.jpg)
Wakati makocha wa timu za taifa za Tanzania na Jamhuri ya Afrika ya Kati watazungumza na waandishi wa habari leo kuhusu mechi yao ya Jumamosi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (CAN) 2012, kambi ya wageni imesema inajipanga namna ya kukabiliana na winga Mrisho Ngassa wa Taifa Stars, huku ikishangaa kutojumuishwa kikosini kwa Mussa Hassan 'Mgosi'.
Taarifa ya TFF ilisema jana kuwa kocha Jan Poulsen wa Stars na Jules Accorsi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati watakutana na waandishi leo saa 5:00 kwenye ukumbi wa Shirikisho hilo la Soka Tanzania, lakini kambi ya wageni inaonekana inajiandaa kucheza kwa tahadhari sana mechi ya Jumamosi.
Kwenye mazoezi yao ya jana asubuhi, wachezaji wa timu hiyo ambao wana maumbo makubwa walionekana makini na wanachokifanya na wakati wa mapumziko walikuwa wakitaniana.
Kocha wao, Accorsi alisema kikosi chake kinaundwa na wachezaji vijana na kwamba mwenye umri mkubwa zaidi ana miaka 27 wakati kipa wao chaguo la kwanza ana umri wa miaka 22.
Alisema japo hawezi kusema kama watashinda mechi hiyo "kwa vile mpira ni dakika 90", wamejiandaa vyema na waliweka kambi yao katika nchi za Ulaya.
Accorsi alisema kikosi chake kinaundwa na wachezaji wanne tu wanaocheza soka katika ligi kuu yao ya ndani, wakati sita wanatoka nje ya Afrika na waliobaki wanacheza soka katika nchini mbalimbali za Afrika, akiwemo mmoja anayekipiga katika klabu bingwa ya Afrika, TP Mazembe.
Akizungumza kwa lugha ya Kifaransa huku akimtumia mkalimani meneja mkuu wa timu hiyo, Willy Kongo, anayezungumza Kiingereza, Accorsi alisema anatarajia mechi ngumu Jumamosi kwa sababu Tanzania watashuka uwanjani wakijua kwamba ni lazima washinde kwani kama hawatashinda, watakuwa wamejimaliza.
Meneja Willy Kongo alisema hawaifahamu vyema Stars lakini wanajua makali ya winga
Mrisho Ngassa na Mussa Mgosi, ambao waliwaona katika mechi dhidi ya Brazil, Algeria na Morocco.
Hata hivyo, meneja huyo alisikitishwa kukosekana kwa Mgosi kikosini. "Kama Mgosi ameachwa, basi walioitwa inawezekana ni wakali zaidi yake na mechi itakuwa ngumu sana," alisema Kongo.
Kongo pia aliponda dimba la nyasi bandia la Uwanja wa Karume waliopangiwa kwa ajili ya mazoezi yao, akisema sio mzuri na umewapa taabu sana huku akisisitiza kuwa nyasi bandia zinapingwa sana duniani.
Wakati huo huo, Taifa Stars inatarajiwa kumkosa kiungo wake Nizar Khalfan baada ya uongozi wa klabu yake ya Vancouver Whitecaps kugoma kumruhusu kwa maelezo kwamba TFF haikufuata taratibu katika kumuomba mchezaji huyo.
Uongozi wa klabu hiyo unadai kuwa TFF iliandika barua iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawembwa na kutumwa kwa Nizar mwenyewe na nakala kupelekewa kwa uongozi wa klabu, jambo ambalo ni kinyume na taratibu. Uongozi huo unadai kuwa wao ndio waliopaswa kuandikiwa barua hiyo ili wamruhusu mchezaji huyo kuja kuichezea Stars, kama ambavyo umekuwa ukimruhusu mara zote.
Alipoulizwa Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura juu ya suala hilo alikiri kwamba ni kweli TFF ilimwandikia barua mchezaji husika kwa kuwa aliomba ifanywe hivyo na nakala yake ilitumwa kwa viongozi wake.
"Wachezaji wenyewe wanaomba tunapoandika barua kwa klabu zao kuwaomba kuja kuchezea timu ya taifa tuwapatie nakala na wao ili waweze kuzitumia kuweka msisitizo wa kupata ruhusa na ndivyo TFF tulivyofanya," alisema Wambura.
Alisema kuwa wanaamini mchezaji huyo atawasili nchini leo kujiunga na wachezaji wengine wa Stars na ikishindikana watalipeleka suala hilo FIFA, Shirikisho la soka la kimataifa.
Jamhuri ya Afrika ya Kati inaongoza msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi 4 baada ya mechi mbili, ikifuatiwa na Morocco (pointi 4), Tanzania (1) na Algeria (1).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment