
SIMBA ya Dar es Salaam imetamba itaifunga TP Mazembe na kuitupa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa timu hiyo haitishi.
Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki katika michezo ya kimataifa ngazi ya klabu, wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 watakaporudiana na TP Mazembe mwishoni mwa wiki ili wasonge mbele katika michuano hiyo.
Hatua hiyo inatokana na kipigo cha mabao 3-1 ilichokipata juzi kutoka kwa TP Mazembe katika mchezo wa kwanza raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika Uwanja uitwao Stade de La Kenya mjini Lubumbashi.
Akizungumza baada ya mchezo huo mjini hapa, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema kiwango kilichooneshwa na wapinzani wao si kama walivyotarajia kwani kilikuwa cha chini licha ya kwamba ilishinda.
Kutokana na hali hiyo, Rage alisema wanaamini watashinda mechi ya marudiano itakayofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
“Hawa sisi tutawafunga nyumbani (Dar es Salaam), tumeshawasoma na pia kiwango chao sasa hivi hakitishi,” alisema Rage aliyeongoza msafara wa Simba mjini hapa uliokuja na ndege maalum Jumamosi asubuhi na kuondoka Jumapili mara baada ya mchezo kumalizika.
Naye Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri amesema mabao waliyofungwa ni ya kawaida na kuwa wanajipanga kushinda Dar es Salaam. Phiri hakurudi na timu juzi, aliunganisha kwenda kwao Zambia.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa TP Mazembe, Mamadou Ndiaye alikiri kupata upinzani mkubwa ambao hawakuutarajia kutoka kwa Simba.
Akizungumza baada ya mechi, Ndiaye alisema alitarajia Simba ni kama timu nyingine zinazoenda Lubumbashi kucheza na Mazembe, lakini hali imekuwa tofauti.
“Tumeshinda lakini tumecheza na timu nzuri, sikutarajia kupata upinzani kiasi kile, timu yao nzuri.
“Kipindi cha kwanza hawakucheza vizuri sana, lakini kipindi cha pili hasa dakika za mwisho walibadilika sana, nikahisi wanaweza kusawazisha na hasa walipopata bao,” alisema kocha huyo.
Bao la Simba lilifungwa dakika ya 76 na Emmanuel Okwi kwa mkwaju wa penalti, wakati huo ikiwa tayari imefungwa mabao hayo matatu.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment