yakiwemo ya kiuchumi na kwamba badala ya kuhangaika kupata suluhisho la matatizo imekuwa ikiyatumia matatizo hayo kuwatajirisha wachache.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro alisema Serikali ya CCM imekuwa ikiendeshwa kiujanja ujanja kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi mtaa.

“Nchi inaendeshwa kiwizi wizi kuanzia huko Ikulu hadi kwa watendaji wa mitaa, serikali imekosa mipango ya kukabili matatizo ya wananchi,” alisema Bw .Mtatiro.

Alisema leo wanawake wajawazito wakifika hospitali wanapata tabu huku wakitakiwa kwenda na nyembe na kubaisha kuwa kama serikali imeshindwa kuwanunulia wembe kwenye zahanati na hospitali itawezaje kuwaletea viwanda vikubwa vya korosho wakazi wa Mtwara.

“Ndugu zangu serikali isiyoweza kununua wembe kwa mama mjamzito itawezaje kujenga kiwanda kikubwa kwa wananchi wake wa Mtwara,” alisema Bw. Mtatiro.


CHANZO:MAJIRA

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake